Wenzhou ni mji wa kale uliostawi kibiashara tokea miaka 1300 iliyopita, lakini ustawi wake umekuwa mkubwa zaidi katika miaka 20 ilipita kutokana na China kufanya mageuzi. Mji huo unajulikana sana kwa sanaa za mikono na bidhaa zake zilizoenea kote nchini China. Huu ni mmoja kati ya miji inayostawi ya China.
Ukitembea barabarani na vichochoroni utaona maduka yalijaa yakionesha ustawi wa biashara mjini humo. Kama miji mingine ilivyo, pamoja na uchumi unavyoendelea, sura ya mji pia inabadilika haraka, sasa kuna majumba marefu, barabara pana zinazofika kila mahali, uwanja mkubwa na jumba la makumbusho.
Licha ya kuona kuwa huu ni mji wa kisasa, utagundua pia utamaduni wake mkubwa wa kale. Katikati ya mji huo kuna barabara iliyostawi zaidi kibiashara, hii ni barabara ya Wuma. Majumba yenye usanifu wa Kiulaya katika barabara hiyo yamekuwepo kwa miaka zaidi ya mia moja lakini bado yaonekana kuwa na uzuri wake. Ukiingia vichochoroni kutoka kwenye barabara hiyo utaona karakana nyingi ndogo za kazi za mkono, na ufundi wa kazi unaendelea kuwa wa kijadi. Ingawa karakana hizo ni ndogo lakini vitu vya sanaa vinavyotengenezwa humo ni safi sana na vya bei nafuu.
Karakana hizo ndogo ndogo ni alama ya mji huo na vitu vya sanaa vilivyotengetezwa huko kwa mikono vimeupatia mji huo umaarufu. Vinyago na utarizi mjini Wenzhou ni sanaa za mkono zinazojulikana nchini China na zinavutia watalii.
Sanaa ya utarizi ilianzia miaka mingi iliyopita, mapema katika karne ya 17 sanaa ya utarizi ilipamba moto, kulikuwa na mafundi wa kike kiasi cha mia nane kwenye maduka ya utarizi.
Picha zilizotariziwa, mbali na maua, ndege, visura, na farasi wanaokimbia pia kuna picha za Ulaya zilizochorwa. Ukienda kwenye barabara ya Wuma na Wuqiao hutakosa kuzipata sanaa hizo madukani.
Vinyago vya Wenzhou vinachongwa kwa mbao ngumu yenye rangi ya manjano. Kutokana na mti wa aina hiyo unakua taratibu sana, mbao zinazofaa kuchonga vinyago vikubwa ni shida kupatikana. Mchonga vinyago Bw. Ye Xiaoquan alisema,
"Kutokana na shida ya kupata mbao kubwa, vinyago vyetu huwa ni vidogo, kuanzia miaka ya 80 ya karne iliyopita tulianza kuagiza mbao kutoka sehemu nyingine, tulipoanza kuchonga vinyago vikubwa kwa ukubwa wa mbao."
Madukani kuna mitindo miwili ya vinyago, moja ni mtindo wa kiasili ambao unfalingana na vitu vilivyoigwa. Vinyago vya mtindo huo vinachongwa kwa makini hata pindo za nguo zinaonekana vizuri. Vinyago vya mtindo mwingine vinachongwa kwa kutiwa chumvi, ambavyo vinachongwa kwa kuonesha hisia tu na vitu vilivyoigwa vinatiwa sana chumvi. Fundi mzee Gao Gongbo alisema,
"Mtindo wa kwanza unafuatilia mfananisho wa vitu halisi, huu ni mtindo wa kijadi. Mtindo wa pili unafuatilia mfananisho wa kijujuu na kutiwa sana chumvi, huu ni mtindo wa kisasa."
Picha nyingine husika >>>
1 2
|