Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-05 20:04:59    
Ziara ya Spika Wu Bangguo wa China nchini Kenya yahimiza mawasiliano kati ya nchi hizo mbili kuingia katika kipindi kipya

cri
    Kuanzia tarehe 29 mwezi uliopita hadi tarehe 1 mwezi huu, spika wa halmashauri ya kudumu la bunge la taifa la China Bw. Wu Bangguo alifanya ziara rasmi ya kirafi ya siku nne nchini Kenya. Ziara yake ilipata mafanikio makubwa, ambapo viongozi wa China na Kenya walifikia makubaliano mbalimbali katika mkutano na mazungumzo. Hivi karibuni mwandishi wetu wa habari aliyeko huko nairobi alimhoji balozi wa China nchini Kenya Bw. Guo Chongli juu ya ziara hiyo ya spika Wu.

    Bw. Guo alimwambia mwandishi wa habari kuwa, ziara ya Bw. Wu Bangguo ilifanyika wakati uhusiano kati ya China na Kenya upo katika kipindi muhimu. Alisema kuwa, kwa upande wa siasa, kuanzia mwezi Januari mwaka 2003, NARC ilipoingia madarakani kuiongoza nchi hiyo, muundo wa serikali ya Kenya amebadilika sana, ambapo mwezi Machi mwaka 2003, serikali ya awamu mpya ya China ilianzishwa. Hivyo ziara hiyo ya Spika Wu ina umuhimu mkubwa kwa kuhimiza uhusiano kati ya serikali mpya za nchi hizi mbili na kuimarisha mawasiliano ya kirafiki ya kijadi kati ya pande hizi mbili.

    Bw. Guo anasema,

    "Tangu serikali mpya ziingie madarakani, uhusiano kati ya China na Kenya umepata maendeleo mapya. Hivi sasa uhusiano wa kisiasa wa nchi hizi mbili umeingia kwenye kipindi kipya cha kuendelea kwa utulivu."

    Balozi Guo alisema kuwa, katika miaka kadhaa ya hivi karibuni, uhusiano wa kiuchumi na kibiashara unaendelea vizuri kati ya China na Kenya. Mwaka 2003, thamani ya jumla ya biashara kati ya nchi hizi mbili ilifikia dola za kimarekani zaidi ya milioni 250. Aidha, makampuni nyingi zaidi za China zimewekeza vitega uchumi nchini Kenya. Mbali na hayo, ushirikiano na mawasiliano katika nyanja za habari, utamaduni, elimu, afya na jeshi zinaendelea vizuri kati ya nchi hizi mbili. Mwaka huu, serikali ya China pia imeiweka Kenya kwenye orodha ya nchi zinazopokea watalii kutoka China. Katika sekta ya elimu, wizara ya elimu ya China imeamua kuanzisha chuo cha Confucius katika chuo kikuu cha Nairobi cha Kenya ili kutoa mafunzo ya lugha na utamaduni wa kichina. Bw. Guo alisema kuwa, hivi sasa ushirikiano kati ya nchi hizi mbili katika nyanja mbalimbali unastawi, na una mustakabala mzuri.

    Bw Guo alieleza kuwa, alipofanya ziara nchini Kenya na Spika Bw. Wu Bangguo na Spika wa bunge la Kenya Bw. Francis Ole Kaparo, walikutana tarehe 30, ambapo walibadilishana maoni kuhusu masuala mbalimbali, na kufikia maoni mengi ya pamoja, na imezidisha maelewano na urafiki kati ya mabunge ya nchi hizo mbili.

    Bw. Guo anasema,

    "Uhusiano kati ya mabunge ya China na Kenya ni mzuri sana. Viongozi wa mabunge hayo wanatembeleana mara kwa mara. Mwaka 1999, Bw. Li Peng aliyekuwa spika wa bunge la umma la China alitembelea Kenya. Baada ya hapo naibu spika Bw. Li Tieying na Bw. Han Qide pia waliitembelea Kenya kwa nyakati tofauti. Kwa upande wa Kenya, spika na naibu spika wa bunge la taifa la nchi hiyo pia walifanya ziara nchini China. Mabunge ya nchi hizi mbili pia yameanzisha vikundi vya urafiki katika kila upande.

    Bw. Guo alisema kuwa, bunge la taifa linawakilisha nia ya wananchi, hivyo ushirikiano na mawasiliano mazuri kati ya mabunge ya China na Kenya bila shaka yataongeza urafiki wa watu wa nchi hizi mbili.

    Licha ya kukutana na spika na watu wengine wa bunge la Kenya, spika Wu Bangguo pia alikutana na viongozi wa serikali ya nchi hiyo. Kwa kuwa rais Kibaki wa Kenya walikuwa nje ya nchi, makamu wa rais wa Kenya Bw. Moody Awori alikutana na spika Wu. Katika mazungumzo yao, pande hizi mbili zilijadili masuala yanayozihusu nchi hizi mbali, pia zilibadilishana maoni kuhusu masuala ya kimataifa.

    Bw. Guo alisema,

    "Ziara hiyo ya spika Wu ilipata mafanikio makubwa, na imefikia malengo. Kwa upande wa kisiasa, viongozi wa China na Kenya wamezidisha uaminifu kupitia mazungumzo, na kukuza maelewano na urafiki. Pande hizi mbili pia zimeahidi kuzidisha ushirikiano katika mambo ya kitaifa na kimataifa. Katika ziara hiyo, viongozi wa nchi hizi mbali wamesaini mikataba kadhaa ya ushirikiano. Kutokana na mkataba mmoja, serikali ya China itatoa msaada wa dola za kimarekani zaidi ya milioni 3 laki 6 kwa miradi ya maendeleo nchini Kenya. Mbali na hayo, pande hizi mbili pia zimeonyesha nia ya kushirikiana katika miradi mingine ya barabara, tiba na kilimo.

    Bw. Guo alisema kuwa, ziara hiyo ya spika Wu Banguo nchini Kenya imeendeleza uhusiano na maelewano ya nchi hizi mbili, na kuweka msingi imara kwa maendeleo ya uhusiano na maelewano. Alieleza kuwa ana imani kubwa kwamba, ziara hiyo itahimiza uhusiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya China na Kenya kuingia kipindi kizuri kipya.

Idhaa ya Kiswhaili 2004-11-05