Wasikilizaji wapendwa ni watangazaji wenu Chen na Fadhili Mpunji tunawakaribisha katika kipindi hiki cha sanduku la barua. Leo kwanza tunawaletea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu, baadaye tutawaletea marudio ya makala ya pili ya chemsha bongo kuhusu ujuzi wa Miaka 55 ya China mpya.
Msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija wa Kiliwi shule ya msingi, sanduku la posta 1421 Mwanza, Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, ana furaha ya kututumia barua yake akitumai kuwa sisi wafanyakazi wote wa idhaa ya kiswahili ya Redio China Kimataifa inayotangaza kutoka Beijing, China hatujambo kabisa.
Anasema anapenda kutoa pole sana kwa kupotelewa na marafiki wa China walioangukiwa na paa la nyumba huko Paris Ufaransa, katika sehemu ya uwanja wa ndege wa Charles de Gaulle mjini Paris, vilevile pamoja na wachina waliouawa huko Afghanistan waliokuwa wakifanya kazi za kandarasi.
Anasema pia anataka kuwapa pole wale waliouwawa kwa kupigwa risasi marafiki zake wapendwa. Mungu aziweke roho za marehemu wote mahali pema peponi.
Pamoja na hayo yote anasema anaomba kama uwezekano upo, kipindi hiki cha sanduku la barua kiongezewe muda. Anasema muda uliopo sasa hautoshi, muda ukiongezwa angalau kuwa dakika kama ishirini kutakuwa na uwezekano wa kusikia barua nyingi za wasikilizaji wa redio china kimataifa.
Bwana Stephen Magoye Kumalija anatushukuru kwa kumtumia barua zetu mbili zikielezea maadhimisho ya miaka 40 ya uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania. Pia ndani ya barua hizo zikiwemo bahasha zikiwa ambazo zimelipiwa gharama ya stempu pamoja na picha za wanyama adimu kama mbawala na aina moja ya chui.
Anasema katika uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania ambao mwaka huu umetimia miaka 40 tangu kuanzishwa kwake, nchi hizi mbili kwa kweli zimekuwa zikiimarisha uhusiano huu siku hadi siku. Tarehe 26, Mwezi Aprili mwaka huu ilikuwa ni kilele cha maadhimisho ya miaka 40 tangu kuadhimishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania, katika uhusiano huo wa urafiki serikali hizi mbili zimeshirikiana vizuri sana katika juhudi za kujenga uhusiano wa mataifa haya mawili, na kuendeleza mambo mengi mbalimbali ya kimataifa.
Anasema anaamini kuwa uhusiano huo wa kibalozi kati ya Jamhuri ya watu wa China na Jamhuri ya muungano wa Tanzania utaendelea zaidi na kuutakia uhusiano huo udumu. Kwa kumaliza barua yake anautakia urafiki kati yake na wafanya kazi wote wa Redio China Kimataifa uendelee. Na anatutakia kila la kheri na maisha mema katika mwaka huu wa 2004
Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija kwa barua yake ya kueleza matumaini mazuri kuhusu maendeleo ya uhusiano kati ya China na Tanzania, tuna imani kuwa baada ya kufanya juhudi za pamoja, urafiki wa kijadi na ushirikiano wa kunufaishana kati ya China na Afrika pamoja na Tanzania utaimarishwa na kuendelea siku hadi siku.
Idhaa ya Kiswahili 2004-10-19
|