Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-10-18 18:19:44    
Maisha ya wakazi wanaoishi kwenye kando ya Mto Li

cri

    Watu wengi waliowahi kutembelea mkoa unaojiendesha wa kabila la Wazhuan, kusini magharibi mwa China wakizungumzia utalii wao, kila mmoja anajivunia sana, huku akisikitika kuwa aliweza kutembelea huko kwa muda tu.

    Mto Li wenye urefu wa kilomita 84 toka Guilin hadi Yangshuo, kaskazini mashariki ya mkoa wa Guangxi ni sehemu yenye mandhari nzuri kabisa. Mto huo unaonekana kama ni ukanda wa hariri wa kijani unaozunguka kwenye milima mingi. Mandhari nzuri hiyo inaonekana kama ni mchoro mkubwa. Katika sehemu hiyo, kila mita moja ya ujazo ya maji ya mto ina mchanga kilo 0.037 tu, hivyo maji ya mto huo ni safi sana, hata unaweza kuhesabu idadi ya samaki wanaotembea ndani ya maji. Na mji wa kale wa wilaya Daxu uko kwenye kando ya mto huo wenye mandhari nzuri ya kupendeza.

    Mji wa wilaya Daxu uko kwenye kando ya kaskazini ya Mto Li umbali wa kilomita 19 toka kusini mashariki ya mji wa Guilin, mji huo ulijengwa miaka 200 iliyopita. Barabara ya mawe ya kale yenye urefu wa kilomita 5 inapita kwenye mji huo mdogo wote, na nyumba zilizopo kwenye kando mbili za barabara hiyo zote ni za matofali zilizojengwa miaka zaidi ya 100 iliyopita. Nakshi nzuri za mbao kwenye milango ya nyumbani hizo bado zinaonekana vizuri na kuwakumbusha watu historia ya mingi ya mji huo mdogo.

    Hivi leo, maisha ya watu wa mji wa Daxu yanabadilika. Ukienda sehemu iliyo karibu na Mto Li unaweza kuona kuwa, kwenye mto mkubwa, mitumbwi ya mianzi na motaboti za aina mbalimbali zikiwemo motaboti za kifahari zenye ghorofa mbili au tatu zimetapakaa kwenye mto huo. Kuendesha mitumbwi au motaboti ndiyo maisha halisi ya wakazi wa Mji wa Daxu. Katika miaka mingi iliyopita, watu wa Daxu wamekuwa wakiishi kwenye kando ya mto, na wanasema kuwa maji ya Mto Li yamewalea mababu zao na watu wa vizazi hadi vizazi. Mzee Huang Qinggao anayeendesha mtumbwi wa mianzi kwa ajili ya watalii kwenye mto alisema:

    Baba yangu ni mvuvi, na mababu zangu wote walikuwa wavuvi, waliishi kwa kutegemea kuvua samaki. Lakini mpaka kizazi changu, tunajishughulisha na uchukuzi.

    Wakazi wa Mji wa Daxu kila mchana wanaambatana na watalii kutembelea mto, usiku wanapumzika nyumbani wakinywa chai au kuangalia mwanga wa wavuvi, kusikiliza sauti za mawimbi ya maji huku wakiburudika kwa furaha. Bwana Huang Liufei ni kijana mwenye umri wa miaka zaidi ya 20, mababu zake pia waliishi kwa kutegemea uvuvi, baadaye baba yake alifanya shughuli za uchukuzi kwenye mto na kupata kiasi fulani cha fedha, halafu wakaomba mkopo na kununua motaboti mbili ili wajishughulishe na mambo ya utalii, hivyo yeye amekuwa mwendeshaji wa motaboti. Kijana huyo akitaja Mto Li anasema neno moja tu "Mei", maana ya neno hilo la kichina ni nzuri. Alisema kuwa, mandhari ya Mto Li ni nzuri, milima ya sehemu hiyo ni mizuri ya kupendekeza, maji ya mto ni masafi, mapango ya milima ni ya ajabu, na majabali ya huko ni marefu na yenye kuvutia. Mandhari nzuri ya sehemu hiyo inawavuta watalii wengi wa nchini na wa nchi za nje kuja huko kutalii. Na mambo ya utalii yameleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wakazi wa Daxu, na shughuli za kutoa huduma za utalii zimekuwa moja ya sehemu ya maisha yao. Hata wakulima wengi wanawake wamekuwa waongoza watalii ambao wanawafurahia sana watalii.

Idhaa ya Kiswahili 2004-10-18