Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-10-14 21:54:01    
Maisha ya Sarakasi ya Wakazi wa Jian Hu

cri

    Sarakasi ni maonyesho ya kijadi ya kisanii nchini China. Kupenya kwenye duara inayowaka moto, kusimamisha baiskeli kwenye jukwaa la juu, kutembea kwenye ngazi ya visu na michezo mingine inakaribishwa sana na watazamaji wa nchini China na wa ng'ambo. Watu wote waliowahi kutazama maonesho ya sarakasi ya China huwa wanastaajabishwa kwa ugumu na usanii wa kiwango cha juu wa sarakasi hizo. Katika kipindi hiki cha leo, tunawaongoza kwenda wilaya ya Jian Hu ya mji wa Yancheng, mkoani Jiangsu, ambayo ni moja ya chimbuko la sarakasi la China.

    Wilaya ya Jian Hu iliyoko kwenye delta ya mto Changjiang, mashariki mwa China, inajulikana sana kwa michezo ya sarakasi. Ukitembea mitaani au mashambani kwenye wilaya ya Jian Hu, utawaona watoto wakifanya mazoezi ya sarakasi. Baada ya pilikapilika za kilimo, wanakijiji husimamisha nguzo kwenye uwanja wa kuanika mpunga, na kufunga kamba kwenye nguzo hizo. Watoto wenye umri wa miaka 4 au 5 wanafanya mazoezi kwenye kamba hizo ili kujifunza ustadi wa kutembea kwenye kamba. Mazoezi hayo ndiyo msingi wa mchezo wa kutembea kwenye kamba ya chuma cha pua, ambao ni mchezo maarufu sana wa sarakasi nchini China. Mwaka 2003, kwenye tamasha la sarakasi lililofanyika nchini Ufaransa, mchezo wa kutembea kwenye kamba ya chuma cha pua wa kundi la sarakasi la Yan Cheng ulipata tuzo ya rais wa Jamhuri ya Ufaransa.

    Watu wa Jian Hu zamani waliishi kutokana na kuzalisha chumvi, lakini kutokana na kurundikana kwa udongo na kuinuka kwa ufukwe, mstari wa pwani ulisogea mbali. Wakazi wa Jian Hu walipaswa kuacha biashara ya chumvi. Kwa kuwa wakazi wa Jian Hu hawana mashamba ya kutosha, hivyo walipaswa kutafuta njia nyingine ya kujipatia chakula yaani kutembeza michezo ya sarakasi.

    Zamani, waliokuwa wanajifunza michezo ya sarakasi ni watoto wa familia maskini. Walikuwa wanajifunza huku wakitembelea hapa na pale kufanya maonesho, waliishi maisha ya taabu. Mchezaji mzee wa kundi la sarakasi la Yan Cheng Bi. Xu Meifang alisema:

    "Nilipokuwa mtoto sikuwahi kwenda shule hata siku moja, kila siku alfajiri na mapema nilipaswa kuamka na kufanya mazoezi bila kujali joto au baridi, hata ikianguka theluji. Tuliposhindwa kucheza vizuri tulichapwa viboko."

    Wachezaji wa zamani walijifunza na kucheza sarakasi kwa ajili ya kujipatia chakula, lakini hivi sasa watoto wanajifunza sarakasi kutokana na kupenda usanii wa sarakasi, hawana haja ya kuvumilia tena matusi na viboko. Kundi la sarakasi la Yan Cheng lililoko kwenye wilaya ya Jian Hu, linawachagua watoto wenye uwezo na hamu ya kujifunza sarakasi, na kuwafundisha michezo tofauti kutokana na hali yao ya kimwili. Mwalimu wa kundi hilo Bi. Zhao Jun ndiye aliingia katika kundi hilo la sarakasi kutokana na kuupenda mchezo wa sarakasi. Alisema:

    "Mimi nilijiunga na kundi la sarakasi nilipokuwa na umri wa miaka 8 kutokana na kupenda mchezo huo, mwanzoni wazazi wangu walikataa kunipeleka kwenye kundi hilo la sarakasi, lakini sasa nimejishughulisha na sarakasi kwa miaka 20, napenda michezo ya sarakasi."

    Kwenye kundi la sarakasi, wanafunzi huamka saa kumi na mbili asubuhi, wanafanya mazoezi mchana, na kujifunza masomo usiku. Wanafanya mazoezi kwenye ukumbi maalum wenye zana za aina mbalimbali za kisasa. Mafunzo ya kisayansi na upendo wa walimu kwa wanafunzi si kama tu vimezidisha uhusiano kati ya walimu na wanafunzi, bali pia vimewaandaa wachezaji watoto wengi hodari. Mwalimu wa kundi hilo Bi. Gao Wenjing alisema :

    "Nawachukulia kama watoto wangu mwenyewe, nawatendea kwa makini wakati wa mazoezi, na baada ya darasa, ninawaangalia vizuri."

    Sanaa ya sarakasi inahitaji ari na ukakamavu, wachina husema kuwa, dakika moja ya maonesho kwenye jukwaa huhitaji mazoezi ya miaka 10. Kila siku kutoka asubuhi hadi usiku, wanafunzi wanarudia vitendo vya aina moja mara elfu kadhaa mpaka wavimudu kabisa, ama sivyo hawawezi kucheza vizuri kwenye jukwaa. Mwanzoni wanafunzi wengi huona taabu, wengine hata wanalia mara kwa mara kutokana na ugumu wa michezo ya sarakasi, lakini wanapofuta machozi hupanda tena kwenye zana za kufanyia mazoezi na kurudia tena vitendo hivyo.

    Hivi sasa, sarakasi ya China imekuwa ua la ajabu linalochanua vizuri kwenye sanaa duniani. Kundi la sarakasi la Yan Cheng limefanya maonesho katika nchi nyingi duniani. Sarakasi imekuwa sehemu moja muhimu ya maisha ya wakazi wa Jian Hu.

Idhaa ya Kiswahili 2004-10-14