Msikilizaji wetu Nsorani George Mwita wa Security Group LTD sanduku la posta Nairobi, Kenya ametuletea barua akianza kwa salamu kwa watangazaji na wasikilizaji wa Radio China kimataifa, na akituelezea kuwa yeye huko Nairobi anaendelea vizuri na kazi na kuisikiliza Radio China kimataifa..
Anasema lengo la kutuandikia hii barua ni kushukuru kwa barua tuliyomwandikia, ambayo anasema ilimfurahisha sana. Pia anasema anapenda kutuambia machache kuhusu kabila lake la Kurya. Yeye ni Mkurya anayetoka wilaya ya Kurya katika mkoa wa Nyanza nchini Kenya.
Kwenye Mila na desturi za kabila la wakurya kijana anapofikia umri fulani anapaswa kufanyiwa tohara. Anapotimiza miaka kumi na tano yeye hutoka nyumbani na kwenda msituni akiwa na na kibuyu kimoja cha maziwa na kwenda nacho msituni. Huko msituni atatakiwa amuue simba na achukue ulimi wake kama ishara ya yeye kuweza kumuua simba. Ulimi huo utathibitishwa na wazee wa kikurya wanaoitwa abagaka binchama yaani wazee wa kimila. Hao wazee huchukuwa kibuyu kimoja cha maziwa na kingine cha damu halafu huvipeleka vikiwa vitupu katika mlima mmoja, na kuviacha huko kwa mwezi mmoja.
Baada ya huo mwezi mmoja vibuyu hivyo hujazwa maziwa na damu, lakini siyo watu wanaojaza vibuyu hivyo bali ni mizimu. Baada ya hayo vijana hufanyiwa tohara katika mlima unaoitwa Yeuchoka. Muda wa kufanyiwa tohara ni usiku wa manane na ni vijana zaidi ya mia tano wanaofanyiwa tohara na mtu mmoja.
Baada ya hayo, kijana huambiwa atafute msichana aoe. Kabla ya kuoa hutakiwa kuwa na mchumba kwa mwezi mmoja, na hapo ndiyo anapatiwa ng'ombe thelathini na baba yake apeleke kwa msichana, ili msichana aruhusiwe kwenda kufanya harusi. Baada ya hayo kijana huhama kutoka kwa baba yake na kwenda kuanza kujitegemea. Huko anaweza kuanza maisha yake na kufuga ng'ombe, mbuzi, mbwa kondoo, kuku, na wanyama wengine.
Anapozeeka hutoa wosia, akisema anapokufa ng'ombe fulani achinjwe na ngozi yake itumike kumzikia. Baada ya kaburi lake kuchimbwa, chini hutandikwa ngozi ya ng'ombe halafu yeye huzikwa hapo na baada ya siku nne watu huchinja ng'ombe wanne, mbuzi saba, na kulala nje siku mbili kumuaga. Anasema hayo ni maelezo kwa ufupi ya wakurya toka wanapozaliwa, wanapofanyiwa tohara, uchumba, ndoa harusi mpaka kifo.
Msikilizaji wetu mwingine Richard Chenibei Mateka wa sanduku la barua 65, Kapkateny Mlima Elgon Kenya, naye ametuletea barua yenye maelezo kuhusu kabila lake la Sabot. Anasema kabila hili ni moja kati ya makabila ya kalenjin, ya watu wanaoishi kwenye maeneo karibu mlima Elgon na Transoia Magharibi mwa Kenya. Ni jamii ndogo iliyo na mila na desturi zake za maisha tokea enzi za zamani hadi sasa, kwani wanaamini anayeacha mila zake ni mtumwa na wanaishi wakienda kwa wakati na maendeleo yake.
Wasabaot wanapenda kuishi kwenye Miinuko, juu ya milima, kandokando ya mapango na misitu ya kiasili huku makabila mengine yakiishi chini yao sehemu tambarare. Wasabot wengi ni wakulima na wafugaji, hivyo basi sehemu yao ya juu kuna nyasi kwa ajili ya mifugo na maji na kivutio cha mvua yaani misitu kwa ukulima bora. Wasabaot hupenda sana ugali wa mahindi, nyama, maziwa na asali. Mboga za kienyeji wanazotumia zaidi ni Sakaa, Sujaa na Malenge. Vyakula hivi huzuia mgonjwa mbalimbali, hujenga mifupa yenye nguvu na humfanya mtu aishi kwa miaka mingi.
