Hapo kale, kwenye ukingo wa bahari ulikuwapo mlima mmoja, unaitwa Laoshan, ambako aliishi kuhani mmoja. Inasemekana kwamba kuhani huyo wa Mlima Laoshan alikuwa na uganga wa ajabu.
Kutoka Mlima Laoshan umbali wa kiasi kama kilomita mia moja hivi ulikuwapo mji mkuu wa wilaya ambapo aliishi mtu mmoja, aliyejulikana kama Wang Qi. Wang Qi alikuwa na hamu ya kupata uganga tangu utotoni mwake. Baada ya kusikia fununu kuhusu uganga wa kuhani wa Mlima Laoshan, Wang Qi alimuaga mkewe na kuelekea mlimani kumtafuta ili apate uwezo huo wa ajabu kama wake.
Wang Qi alimkuta kuhani na kutokana na mazungumzo yao alibaini kuwa ni kuhani kweli mwenye uwezo mkubwa usio wa kawaida. Basi akamwomba awe mwanafunzi wake. Kuhani wa Mlima Laoshan alimchunguza, kisha akamwambia, "Nakuona wewe ni mtu wa kulelewa kwa kiganja cha mkono, nahofia hutawezana na maisha magumu." Wang Qi alizidi kumwomba na kumsihi hadi mwishowe akamkubalia.
Usiku huo Wang Qi alipoangalia mbalamwezi kutoka dirishani, moyo wake ulilipuka kwa furaha akifikiri kuwa baada ya siku chache atakuwa mtu asiye wa kawaida kama yeye. Asubuhi ya siku ya pili alidamka mapema, alimkimbilia kuhani wa Mlima Laoshan kwa matumaini atafundishwa uganga, badala yake aliambiwa achukue shoka aende mlimani kutema kuni pamoja na wanafunzi wenzake. Wang Qi aliondoka na karaha rohoni. Pale mlimani kulikuwepo mawe na kokoto nyingi, vichaka na miiba, ambavyo vilimfanya kutokwa na malengelenge mikononi na miguuni kabla jua halijazama.
Muda ulipita haraka kama mshale, mwezi mmoja ulipita vivyo hivyo, malengelenge yakawa sugu, lakini Wang Qi hakufundishwa lolote kuhusu uganga. Alishindwa kuvumilia zaidi kazi ya sulubu ya kukata kuni siku nenda siku rudi, hivyo wazo la kurudi nyumbani likamjia kichwani. Siku moja jioni alirudi kwenye hekalu la kuhani pamoja na wenzake ambapo kutoka dirishani alimwona mwalimu wake na wageni wawili wakinywa pombe pamoja kwa furaha pembeni mwa meza. Wakati huo giza lilikuwa limekwishaingia, lakini chumbani hakukuwashwa taa, na hapo ndipo alipomwona mwalimu wake akichukua karatasi nyeupe akaikata duara kama mwezi mpevu, akabandika ukutani; punde si punde ile duara ikatoa mwanga kama mwezi ukiangaza kote chumbani kama mchana.
Wang Qi aliingiwa na mshangao, na wakati huo huo alisikia mmoja wa wageni akinena, "Katika usiku mzuri kama huu wa karamu kubwa na pombe, inafaa tuburudike pamoja na wenzetu." Basi kuhani wa Mlima Laoshan akawapa kuzi dogo la pombe wanafunzi wake, akiwaambia wanywe kwa uwezo wao. Wang Qi aliwaza: kuzi dogo kama hili lawezaje kuwatosheleza wote hawa? Lakini ajabu ni kwamba hata kuzi likimwagwa namna gani pombe ilikuwa haipungui. Wakati huo mgeni mwingine akasema, "Ingawa kuna mbalamwezi na pombe, lakini bila mcheza ngoma furaha yetu haikamiliki." Kusikia hayo, kuhani alichukua kijiti kimoja cha kulia na kukielekeza kwenye ile duara, na mara akatoka msichana mmoja mwenye kimo cha futi moja lakini alipokanyaga sakafu papo hapo akawa na urefu wa kawaida. Msichana huyo alikuwa na kiuno chembamba kama nyigu, ngozi laini kama yavuyavu, na tepe za nguo zikipepea alipocheza ngoma na wimbo. Baada ya kumaliza wimbo wake akarukia juu ya meza akarudia hali ya awali ya kijiti. Yote hayo yalimwacha Wang Qi mdomo wazi.
