Ziwa Qiandao liko katika mkoa wa Zhejiang ulioko pwani ya mashariki ya China. Sehemu hiyo yenye vivutio vya utalii inawapendeza sana watu kutokana na maji yake safi ya kijani, visiwa vya kijani, mandhari yake nzuri ya kijani. Baada ya kutembelea sehemu hiyo, mioyo ya watalii huwa inajaa usafi wa rangi ya kijani.
Ziwa Qiandao liko umbali wa kilomita 150 kutoka Hangzhou, mji mkuu wa mkoa wa Zhejiang, kwa maana ya kichina, Ziwa Qiandao ni ziwa la visiwa 1000. Kwenye ziwa hilo, mbali na maji, hakika watalii wanaweza kuona visiwa vikubwa na vidogo vingi mbalimbali vilivyotapakaa kwenye ziwa, visiwa hivyo vyenye maumbo tofauti vinaonekana kuwa ni vivutio vinavyoweza kugusa hisia za watu na kuwawezesha wapate taswira kuhusu maumbile mbalimbali, ndiyo maana watalii huwa wanajihisi kama wanaota ndoto nzuri.
Tulipanda meli kutembea kwenye ziwa, njiani mwongozaji wetu akitufahamisha alisema:
Ziwa Qiandao lilijengwa mwishoni mwa miaka ya 50 ya karne iliyopita kutokana na ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji, kwa lengo la kulimbikiza maji. Eneo la ziwa ni kilomita 573, hilo ni ziwa kubwa kabisa la maji baridi katika sehemu ya mashariki ya China. Katika eneo hilo kuna visiwa 1078 vya aina mbalimbali, hivyo ziwa hilo lilipewa jina la Ziwa Qiandao yaani ziwa la visiwa elfu moja.
Ziwa hilo lina maji safi sana ambayo yanaonesha rangi ya kijani au kibuluu kama rangi ya maji ya bahari inavyobadilikabalika. Maji yake ni safi na matamu sana.
Bwana Yu Guofu alituambia kuwa, maji safi na matamu ya ziwa hilo yanatokana na hali yake ya kiasili na vilevile kutokana na utunzaji wa watu. Watu wanaoishi kando ya ziwa wanalinda usafi wa maji ya ziwa hilo, kama wanavyolinda mboni za macho yao wenyewe. Bwana Yu akisema:
Maji ya ziwa Qiandao ni masafi sana. Ukitazama kwenye maji utaweza kuona ndani hadi kina cha mita 9 na 12. Maji yake masafi yanasifiwa kuwa ni maji bora ya No.1 duniani, ni maji ya ngazi ya kwanza ya kitaifa. Maji hayo yanaweza kunywewa moja kwa moja, na watu wakiogelea kwenye ziwa hilo wanapata burudani safi ya ajabu.
Katika eneo la ziwa Qiandao, pia kuna sehemu mbalimbali zinazoonesha historia na utamaduni wa eneo hilo, pamoja na hekalu la dini ya Ki-Buddha.
Wakazi wa eneo hilo wanaoishi kando ya ziwa katika hali ya utulivu, wanahifadhi mji wa kale ulioko chini ya ziwa. Bwana Zhang Zhipeng alituambia kuwa, mwanzoni mwa miaka ya 50 ya karne iliyopita, lilipojengwa Ziwa Qiandao kwa ajili ya kujenga kituo cha kuzalisha umeme, maji yalipolimbikizwa mji wa kale ulizama. Sasa mji wa kale uliopo chini ya mita 25 ya ziwa hilo, na bado unaonekana kikamilifu bila kuharibika karibu miaka 50 imepita, hata kuta za miji zilizojengwa kwa mawe na matofali bado zipo, na milango mitatu iliyogunduliwa bado ni imara, miongoni mwa milango hiyo mlango wa magharibi bado unaweza kufunguka. Na baadhi ya nyumba, nguzo za nyumba, ngazi na kuta bado zimesimama bila kuoza. Katika nyumba kadhaa kubwa, ndani hata samani zinaonekana kama zilivyowekwa katika zama za kale.
Bwana Zhang alisema kuwa, hivi sasa sehemu hiyo inafanya maandalizi ya kuanzisha shughuli za utalii katika mji wa kale ulioko chini ya ziwa, ili kufanya utafiti kuhusu hali ya ajabu katika mji huo wa kale uliozamishwa.
1 2 3
|