Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-11-23 18:10:37    
Barua za wasikilizaji 1123

cri
    Leo tunawaletea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu na baadaye tutawaletea maelezo kuhusu msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa sanduku la barua 52483 Dubai Emirates ametuletea barua akisema kuwa, ushindi mkubwa wa wanamichezo wa China walioupata katika mashindano ya michezo ya Olimpiki yaliyomalizika mwishoni mwa mwezi August mwaka huu huko mjini Athens Ugiriki, kwa kweli ni jambo linalostahili kupongezwa sana.

    Anasema yeye binafsi alikuwa akijawa na furaha pale alipokuwa akiwaona wanamichezo hao hodari na waliojaa ukakamavu wa China, walipokuwa wakichukua nafasi za kwanza katika mashindano ya michezo mbalimbali na kutunukiwa medali za dhahabu.

    Bila shaka ushindi huo wa wanamichezo wa China katika mashindano ya michezo ya Olimpiki yaliyomalizika mjini Athens hivi karibuni na kuifanya China kuwa ni taifa lililochukua nafasi ya pili kwa kujinyakulia medali nyingi za dhahabu baada ya Marekani, kunaudhihirishia ulimwengu kwamba Jamhuri ya watu wa China, sio tu taifa kubwa kabisa ambalo lina uwezo wa kuandaa michezo mikubwa ya kimataifa kama vile Olimpiki, lakini pia ni moja kati ya mataifa makubwa yenye ufanisi wa hali ya juu katika fani ya kimichezo hapa duniani.

    Pia kuna usemi usemao, "Nyota njema huonekana asubuhi" hivyo ushindi huo mkubwa uliopatikana kwa wanamichezo wa China, unaweza kuhesabiwa kuwa ni dalili njema inayoashiria kufaulu kwa mashindano yajayo ya michezo ya Olimpiki ambayo yatafanyika mjini Beijing mwaka 2008. Na mwisho anasema angependa kutoa pongezi zake kwa wanamichezo wote wa China waliojipatia ushindi katika mashindano hayo ya michezo ya Olimpiki mjini Athens kupitia shairi langu fupi lifuatalo:

Hongereni! Hongereni! Wanamichezo wa China

Pongezi zipokeeni, Athens mlitajikana

Mlichopeleka nyumbani, Hakika chasifikana.

Hongereni! Hongereni! Wanamichezo wa China

Medali zenye thamani, Nyingi zaonekana

Mumezivaa shingoni, Nazo zapendeza sana

Hongereni! Hongereni! Wanamichezo wa China

Ushujaa wa moyoni, Vyema wajulikana

Ulizaa matumaini, Ushindi ukapatikana.

Hongereni! Hongereni! Wanamichezo wa China

Nyote mko furahani, Mikono mwashikamana

Ushindi ulio makini, Na wenye kufurahisha sana

    Tunashukuru sana kwa barua aliyotuletea Bwana Mbarouk Msabah pamoja na shairi lake la kuwapongeza wanamichezo wa China kupata mafanikio mema katika michezo ya Olimpiki ya Athens. Kwa kweli shairi hili limetusisimua sana.

    Msikilizaji wetu Oresmus Mwaniki Kiema wa Kenya ametuletea barua akisema kuwa, kwanza kabisa ana furaha kubwa sana kwa kumhusisha katika kipindi hiki cha Radio China Kimataifa. Sababu nyingine ni kuwa anafurahia sana kipindi cha salamu ambacho huwa hakimpiti kila wakati, na ambacho kimemwezesha kuwakumbuka wenzake wengi asiowafikia kila wakati. Lakini kwa kupitia cha salamu zenu kwake imemuwia rahisi kuwasiliana na wenzake kiurahisi sana.

    Kuhusu hali hiyo tunapenda kuwaelezea wasikilizaji wetu kuwa, salamu zenu tunazozipokea na kuzirusha hewani ni nyingi, lakini kila siku muda wa kipindi hiki cha salamu zenu ni wenye kikomo yaani dakika tatu hivi. Hivyo kila mara tunaweza kusoma kadi chache tu, na huwa hatuchagui kadi za kusoma, lakini tulipopata barua ya Bwana Oresmus Mwaniki Kiema ambayo alilalamika kuwa hatusomi kadi zake za salamu, ilibidi tupekue mara moja na kupata kadi zake na kuzisoma. Tunaomba mtuwie radhi kama wakati fulani mnaona tumekosea kupitia kadi zenu, lakini pia tunakaribisha maoni ya wasikilizaji wetu ili tuweze kuboresha zaidi kipindi hicho.

    Msikilizaji wetu huyo Bwana Kiema anasema pia katika barua yake hiyo kuwa, amefurahia picha na nakala tulizokuwa tukimtumia. Anasema hii inaonesha kwamba amekuwa akitambulika nchini China kama mmoja wa wasikilizaji wetu wa Kenya. Na mwisho anatushukuru kwa majibu la ombi lake la kadi za salamu, baada ya kuomba kadi za salamu ili aweze kuwasalimia jamaa na marafiki wengi, kupitia kipindi cha salamu zenu cha radio China kimataifa. Anasema hatasahau kuwapongeza wafanyakazi wote wa Radio China kimataifa kwa kazi yao nzuri ya kushirikiana kwa karibu na wasikilizaji.

Idhaa ya Kiswahili 2004-11-23