Watoto wenye umri wa miaka kumi na mitano wa kiume hufanyiwa sherehe baada ya kufanyiwa tohara ikiwa ni ishara ya kutoka kwa utoto hadi utu uzima ili kujitegemea na kulinda jamii. Vijana hupewa ushauri na wazee wa mtaa, wazazi ili waishi maisha bora na marefu hata bila wazazi wake. Sherehe kama hiyo hufanyika kila baada ya mwaka mmoja mwezi Desemba. Huu ndio wakati mlima Elgon hupata watalii, na wageni wengi huwa wanavutiwa sana na utamaduni wa wasabaot.
Huko milimani wasabot huishi kwenye vyumba vilivyojengwa kwa ustadi kwa miti au mianzi na kukandikwa udongo. Mapaa ya nyumba zao huezekwa kwa nyasi au mabati ili kuleta joto ndani wakati wa misimu ya mvua mwezi wa nne, tano, saba na nane. Watu hawa pia hupenda sana majirani, marafiki na wageni. Kuna makabila mengi yanayoishi pamoja na wasabaot kama vile ndugu zao wapokot, wasebei, wateso, wabukusu na wakikuyu na wengine. Wao hula pamoja, hufanya kazi pamoja maana wanaamini kuwa umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.
Iwapo kuna maadui wanoingilia jamii hii ndogo, kuna watabiri wa mambo yajayo waitwao Orkooyik, wanaotoa habari mapema kabla ya adui kuja. Na kama vijana wanapokwenda kinyume na mila zao, wao huwarekebisha ili kudumisha upendo kati ya makabila yote.
Kwenye mila ya wasabaot watoto hupewa majina kulingana na wakati wa kuzaliwa, kama vile mchana mtoto wa kiume huitwa kibet na msichana huitwa chebet, usiku mtoto wa kike huitwa chepkwemoi na wa kiume huitwa kwemoi na mengine mengi. Mapacha wa kike huitwa chesiro na wa kiume huitwa chepkech na hawa hufanyiwa sherehe maalum kwani ni baraka kutoka kwa mungu kupata watoto wawili au watatu kwa wakati mmoja.
Wamisionari au wakristo walipoingia kwenye eneo lo miaka ya nyuma walileta neno la Mungu na elimu, hapo ndipo wasabaot wakaanza kutanguliza jina la kikristo mbele ya majina yao kuonesha kuwa wao ni wakristo. Majina ya mwanzo yanatoka kwenye Biblia au yanatoka kwenye nchi za ng'ambo. Anasema jina kama lake yaani Richard Chenibei, lina maana ya kumkumbuka Dk Richard Leakey kwa kazi aliyoifanya.
Anasema Wasabaot pia hupewa majina ya rika kutokana na kufanyiwa tohara. Kutokana na matendo yao mema huchukua muda wa miaka kumi kubadilishwa kwa jina la rika. Majina haya ya rika ni Cheepkuy, Mayneek, nyoonkiik, na soweek.
Jamii ya wasabaot haiwezi kuzuia kijana kuoa au kuolewa, bali familia ya msichana na mvulana huchunguzwa ili kupata mke au anayeweza kulima kwa bidii, mkarimu, mwenye elimu ya wastani na mwenye kulinda mali na mwenye kuheshimu wageni wote bila kujali kabila au rangi. Wanaamini kuwa, kama baraka kukaribisha wageni katika jamii, na siku moja unaweza kukaribisha malaika.
Pia anasema Wasabaot wanaamini Mungu Mmoja (yeeyin) ambaye ni mwenye uwezo na mamlaka yote. Na wanaishi milimani kwa kuamini kuwa milima iko karibu na mungu na huko ni rahisi mungu kuwasikia haraka wakati wa maombi yao, na makanisa mbalimbali yamejengwa milimani na waumini wote wanaabudu mungu mmoja.
Kwenye Mila na desturi za kisabaot, watu wote huamini kuwa kuna maisha baada ya kifo, mungu huponya kila aina ya magonjwa, mungu husikia maombi ya watu hata ukiomba kanisani, nyumbani, safarini, ugenini na hata ukiwa mahali popote duniani.
Wasabaot huishi na watu tofauti kama vile wasomali, watu wanaotoka Ulaya, na wanaotoka Asia kama vile wahindi, wachina, waarabu. Kuna ambao wamejenga miradi mbalimbali kwenye mlima Elgon, wao wanaona huu ni undugu na ujirani mwema. Na wanaamini kuwa ni vizuri kumpenda jirani kama nafasi yako.
Bwana Richard pia anasema kuwa anatukaribisha sote twende mlima Elgon, kujionea na kushuhudia maendeleo na maisha ya wasabaot na hali ya nchi inavyovutia na kupendeza kuwa makazi, kwa kilimo na ufugaji elimu na hata kuweka vitega uchumi.
Idhaa ya kiswahili 2004-11-16
|