Kuanzia leo tarehe 29, spika wa bunge la umma la China Bwana Wu Bangguo atafanya ziara rasmi nchini Kenya, Zimbabwe, Zambia na Nigeria, na Kenya ni kituo cha kwanza cha ziara yake. Kabla ya ziara hiyo, mwandishi wetu wa habari aliyeko Nairobi alimhoji ofisa wa habari wa Ubalozi wa China nchini Kenya Bwana Zhuang Yaodong na baadhi ya wasikilizaji wetu wa Kenya.
Bwana Zhuang Yaodong alisema:
Kutokana na mwaliko wa serikali za nchi 4 za Kenya, Zimbabwe, Zambia na Nigeria, spika wa bunge la umma la China Bwana Wu Bangguo ataanza ziara yake ya kirafiki katika nchi hizo kuanzia tarehe 29 Oktoba hadi tarehe 8 Novemba. Kenya ni kituo chake cha kwanza. Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu wa serikali ya awamu mpya ya China kuitembelea Kenya tangu serikali mpya ya Kenya kushika hatamu za serikali. Ziara hiyo ina umuhimu mkubwa katika kusukuma mbele maendeleo ya uhusiano wa kisiasa kati ya China na Kenya, kuimarisha mawasiliano kati ya mabunge ya nchi hizo mbili, kuimarisha na kuendeleza urafiki wa kijadi wa nchi hizo mbili.
Bwana Zhuang Yaodong alisema kuwa, Kenya ni nchi yenye athari kubwa barani Afrika hasa kwenye sehemu ya mashariki ya Bara la Afrika, na imetoa mchango mkubwa katika kulinda amani ya kikanda na kusukuma mbele maendeleo ya uchumi wa kikanda kwa miaka mingi iliyopita. Pia Kenya imekuwa ikidumisha uhusiano wa kirafiki na China katika miaka mingi iliyopita. Baada ya serikali mpya ya Kenya kushika madaraka mwaka 2003, uhusiano wa kirafiki kati ya China na Kenya unaendelea kwa hatua madhubuti, ambapo viongozi wa nchi hizo mbili wametembeleana mara kwa mara. Naibu spika wa bunge la umma la China Bwana Han Qide, naibu mwenyekiti wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la China Bwana Bai Lichen, waziri wa elimu Bwana Zhou Ji, na mkurugenzi wa Shirikisho la kuhimiza biashara la China Bwana Wan Jifei na wengineo walifanya ziara nchini Kenya; ambapo waziri wa mambo ya nje wa Kenya Bw Kalonzo Musyoka, waziri wa mipango na maendeleo ya nchi Bwana Nyongo, na waziri wa utalii na habari Bwana Tuzhu pia walitembelea China kwa nyakati tofauti. Wakati huohuo, uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Kenya unaendelea vizuri kwa haraka. Mwaka 2003, thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili ilifikia dola za kimarekani milioni 250. Uwekezaji vitega uchumi wa China na miradi inayojengwa na China nchini Kenya pia imeongezeka siku hadi siku katika miaka ya hivi karibuni. China imeanzisha kituo cha kuhimiza uwekezaji vitega uchumi na biashara nchini Kenya, na mradi wa barabara ya Kisasa unaofadhiliwa na serikali ya China utaanzishwa hivi karibuni, ambapo mazungumzo kuhusu ujenzi wa miradi ya ukarabati wa hospitali ya Kenyatta ya Nairobi, kiwanda cha kutengeneza unga wa mahindi, ukarabati wa mfumo wa umeme mijini na mfumo wa simu vijijini pia unafanyika hivi sasa. Aidha, China na Kenya zinafanya juhudi kubwa za maingiliano na ushirikiano katika nyanja za habari, utamaduni, elimu na mambo ya kijeshi, na zimesaini makubaliano mengi kuhusu ushirikiano mpya katika nyanja za utalii, habari, elimu na afya, hayo yote yameweka msingi imara kwa maendeleo ya kiutaratibu ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Zaidi ya hayo, China imeikubali Kenya kuwa nchi inayowapokea watalii wa China, na kuamua kujenga chuo cha Confucius katika Chuo kikuu cha Nairobi ili kuanzisha somo la kichina na somo la utamaduni wa China. Hivi sasa China na Kenya zimeanzisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali kwenye ngazi mbalimbali, na mustakbali wa ushirikiano huo ni mkubwa sana.
Bwana Zhuang Yaodong amemwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, katika ziara yake nchini Kenya, Spika Wu Bangguo atafanya mazungumzo na makamu wa rais wa Kenya Bwana Moody Awori, na kuhudhuria sherehe ya kutia saini makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na kiteknolojia kati ya nchi hizo mbili. Aidha, spika Wu Bangguo atatembelea makao makuu ya shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa yaliyoko Nairobi, Kenya.
Bwana Hassan ni msikilizaji makini wa Radio China kimataifa, ambaye anajua mengi kuhusu mawasiliano kati ya China na Kenya, anasema:
Tumefaidika mengi kutoka kwa China, tunashukuru sana, anafurahia sana kwa moyo mkunjufu ziara ya spika Wu Bangguo nchini Kenya, na anaamini kuwa kutokana na ziara hiyo, mwangaza umepanuliwa katika uhusiano wa kirafiki kati ya Kenya na China, na anatarajia Kenya na China zitauwezesha ushirikiano huo uzidi kiwango ambacho tuko nacho sasa. Ana imani kuwa, ziara ya spika Wu nchini Kenya itafungua mlango mpya na sura mpya kwa uhusiano kati ya Kenya na China.
Na msikilizaji wetu mwingine Bwana Dose pia anasema:
Ziara hiyo ni jambo zuri, hivi sasa uhusiano kati ya Kenya na China ni mzuri sana, ziara ya spika Wu Bangguo itasaidia kuendeleza shughuli mbalimbali kama vile shughuli za utalii ambazo zinanufaisha wananchi wa Kenya.
Idhaa ya Kiswahili 2004-10-29
|