Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-15 18:44:44    
Maingiliano ya Vyombo vya Kauri vya China katika Zama za Kale

cri

    Vyombo vya kauri vilikuwepo nchini China kabla ya miaka 1700 iliyopita. Tokea hapo, vyombo vya kauri vya China vilienea duniani na baadhi vinahifadhiwa hadi leo katika majumba makubwa ya makumbusho duniani.

    Kwa mujibu wa historia, vyombo vya kauri vya China vilianza kuonekana nchi za nje katika karne ya 8. Wakati huo vyombo hivyo kwanza vilionekana Mashariki ya Kati ya Asia, ambapo ni moja kati ya sehemu za asili ya utamaduni duniani. Waliomiliki vyombo hivyo walikuwa ni wafalme, matajiri na wafanyabiashara wakubwa. Katika karne ya 9 mji wa Baghdad ulikuwa ni kituo cha biashara cha Waislamu. Vitambaa vya hariri, na vyombo vya kauri vya China vilikuwa ni bidhaa muhimu sana, hasa vyombo vya kauri nyeupe na nyeusi.

    Mtu anayestahili kutajwa ni baharia maarufu wa China, Zheng He. Tokea mwaka 1405 hadi 1433, katika miaka 29 aliwahi kusafiri mara saba, na kufanya biashara ya China na nchi za nje kupamba moto. Wakati huo bidhaa muhimu za China zilikuwa ni vyombo vya kauri nyeupe na nyeusi. Pamoja na bidhaa hizo Zheng He pia alisafiri na vyombo vya kauri vilivyotengenezwa katika mji wa Jingdezhen na kuwazawadia watawala wa nchi alizopita, hadi sasa baadhi ya vyombo hivyo vinahifadhiwa na nchi nyingi katika majumba ya makumbusho.

    Katika jumba la makumbusho la Topkapi mjini Istanbul, Uturuki, bado vipo vyombo vya kauri 13058 vya China, na vyote ni vya daraja ya juu vilivyotengenezwa kutoka kwenye tanuru la kiserikali mjini Jingdezhen. Na miongoni mwa vyombo hivyo vyombo vya kauri nyeusi vilivyotengenezwa katika Enzi ya Yuan (1206-1368) ni vizuri zaidi kuliko vinavyohifadhiwa nchini China. Hii inamaanisha kuwa vyombo hivyo vilitengenezwa mahsusi kutokana na maagizo.

    Katika karne ya 16 vyombo vya kauri vya China vilianza kuonekana nchini Ureno. Baada ya miaka kadhaa ya vita vya kunyakua biashara ya baharini, Uholanzi ilichukua nafasi ya ukiritimba wa biashara ya baharini badala ya Ureno katika bahari ya Pasifiki ya magharibi na ilikuwa mnunuzi mkubwa wa vyombo vya kauri vya China. Katika mwaka 1636, 1637 na 1639 Uholanzi ilinunua vyombo vya kauri vya Jingdezhen jumla laki kadhaa. Katika kipindi cha miaka 100 ya karne ya 18, vyombo vya kauri vya China vilivyonunuliwa na nchi za Ulaya vilikuwa milioni 60.

    Ili kuridhisha uzuri walivyoona watu wa Ulaya, vyombo vya kauri vya Jingdezhen vilikuwa tofauti na vya kuuzwa humu nchini, ambavyo vingi vilikuwa ni vya kauri nyeusi vya sahani, mabakuli na chupa, na michoro kwenye vyombo hivyo pia ilikuwa ya mtindo wa Ulaya ingawa kulikuwa na michoro ya maua na ndege kwa mtindo wa Kichina.

    Sambamba na vyombo vya kauri vya China kusafirishwa nchi za nje, vyombo vya kauri vya China vilitengenezwa kutokana na maagizo. Sehemu ya Iznik, kusini mashariki mwa Uturuki ilikuwa kama mji wa Jingdezhen wa China. Hadi mwaka 1755 watu wa Ulaya waligundua udongo wa "Kaolin" kwenye bara lao, huu ni udongo uliopatikana tu katika mji wa Jingdezhen kwa ajili ya matengenezo ya vyombo vya kauri. Mwaka 1768 watu wa Ulaya kwa mara ya kwanza walifanikiwa kutengeneza vyombo vya kauri vilivyolingana na vya Jingdezhen. Kama mwanahistoria wa Marekani Bw. Atherton alivyosema katika kitabu chake cha "China katika Historia ya Dunia", kwamba "kutokana na wamissionary kuleta teknolojia ya China katika karne ya 18, Ulaya iliweza kutengeneza vyombo halisi vya kauri."

    Hivi sasa katika jumba la makumbusho la Louvre, na la Versilles nchini Ufaransa, jumba la makumbusho la Heideberg nchini Ujerumani, jumba la makumbusho la British na la Victoria nchini Uingereza, watu wanaweza kuona vyombo hivyo vya China vilivyosafirishwa kwenda huko Ulaya katika zama zile. Vyombo hivyo vinashangaza sana watazamaji kwa uzuri na ufundi uliotumika katika utengenezaji wake.

Idhaa ya Kiswahili 2004-11-15