Wakati huo mgeni mmoja akasema, "Leo ni leo asemaye kesho ni mwongo, tumefurahi kweli, lakini inatupasa tuondoke sasa." Basi wageni wawili wakainuka, wakaingia kwenye ile duara ukutani, wakatoweka. Mwanga wa mwezi wa karatasi ukafifi, wanafunzi wakawasha taa, wakamwona mwalimu kuhani akiwa peke yake na masalio ya pombe na vitoweo mezani.
Mwezi mwingine ukapita tena, lakini mwalimu hakumfudisha Wang Qi lolote. Hapo Wang Qi alishindwa kabisa kuvumilia, akaenda kwa mwalimu wake, akamwambia, "Mimi nimekuja kutoka mbali, kama hunifundishi uganga wako wa kuishi milele, basi nifundishe uganga mwingine angalau kidogo nipate kitulizo." Lakini mwalimu alitabasamu tu bila neno. Wang Qi akaendelea, "Kutema kuni toka asubuhi mpaka jioni, kazi ya nguvu kama hii siiwezi." Hapo mwalimu kuhani akacheka na kusema, "Si nilikuambia, hutayaweza maisha magumu? Kama ni hivi basi rudi nyumbani kwenu kesho asubuhi." Wang Qi akamsihi, "Naomba unifundishe uganga angalau kidogo nisirudi mikono mitupu". Mwalimu akamwuliza, "Unataka uganga gani?" Wang Qi akanena, "Mara nyingi nilikuona ulipotembea hukuzuiliwa na ukuta, nifundishe uganga huu basi." Mwalimu akakubali, akamwambia Wang Qi amfuate. Walikwenda penye ukuta mmoja. Mwalimu akamwambia maneno ya kunuizia ili aweze kupita kwenye ukuta. Wang Qi alirudia kama aliyoambiwa, na alipoimaliza tu mwalimu alinyoshea kidole ukutani akimwambia Wang Qi "Ingia ukutani." Wang Qi hakuthubutu kusogeza mbele miguu yake kwenye ukuta. Mwalimu akamhimiza, "Ingia tu!" Wang Qi alijivuta hatua kadhaa mbele kisha akasimama kwa hofu. Mwalimu alimhimiza tena, "Inamisha kichwa, uingie ndani." Wang Qi alijikakamua, akaukimbilia ukuta akiwa amefumba macho kwa nguvu. Bila kuhisi chochote akapita! Wang Qi alifurahi sana, mara akapiga magoti sakafuni kumshukuru. Mwalimu akamwambia, "Jihadhari vizuri utakapokuwa nyumbani, uwe mwenye juhudi za kazi. La sivyo, uganga hautafanya kazi yoyote."
Baada ya kufika nyumbani Wang Qi alimwelezea mkewe mambo mengi ya kujisifu akisema, "Nilimkuta mtu wa mungu, akanifundisha uganga wote. Sasa kuta zote haziwezi kunizuia nisipite." Mkewe hakumwamini, akamwambia "Acha, unamzuga nani? Jambo kama hili halipo duniani." Kusikia hayo Wang Qi alianza kunuizia, kisha akaukimbilia mbio ukuta. Pu! Akabamiza kichwa ukutani, akuanguka chali. Mkewe alimsaidia kunyanyuka, akajikuta kichwa chake kimevimba kama yai. Wang Qi alining'iniza kichwa kama puto lililovuja hewa. Alivyoona jinsi mumewe alivyoadhirika, mkewe hakujua acheke au akasirike, alisema, "Hata uganga ungekuwepo duniani, mtu mjinga kama wewe usingaliweza kuupata kwa muda wa miezi miwili, mitatu." Wang Qi alikumbuka wazi jinsi alivyopita ukuta bila shida yoyote mbele ya mwalimu wake, hivyo akaona hakika yule kuhani alimchezea shere, akaanza kulaani na kutoa matusi.
Wang Qi aliendelea kuwa mtu asiyefaa kwa lolote.
Idhaa ya Kiswahili 2004-09-30
|