Msikilizaji wetu Bramwel Sirali wa Kenya ametuletea barua ikiwa na maelezo kidogo kuhusu Mila za China. Makala yake inasema kuwa, China ni nchi kubwa iliyoko barani Asia. China inachukua nafasi ya tatu kwa ukubwa wa eneo baada ya Canada na Russia. Kwa vile China ni kubwa, pia ni nchi yenye watu wa makabila mbalimbali ambao wamechanganya mila na desturi.
Anasema, China ina makabila 56, kila kabila lina mila zake. Baadhi ya makabila ya wenyeji wa China ni haya: wa Han, wa Kazak, wa Uyghr, wa Mongolia, wa Xibe, wa Manchu, wa Hui, wa Wei, wa Dai, wa Zhuang, wa Bai, wa Yi, wa Jingpo, wa Tujia, wa Miao, wa Naxi, wa Lhoba na wengine wengi.
Katika eneo la magharibi mwa China kuna kabila la watu wasiopungua 2000, hawa ni wa Lhoba. Wa Lhoba wanaishi magharibi ?mashariki mwa Tibet. Watu hao wana lugha wanayoweza kuongea lakini hawana maandishi wanayoweza kuandika. Kabla ya kuasisiwa kwa Jamhuri ya watu wa China, wa Lhoba waliweka kumbukumbu zao kwenye. Wana utajiri wa hadithi ambazo zilizopokelewa kwa midomo tu. Wachache wao wanaweza kuzungumza kitibet. Na hata jina la "Lhoba" ni neno la kitibet na linamaanisha "waishio Magharibi".
Maisha ya Wa Lhoba yanategemea kilimo na uwindaji, na kukusanya matunda na vyakula vingine. Watu wa Lobha wanawaheshimu sana wawindaji. Vijana huanza kujifunza kuwinda katika umri wa miaka saba au nane pamoja na wazazi wao Misituni. Wa Lhoba wanaume ni wawindaji wazuri na wanaufahamu mkubwa kuhusu misitu na wanyama wanaoishi humo. Mawindo wanayoleta nyumbani hugawanywa kwa wanakijiji.
Wa Lhoba wanaishi zaidi katika sehemu za milima na mabonde mahali ambako usafiri sio thabiti. Wametunukiwa ujuzi wa kujenga madaraja yaliyochongwa kwa miti ya mizabibu na kuyaeneza ili waweze kupita kwenye mito na mabonde mengi.
Wa Lhoba pia wanahifadhi upishi wao wa jadi wa chakula, kama uchomaji wa nyama, kuchemsha au kupika ndani ya vibuyu. Wanapoenda safari wao hubeba mara kwa mara chakula kama wali au chakula kingine hupikwa njiani wakiwa safarini. Wakati wanahitaji kula hutumia kisu kufungua vibuyu walivyobebea chakula.
Wa Lhoba pia wanafahamika pia kwa ukarimu wakati wa ukaribishaji huu. Mgeni anapokuwa hupewa chakula kizuri. Kabla wageni hawajaanza kula, mwenyeji hunywa mvivyo kidogo na kula wali kidogo ili kuonesha uaminifu. Wao huona ni jambo la heshima kwa mgeni kukaa na kula nao. Lakini mgeni lazima ale chakula chote la sivyo mwenyeji ataona kwamba ameshindwa kwa makaribisho yake.
Mara nyingi wanaume hubeba kisu kirefu ambacho hakitumiki tu kama pambo bali kama kifaa na silaha. Wakati mwingine kinawasaidia kuwakinga dhidi ya mashambulizi ya wanyama wa mwituni na pia kwa matumizi ya kawaida ya kukata mabua na kuni na kwa kutengenezea nyavu za miti ya mizabibu.
Upinde ni kifaa cha uwindaji kisichoweza kukosekana. Wana uthabiti wa utengenezaji wa pinde na mishale, na wakati wa kutengeneza mishale huchagua miti mizuri, na inaweza kuchukua karibu siku 20 kumaliza idadi ya kiwango cha juu kizuri cha utengenezaji sanifu cha upinde na mishale.
Upinde ukiwa mzuri unakuwa ni silaha nzuri na ni ishara nzuri ya mwindaji shupavu. Na vijana wadogo wanaoweza kutengeneza silaha nzuri hupata wasichana warembo. Upinde na mshale hutolewa kama zawadi kwa wazazi wanaojivunia kuzaa mtoto. Na pia si ajabu silaha kuwa ni moja ya vitu vinavyokuwepo wakati wa sherehe. Isipokuwa tu kwa wa Lhoba wanaoishi Motuo na Milin, wanapoadhimisha mwaka mpya wa Tibet wa Lhoba wengi wanashrehekea mwaka mpya kwa namna tofauti kidogo.
