Kama inavyofahamika, Wachina wanapokula hutumia vijiti vya kulia. Mazoea hayo yamekuwa na miaka elfu kadhaa. Kuna miiko katika matumizi yake, na usipoelewa pengine utawaudhi wageni au wenyeji. Ifuatayo ni baadhi ya miiko muhimu:
* Mwiko wa kulaza vijiti juu ya bakuli.
Ikiwa mwenyeji anawakaribisha marafiki au jamaa zake kwenye chakula, anapoandaa meza ni mwiko kuweka vijiti vya kulia juu ya mabakuli. Kwani kuweka hivyo kunamaanisha mwenyeji hafurahi kuwapokea wageni wake, ni dalili ya kuwafukuza au kuwadhihaki wageni kama ni waombaji wa vyakula; Wageni wakiweka vijiti vyao juu ya mabakuli yao, wanaashiria kwamba hawajashiba au hawajatia kitu tumboni, ni utovu wa adabu kwa mwenyeji. Lakini wanaokirihi sana kuweka vijiti vya kulia kama hivyo ni wavuvi, kwa sababu wanaona ni ishara ya kuwatakia maafa ambayo ama mashua yao yatakwamwa, au mlingoti utaanguka au mashua itapinduka.
* Mwiko wa kuchomeka vijiti ndani ya chakula.
Kuchomeka vijiti vya kulia ndani ya chakula ni vibaya sana, kwani kuweka hivi kunatumika tu wakati wa kufanya kafara kwa marehemu. Ukiwa mgeni na ukichomeka vijiti kama hivyo una maana ya kumtakia mabaya mwenyeji, pengine unasababisha ugomvi kati yako na mwenyeji.
* Mwiko wa kutumia vijiti vya kulia vinavyotofautiana kwa urefu.
Vijiti vya kulia vinapaswa kuwa na urefu sawa kwa pea, kwa hiyo unapoandalia chakula lazima uhakikishe vijiti vyote vinakuwa sawa kwa urefu na vile vilivyo tofauti kwa urefu visiwekwe mezani. Kwa kuwa vijiti hivi vinaleta maana mbaya ambapo ukiwa mwenyeji kuandalia vijiti hivi una naana ya kumtakia mmojawapo kati ya wenyeji mume na mke, au wazazi wao afe mapema; Ukiwa mgeni na kuandalia vijiti vilivyotofautiana kwa urefu una maana ya kumwapiza mwenyeji. Kutokana na hayo ni muhimu kuhakikisha kwamba vijiti vya kulia vinakuwa sawa kwa urefu kabla ya kuanza chakula.
* Mwiko wa kutumia vijiti vyeupe vya kulia katika chakula cha arusi.
Wachina wana mila ya kupenda rangi nyekundu, kwa kuwa wanaona rangi nyekundu inaashiria furaha na baraka. Ndoa ni jambo kubwa katika safari ya binadamu duniani. Kwa hiyo, vijiti vya kulia katika chakula cha arusi vinapaswa kuwa vyekundu. Ni mwiko kutumia vyeupe ila tu vile vya fedha au vya pembe za ndovu. Katika China ya kusini wenyeji wanaposherehekea siku ya arusi hutumia vijiti vilivyochongwa kwa mianzi, lakini hata hivyo lazima vitiwe rangi nyekundu kabla ya kutumia.
* Mwiko wa kutumia vijiti vyekundu katika chakula cha mazishi.
Rangi ya vijiti vya kulia katika chakula cha mazishi ni tofauti na vile vitumikavyo katika siku za furaha, navyo lazima viwe vyeupe. La, sivyo, ni hali ya kutomheshimu marehemu. Lakini kwenye chakula cha mazishi kwa ajili ya wale marehemu waliozidi umri wa miaka 80 vijiti vyekundu sio mwiko kutumika kwa kuonyesha kuwa marehemu alikuwa na maisha marefu na baraka humu duniani.
* Mwiko wa kutumia vijiti vya kulia vyenye rangi tofauti.
Vijiti hivyo vyenye rangi tofauti vinaonelewa kama ni kutopatana katika familia. Kwa hiyo vijiti kama hivyo havitumiki kabisa wakati wote.
* Mwiko wa kupokea vitoweo kwa vijiti vya kulia.
Wachina ni watu wakarimu, kwenye chakula wenyeji huwasaidia wageni vitoweo, wakati huu wageni wasivipokee au kuvirudisha njiani kwa vijiti vyao badala ya kusubiri kuwekewa kwenye sahani. Kadhalika, walaji wasigonganishe vijiti vyao wanapobana kitoweo kwenye sahani moja, na ni mwiko pia kutia vijiti vyako kwenye kitoweo ambacho hakipo katika upande wako. Yote hayo yaonekana uroho wa kunyang'anyana vitoweo unavyovipenda.
* Mwiko wa kudondosha kitoweo.
Vijiti vya kulia vinapochukua vitoweo na kupeleka kwenye sahani, visidondoshe kitoweo mezani, vijiti hivyo vinaitwa vijiti vya machozi. Walaji wakila hivyo wanaonekana kama hawajafundishwa vizuri adabu na ni wachafuzi pia.
* Mwiko wa kugonga gonga bakuli au sahani kwa vijiti vya kulia.
Ni utovu wa adabu kupiga piga bakuli au sahani, kwani kufanya hivyo kunamaanisha una haraka ya kupatiwa chakula, au unalalamika kwamba "chakula kimeisha" au "vitoweo hamna".
* Pia kuna mwiko mwingine kabla sijasahau, kwamba kwenye karamu usitangulie kula kabla ya mheshimiwa kuanza.
Idhaa ya Kiswahili 2004-10-27
|