Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-09-06 20:34:32    
Mwimbaji Mashuhuri wa Kike wa China Guan Mucun

cri

    Siku chache zilizopita, baadhi ya wasanii wa China walipewa "sifa za usanii mkubwa na uadilifu wa kuigwa", mwimbaji mashuhuri Guan Mucun alikuwa miongoni mwao. Siku moja, mwandishi wetu alipata nafasi kuzungumza naye.

    Guan Mucun alisema, "katika miaka yote niliyopitia maisha yangu yamejaa milima na mabonde, na wakati fulani hali yangu ilikuwa ngumu sana. Sifa ninazopewa, kwangu ni mwanzo mpya. Kwa moyo wangu safi nitawashukuru watazamaji wenzangu kwa kujiendeleza zaidi na kuimba nyimbo nyingi zaidi."

    Guan Mucun alizaliwa mwaka 1953 mkoani Henan, baadaye alihamia kwenye kitongoji cha mji wa Tianjin. Baba yake alikuwa mhariri wa jarida moja, na mama yake alikuwa ni mpenda muziki. Kutokana na kuathiriwa na mama yake, tangu utotoni mwake Guan Mucun alipenda muziki. Lakini bahati mbaya alipotimiza miaka 10 alifiwa na mama yake, na wakati huo China ilikuwa katika kipindi cha msukosuko wa "mapinduzi ya utamaduni", Guan Mucun hakuweza kuendelea na masomo yake ya sekondari ya juu, alipaswa kuwa mfanyakazi wa kiwandani.

    Kazi ya kiwandani ilikuwa ngumu, hata hivyo hakuacha kupenda muziki, alitumia muda wake wa mapumziko kujizoeza uimbaji. Nyuma ya kiwanda kulikuwa na ziwa moja kubwa, kila asubuhi na mapema Guan Mucun alifanya mazoezi ya kuimba mbele ya ziwa hilo. Vivyo hivyo uimbaji wake ulikuwa unaendelea sana hata akawa mwimbaji nyota mdogo hapo kiwandani, kila kiwanda kilipofanya tamasha alialikwa kuimba, na kila baada ya kuimba hakukosa kupigiwa makofi kwa nguvu. Maisha yake katika kipindi hicho imekuwa ni kumbukumbu yake daima.

    Mwaka 1978, China ilianza kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango kiuchumi, na usanii wa Guan Mucun pia ulipata kipindi kizuri. Aliacha kazi kiwandani na kujiunga na Kundi la Nyimbo na Dansi mjini Tianjin, na kuwa mwimbaji wa kulipwa. Katika muda wa miaka mitano hivi, kwa sauti yake inayovutia alikuwa akisafiri huku na huko nchini China na nyimbo zake. Mwanamuziki mashuhuri Li Delun alimsifu kuwa sauti yake inafanana na sauti ya fidla kubwa, na ni nadra kuipata duniani."

    Mwaka 1984 Guan Mucun alijiunga na kozi ya uimbaji katika Chuo Kikuu cha Muziki cha China. Katika chuo hicho aliwahi kujifunza uimbaji wa Kimagharibi. Aliunganisha pamoja uimbaji wa Kichina na wa Kimagharibi na kupata mtindo wake mwenyewe.

    Katika miaka ya 80 alirekodi wimbo wa "Mwezi Wachomoza Baharini" kwa ajili ya filamu na baadaye aliimba nyimbo kwa ajili ya filamu nyingine zaidi ya kumi. Aliwahi kupata tuzo nyingi na mara nyingi alifanya maonesho yake ya nyimbo na aliwahi kwenda Uingereza, Ireland, Japan na nchi nyingine kufanya maonesho ya nyimbo za kikabila na alishangiliwa sana.

    Mwimbaji Guan Mucun ni mtu mnyekekevu, anaona kwamba sifa zake zote zinatokana na watazamaji wake wanaompenda. Alisema, "Mapenzi na heshima wanazonipa wasikilizaji wenzangu kamwe hazitafutika akilini mwangu."

    Mbali na kuimba, Guan Mucun anajitahidi kadiri awezavyo kushiriki katika harakati za kuwasaidia watoto wenye shida ya kiuchumi ili wapate masomo shuleni, katika muda wa miaka 15 aliwasaidia watoto kumi kadhaa mpaka wakamaliza masomo ya sekondari, na mara nyingi alishiriki katika maonesho ya kuchangisha fedha ili kuwasaidia watu waliokumbwa na maafa ya kimaumbile.

    Maishani, Guan Mucun ni mtu mpole, anapenda kusoma, kutalii na kuwasiliana na marafiki. Mume wake ni msomi na wanapendana sana. Alisema, "Mume wangu ni mwalimu wangu, mara kwa mara ananielimisha. Anapenda kusoma, na kuwasiliana na marafiki. Anasoma vitabu vya elimu mbalimbali."

    Hivi sasa Guan Mucun anahariri nyimbo zilizotungwa na mtunzi maarufu wa nyimbo, Shi Guangnan. Marehemu Shi Guangnan pia alikuwa mwalimu wake, alimtungia Guan Mucun nyimbo nyingi ambazo zinajulikana miongoni mwa wananchi wa China. Guan Mucun alisema, "Sasa nimekuwa nikihariri nyimbo alizotunga Shi Guangnan, na nitazifanya ziwe za kuwapendeza vijana na kuwatia moyo wa kujiendeleza, hili ni tumaini langu."

Idhaa ya Kiswahili 2004-09-06