Karafuu ni zao linalotokana na mkarafuu, ingawa karafuu hazimo katika kundi la vyakula wala vinywaji, lakini ni kiungo muhimu sana. Karafuu zina matumizi kadha, wakati fulani zinatumika kwenye utengenezaji wa sigara, upishi, utengenezaji wa aina fulani ya dawa ya meno, na pia mafuta yake hutumika kwa kuchua misuli.
Kutokana na kitabu cha historia, mikarafuu ilianza kupandwa kwenye visiwa vya Shelisheli, Mauritius na sehemu nyinginezo. Miche ya mkarafuu ililetwa Zanzibar kutoka Mauritius mwaka 1818, miti hii imestawi zaidi Visiwani Unguja na Pemba ambavyo vinatoa asilimia 80 ya karafuu zinazohitajika duniani. Na uchumi wa visiwa vya Zanzibar unategemea sana zao la karafuu.
Meneja masoko wa shirika la biashara la taifa la Zanzibar ZSTC Bwana Suleiman Juma Jongo alisimulia kwa undani kidogo kuhusu historia ya kilimo cha karafuu na hali ya upandaji wa mikarafuu visiwani Zanzibar. Alisema kuwa:
"Historia ya upandaji wa karafuu visiwani imeanza zamani sana. Miche ya mikarafuu kuja kwake hapa imetokana na visiwa vya Indonesia, mashariki ya mbali, ilifika huko Madagasca na shelisheli katika karne ya 19, na ndiyo ikakuja hapa kwetu Zanzibar na kupandwa wakati wafalme wa Oman walipotawala hapa. Kimbunga kiliwahi kutokea na na kiling'oa mikarafuu mingi. Kwa hivyo kukawa na juhudi mpya ya wafalme wa wakati ule ya kupanda mikarafuu mipya. Lilikuwa si kitu hiari, bali lilikuwa lakini ni jambo la lazima, watu wapande mikarafuu kwa sababu kitu hicho kinasaidia uchumi."
"Kabla ya mapinduzi, mashamba ya mikarafuu yalikuwa ni ya watu binafsi, lakini baada ya mapinduzi, serikali ilitaifisha ardhi na kuigawakwa wananchi. Kila mwananchi alipata eka tatu za kumwezesha kulima, kupata chakula chake, na kupata mahitaji yake ili ajiendeleze na familia yake. Na hiyo imeendelea mpaka leo, kwa hiyo sasa suala la karafuu linamilikiwa na wananchi wenyewe. Idadi kubwa ya mashamba yalikuwepo ni ya wananchi wenyewe. Ingawa kuna maeneo ya serikali, maeneo yanayomilikiwa na serikali ambayo yana karafuu na serikali inawakodisha watu ambao wanataka kukodi, kuchuma na kuuza, mashamba hayo yapo Zanzibar na Pemba."
Bwana Jongo aliongeza kuwa:
"Sasa utaratibu wa upandaji wa zao la karafuu bado unashughulikiwa na wizara ya kilimo, wizara ya kilimo ndiyo yenye idara maalum ya kuendeleza mazao haya ya biashara. Sasa wizara ya kilimo ndiyo inashughulika kuwa na vitalu vya miche ya karafuu."
"Kwa kuwa ZSTC ndiyo inayoshughulikia zao la karafuu, serikali kupitia wizara ya biashara ya ZSTC inachangia maendeleo ya zao la karafuu. Inawalipa vibarua wanaoshughulikia kuendeleza upandaji wa mikarafuu mipya katika sehemu mbalimbali ambazo mikarafuu imekufa, ZSTC inanunua zana za kutengeneza miche na kupanda miche mpaka kuisambaza kwa wananchi."
Bibi Mosesev Hatibu amefanya kazi katika taasisi ya utafiti wa kilimo ya Zanzibar Unguja, anaelezea kwa undani jinsi ya kuotesha miche ya karafuu na jinsi ya kutunza shamba la mikarafuu. Alisema kuwa:
"Kwanza unatayarisha eneo lako, unapiga tuta kisha unaweka mbolea, halafu unachukua majani makavu yaliyotokea katika mikarafuu. Unapiga mistari unaweka zile mbegu za mikarafuu ambayo ni matende. Ukisha panda unafunika majani makavu ya mkarafuu, unamwagilia maji halafu unaweka kivuli, unapalilia kila baada ya wiki. Baada ya mwezi mmoja, matende tayari yashaanza kuchipua, unaiacha miche yako vile mpaka itimie miezi miwili. Baada ya miezi miwili, unaenda kung'oa unachukua kimoja kimoja pamoja na kile kitende chake kile ambacho ni mchele mkarafuu uliochipua, unauchukua na kuuweka kwenye mifuko, na mifuko hiyo inakuwa imewekwa udongo ambao umechanganya na mbolea, halafu unachukua "humus" ambayo ni takataka zenye mbolea, una mchanganyiko huu unaweka kwenye mifuko."
"Unapandikiza miche yako, miche yako unaitunza inakaa kwa muda wa miezi mitatu mpaka minne. Miche yako imeshakuwa tayari, imeshakuwa mikubwa ina majani sita mpaka manane unaiacha kwa miezi sita, baada ya miezi sita miche yako inakuwa tayari kwa kupelekwa shambani. Katika msimu wa mvua wa masika au vuli, unakwenda kupiga mashimo unapanda, sasa katika kupanda shambani mikarafuu mimi nashauri wakulima wapande na mazao mengine kwa ili shamba la mikarafuu liwe safi, wapande mihogo au migomba ili kupata kivuli na shamba liwe safi sio wapande mikarafuu mitupu."
Idhaa ya Kiswahili 2004-11-30
|