Kuanzia miaka ya 80 ya karne iliyopita, kijiji cha Huaxi kilitangulia kuwa kijiji chenye simu, nyumba nzuri, magari na kompyuta nchini China, na kinasifiwa kuwa ni kijiji cha kwanza duniani. Kufuata njia ya kujiendeleza kwa pamoja ndiyo siri ya maendeleo ya kijiji hicho.
Tarehe 8 Septemba mwaka 2004, kiongozi wa mji wa Jiangying alitangaza kuanzishwa kwa kijiji namba 11 cha Huaxi. Tokea mwezi Juni mwaka 2001, kijiji cha Huaxi kilianza hatua yake ya kuviunganisha vijiji vilivyo karibu nacho, ili kupata maendeleo ya pamoja. Huaxi ya leo ina vijiji 11, eneo lake limepanuka na kuwa na kilomita 29 za mraba, idadi ya watu imefikia elfu 28,600. Mwaka huu, thamani ya jumla ya uzalishaji ya Huaxi ni zaidi ya yuan za Renminbi bilioni 20.
Kijiji cha Huaxi kinafuata utaratibu maalum wa kuviunganisha vijiji jirani, yaani kampuni zitengenishwe na vijiji, usimamizi wa pamoja wa uchumi, matumizi pamoja ya makada na nguvukazi, utoaji wa pamoja wa huduma za umma, na mpango wa pamoja wa ujenzi wa vijiji. Katibu wa chama cha kikomunisti, ambaye pia ni meneja mkuu wa kundi la Huaxi bwana Wu Xieen alisema kuwa, kuviunganisha vijiji jirani kuna lengo la kuongeza nguvu mpya, hatua hii imetoa mchango mkubwa katika kuleta thamani kubwa ya uzalishaji mwaka huu na maendeleo ya baadaye.
Kijiji cha Huaxi kilipoanzishwa mwaka 1961, mashamba yake yenye ekari 120 hivi yaligawanywa kuwa vipande zaidi ya 1200. Hivi sasa, eneo la Huaxi limeongezeka mara 29, na idadi yake ya watu imeongezeka mara 17. Katibu wa zamani wa Huaxi Bwana Wu Renbao alisema kuwa, lengo la Huaxi kuviunganisha vijiji jirani ni kuwaendeleza wanavijiji wote katika miaka 3 ijayo. Alisema kuwa, kuendelea kwa mtu binafsi si jambo gumu, lakini kuendelea kwa watu wote wa vijiji vya Huaxi hata wa China nzima ndiyo maendeleo ya kweli. Katika miaka 2 iliyopita, kijiji cha Huaxi kimegharamia yuan za renminbi zaidi ya milioni 74 katika miradi mbalimbali ya madaraja na barabara kwa vijiji jirani na kwa huduma za wanavijiji. Kimefanya semina zaidi ya 100 kwa mikoa zaidi ya 20 nchini China, na kuwaandaa makada elfu kumi na zaidi, pia kimewaongoza watu laki moja kuondokana na umaskini.
Bwana Wu alisema kuwa, katika miaka mingi iliyopita, kijiji cha Huaxi kimewavutia watu zaidi ya 2000 wenye utaalamu mbalimbali kutoka nchini China na ng'ambo, vijana wa kijiji hicho waliosoma nje wote wamerudi kijijini baada ya kuhitimu masomo yao.
Mafanikio yaliyopatikana katika kijiji cha Huaxi yanatokana na kufuata njia ya kuwaendeleza watu wote kwa hali na mali. Sasa kijiji cha Huaxi kina mali za umma zenye thamani ya yuan za renminbi bilioni 3, pato la wastani kwa kila mkazi wa kijiji kiini cha Huaxi limefikia milioni moja. Wanakijiji wote siku zote wanashikilia moyo wa kupenda chama cha kikomunisti cha China, taifa la China na kijiji cha Huaxi, kuwapenda jamaa, marafiki na wao wenyewe. Katibu Wu Xieen alisema kuwa, sasa kijiji cha Huaxi kinafanya mageuzi ya mfumo, lakini lengo la kujiendeleza kwa pamoja halitabadilika.
Idhaa ya Kiswahili 2004-10-08
|