Kama desturi, wa Lhoba wanaoishi magharibi sana, wanasherehekea mwaka mpya katika mwezi wa pili wa kalenda ya kitibet. Wanakijiji wote hujikusanya pamoja na kuimba na kucheza kando ya moto mkubwa uliowashwa nje wakiomba kwa ajili ya mavuno mazuri mwakani. Pia jamii ya huko hushiriki kwenye harusi ya ajabu pamoja.
Wale wanaoishi mashariki wanasherehekea mwaka mpya, siku 15 ya mwezi wa mwisho kwa kalenda ya kitibet. Hupeana vipande vya nyama ya kondoo na fahali, kama zawadi kwa jamii zao na marafiki. Baada ya kula nyama ya fahali, fuvu lake huning'inizwa ukutani. Inachukuliwa kama ishara ya bidii na uadilifu.
Msikilizaji wetu Kaziro Dutwa wa sanduku la posta 209 Songea, Ruvuma ,Tanzania ametuletea barua akituelezea "Mila za kabila la kisukuma" lililoko nchini Tanzania. Anasema wasukuma ni kabila lililo kubwa kabisa nchini Tanzania, na watu wake wako kwenye mikoa ya Shinyanga na Mwanza. Watu hawa ni wachapa kazi wazuri sana hasa katika kilimo na ni wafugaji wazuri wa ng'ombe, mbuzi na kondoo vilevile kuku, bata na mbwa.
Wasukuma ni waendeshaji wazuri sana wa serikali za kijadi ndiyo maana kuna sheria ndogondogo ambazo huiongoza jamii hii kubwa, na kuiwezesha kuwa na maisha mazuri ya amani na usalama chini ya walinzi wa jadi au kwa jina lingine Sungusungu. Walinzi hawa wa jadi ni wakali na hutembea kwenye vikundi huku wakiwa na silaha za jadi kama vile pinde, mishale, mikuki na ngao.
Wasukuma ni jamii ambayo ilikuwa haitilii maanani sana masuala ya elimu hivyo kutokwenda na wakati, vijana wa jamii hiyo walikuwa wanajilazimisha kumaliza elimu ya msingi kwa kuhofia sheria zilizowekwa na serikali ya Tanzania. Kwani wengi wameshashtakiwa na kufungwa kwa kuwaoza wanafunzi kwa watu matajiri wa mali, mifugo au pesa kwani wanaume wa jamii hiyo ni watu wapendao kuoa wanawake wengi na wanawake hao hufanywa kama kitega uchumi cha mwanaume kwani mume huwagawia wake zake mashamba na huwasimamia katika kuyaendesha. Mavuno yanayopatikana humilikiwa na bwana, na yeye pia ndiye anayepanga matumizi ya mapato yote yanayotokana na kilimo.
Wanaume wa Kisukuma huoa mara tu wanapofikisha umri fulani na hii hutokana na shinikizo la wazazi. Hali hii hufanywa ili yule kijana asiendelee na masomo au kutafuta kazi kwani wao huamini kuwa pindi kijana wakimwachia aendelee na masomo basi atakuwa siyo wao bali wa serikali na hivyo kuwa "mlowezi". Hili ndilo jina analopewa kijana anayeondoka nyumbani na kwenda kuishi mbali na wazazi, iwe kwa kufanya kazi au kusoma. Wasukuma hutoa mali nyingi kama mahari kwa mwanamke hasa mwanamke mweupe hufikia hadi ng'ombe sitini, tena wa kujichagulia!
Msukuma awe mwanamke au mwanaume iwapo ataishi maisha yake bila kujaaliwa kupata mtoto basi siku yake ya kufa atakuwa na wakati mgumu kwani siku ya kuzikwa atadhalilishwa. Pamoja na haya watu hawa ni wakarimu na wacheshi sana, na baadhi yao ni watu wanaoamini sana ushirikina na vikongwe wenye macho mekundu huuawa kwa kutuhumiwa kuwa ni wachawi.
Vikongwe hawa hukatwa kwa mapanga au kupigwa mishale na pengine hufungiwa ndani ya vibanda vya nyasi na kuwashwa moto. Haya yote yalikuwa yakitokea kutokana na kuwa na elimu duni, hata hivyo mila hizi sasa hivi zinatoweka taratibu, kutokana na juhudi za serikali kuwaelimisha, wakiumwa waende zahanati au hospitali, wasidhani kuwa kila kikongwe mwenye macho mekundu kuwa ni mchawi.
Idhaa ya Kiswahili 2004-11-09
|