watoto wanacheza Gobang na roboti
Wanafunzi wanne wa shule ya sekondari ya Yali mjini Changsha, wakisaidiwa na wataalamu husika wamefanikiwa kutengeneza kompyuta ya kwanza inayoweza kucheza mchezo wa Gobang tarehe 26, Agosti mwaka huu. Roboti hiyo ambayo inajulikana kwa jina la "Guess", inapocheza Gobang na binadamu, inaweza kucheza mchezo kamili ikiwa ni pamoja na kuusoma mchezo, kufanya hesabu na kuhamisha kete. Wataalamu husika wamesema kuwa roboti hiyo inayoweza kucheza Gobang na binadamu uso kwa uso ni ya kwanza kutengenezwa nchini China, na ni mafanikio mapya iwe kwa wazo la usanifu au kwa kiwango cha teknolojia. Huu ni moja ya mifano ya mafanikio ya harakati za sayansi kwa wanafunzi wa shule ya sekondari katika uvumbuzi.
Katika maabara ya sekondari ya Yali mjini Changsha, roboti hiyo ilifanya maonesho ya kucheza Gobang na binadamu uso kwa uso. Watu waliona kuwa roboti hiyo ilikuwa ikinyoosha mkono wake na kuchukua kete moja nyeusi taratibu na kuihamisha chini ya kete moja nyeupe kwa upande wa kulia, baada ya sekunde kadhaa roboti hiyo ilinyoosha mkono wake na kumaliza kazi ya kuhamisha kete moja nyingine. Roboti hiyo ilicheza Gobang na binadamu kwa zaidi ya dakika 20, na hatimaye roboti hiyo ilishinda. Lakini Dr. Zhang Daibing wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia ya Ulinzi wa Taifa, ambaye alikabidhiwa jukumu la kuwaelekeza wanafunzi hao katika utafiti na usanifu wao, alisema kuwa kwa hivi sasa roboti hiyo imewekewa mfumo wa upigaji hesabu wa mchezo wa Gobang tu lakini ni ya kiwango cha juu.
Mwalimu wa elimu ya sayansi na teknolojia ya sekondari hiyo Bw. Zhu Quanmin alisema kuwa Yao Jinyu, Long Fan, Cheng Zhiwei na Lai Tao ni wanafunzi wa kidato cha tatu, waliokuwa na wazo hilo mwezi Aprili mwaka jana. Wakati ule, wanafunzi wa idara ya mitambo na elektroniki na wa idara ya mitambo inayojiendesha za Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia ya Ulinzi wa Taifa, wakishirikiana walifanya maonesho ya roboti, hivyo wanafunzi hao wakajiwa na wazo la kutengeneza roboti wao wenyewe. Kutokana na msaada wa mtaalamu Dr. Zhang Daibing, katika muda wa mwaka mmoja na nusu, walishinda matatizo mbalimbali, hatimaye walifaulu kutengeneza roboti hiyo inayoweza kucheza mchezo wa Gobang na binadamu.
Idhaa ya kiswahili 2004-10-27
|