Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-09-16 18:33:55    
Shanghai yasaidia kusukuma mbele maendeleo yenye uwiano ya uchumi wa China katika sehemu ya magharibi na mashariki kwa miradi ya sayansi na teknolojia

cri

    Ili kuunganisha teknolojia ya sehemu ya mashariki na maliasili ya sehemu ya magharibi ya China na kusukuma mbele maendeleo yenye uwiano ya uchumi wa China katika sehemu hizo mbili, hivi karibuni kamati ya sayansi na teknolojia ya Shanghai ilianzisha miradi 75 ya sayansi na teknolojia ili kuharakisha maendeleo ya uchumi wa sehemu ya magharibi.

    Ofisa husika wa kamati hiyo alieleza kuwa, miradi hiyo ikiwemo miradi ya teknolojia za upashanaji habari, upandaji wa mazao ya kilimo, ufugaji wa samaki na chura wa misituni, ufungaji wa nyama za njiwa, upasuaji wa mbao, upimaji wa bidhaa za miti, kukinga na kutibu tezi, kutengeneza nyaya za kupeleka umeme, na kubadilisha nguvu ya umeme itaanzishwa katika mikoa kadhaa ikiwemo Yunnan, Chongqing, Tibet na Ningxia kwa kushirikiana na idara husika za huko. Mpaka sasa, Shanghai imeanzisha miradi 133 katika mikoa 13 ikiwemo Xinjiang, Gansu, Shanxi, Sichuan na Mongolia ya ndani, na jumla ya uwekezaji umefikia yuan za renminbi milioni 330.

    Ili kuondoa pengo kubwa kati ya kiwango cha uchumi wa sehemu ya mashariki na magharibi, katika miaka mitano iliyopita, Shanghai ilianzisha miradi 500 na kuwekeza yuan za renminbi milioni 38 kwa maendeleo ya uchumi wa sehemu ya magharibi. Hivi sasa ujenzi wa nusu ya miradi hiyo umekamilika, na miradi ipatayo mia 2 imeanza kufanya kazi na kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo yenye uwiano ya uchumi wa sehemu ya mashariki na magharibi nchini China.

    Mapato kwa baadhi ya wakulima yalianza kuongezeka na wameanza kuondokana na umaskini. Sehemu ya mashariki ya mlima wa Helan mkoani Ningxiang ni sehemu nzuri kwa kilimo cha zabibu ya kutengenezea mvinyo, lakini kutokana na ukosefu wa teknolojia husika, wakulima wa huko hawajui la kufanya. Shirika moja la Shanghai liliwekeza yuan milioni 19 kujenga kituo cha kupanda zabibu na kiwanda ambacho kinaweza kuzalisha tani 3000 za mvinyo kwa mwaka katika sehemu ya Yuquanying iliyoko mashariki mwa mlima wa Helan kwa teknolojia ya kupanda aina nzuri ya zabibu na kutengeneza mvinyo, na limeanza kupata faida kuanzia mwaka 2002. Hivi sasa, wakulima zaidi ya mia 6 wa huko wanafanya kazi katika shirika hilo, na wastani wa pato kwa kila mkulima umeongezeka kwa yuan 500. Jangwa la zamani limebadilishwa kuwa mashamba ya zabibu. Katika sehemu ya Rikaze mkoani Tibet kuna miradi zaidi ya 40 ya Shanghai, na asilimia 80 ya miradi hiyo imetoa mchango kwa kuongeza mapato kutokana na kilimo na ufugaji. Mradi wa kuzuia mvua ya mawe kwa radar unaweza kupunguza hasara kwa yuan milioni 6.5 kwa mwaka.

    Kuboreshwa kwa mazingira kunaweza kutoa uungaji mkono wa kiteknolojia kwa maendeleo endelevu ya sehemu ya magharibi. Teknolojia ya kuotesha nyasi kwenye mabua iliyogunduliwa na chuo kikuu cha Donghua inawezesha nyasi kukua kwenye jangwa baada ya kuoteshwa kwa mwezi mmoja tu. Majaribio ya teknolojia hiyo yamefanikiwa katika hekta 4 za jangwa lililoko katika mbuga wa Hulunbeier na kuongeza maeneo yenye nyasi katika mbuga huo ambao asilimia 38 ya ardhi imebadilika kuwa jangwa. Teknolojia moja ya kibiolojia iliyovumbuliwa na Chuo kikuu cha ualimu cha huadong cha China inawawezesha watu kutengeneza "flavone" ambayo ni dawa yenye thamani kubwa kwa kutumia masalio ya matunda ya seabuckthorn baada ya kukamuliwa mafuta. Mongolia ya ndani imeanza kutumia teknolojia hiyo na viwanda vya kutengeneza "flavone" vimejengwa. Kutokana na kuanzishwa kwa mradi huo, eneo la mashamba ya seabuckthorn limeongezeka kuwa hekta laki moja na elfu 20, na mapato ya familia zipatazo laki 2 yameongezeka, kwa wastani pato la kila familia kwa mwaka limeongezeka na kuwa yuan elfu 9. Seabuckthorn ya hekta 1 inaweza kuzuia tani 660 za mchanga usihame na asilimia 75 ya maji ardhini yasipoteze, hivyo ina athari nzuri kwa mazingira ya mkoa wa Mongolia ya ndani.

Idhaa ya Kiswahili 2004-09-16