Watu wenye virusi vya Ukimwi wanaotibiwa katika hospitali ya You An mjini Beijing tarehe 27 walifanya maonesho ya picha za kuchorwa katika Klabu ya Kimataifa ya Beijing, watu waliohudhuria ufunguzi wa maonesho hayo walikuwa ni ofisa wa Shirika la Kupambana na Ukimwi la Umoja wa Mataifa, UNAIDS, wajumbe wa jumuiya zisizo za serikali na wanamashirika mashuhuri kutoka Shanghai.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari mwandaaji wa maonesho hayo Bw. Song Pengfei alisema, "mada ya maonesho yetu ni kufahamisha Ukimwi ulivyo, kuondoa unyenyepaa wa watu kwa wagonjwa na wenye virusi wa Ukimwi na kusisitiza kuwa hali ya kutokuwa na usawa kati ya wanaume na wanawake inaweza kuleta madhara kwa jamii."
Katika mahojiano na vyombo vya habari, bwana Song mwembamba alisema wazi kuwa yeye ana virusi vya Ukimwi lakini hana moyo wa kujidhalilisha bali kwa heshima anawakilisha jumuiya ya wagonjwa wa Ukimwi kujiokoa na kushiriki katika shughuli hiyo ya jamii.
Bw. Song Pengfei alisema, "katika muda wa zaidi ya mwaka mmoja uliopita, wagonjwa na wenye virusi vya Ukimwi katika sehemu mbalimbali nchini China walishiriki katika shughuli mbalimbali za uenezi wa elimu kuhusu kinga ya Ukimwi, takriban katika kila mkoa kuna jumuiya za wagonjwa wa Ukimwi na baadhi zimepata fedha kutoka kwa serikali, hili ni jambo zuri."
Tarehe mosi Desemba mwaka huu ni siku ya kupambana na Ukimwi duniani mwaka wa 17, shughuli za kueneza elimu kuhusu kinga ya Ukimwi zinazofanywa na jumuiya hizo za umma zimepamba moto nchini China.
VCD inayojulikana kwa jina la "Maisha Yetu" iliyotengenezwa na Shirikisho la Wagonjwa wa Ukimwi la China ilizinduliwa tarehe 24, na kitabu cha "Maelezo ya Mgonjwa wa Ukimwi" kilichodhaminiwa na shirikisho hilo kilichapishwa na kitasambazwa bure katika Chuo Kikuu cha Beijing. Watu 30 wenye virusi vya Ukimwi mkoani Sichuan wataonesha michezo yao ya sanaa wakiwa pamoja na msanii mkubwa Pu Cunxin katika tarehe mosi Desemba.
Ofisa wa Shirika la Kupambana na Ukimwi la Umoja wa Mataifa alisema, "Hivi sasa habari inayofuatiliwa sana duniani sio tena watu wa mkoa wa Henan walioambukizwa kwa kuuza damu zao bali ni wagonjwa wa Ukimwi waliowahi kuhofia vifo na kudhalilishwa katika jamii wamejitokeza kufanya uenezi wa elimu ya kinga ya Ukimwi."
Kutokana na takwimu zilizotolewa na serikali ya China, tokea mgonjwa wa kwanza wa Ukimwi kutokea nchini humo mwaka 1985 hadi sasa waongjwa wa Ukimwi wameongezeka hadi laki 8.4. Mazingira yao ya kuishi yamewahi kuelezwa na Wizara ya Afya ya China, kwamba wakazi wa mijini na vijijini wanaendelea kuwa na hofu na kuonesha unyenyepaa kwa wagonjwa wa Ukimwi, wanachukua "tahadhari kubwa" kwa wagojwa wanaojitokeza hadharani. Vijijini asilimia 63.3 ya watu wana tahadhari hiyo, na karibu nusu ya wakulima hawakubali wagojwa wa Ukimwi kusoma shuleni na kuficha ugonjwa wao kazini, na asilimia 67.9 ya watu vijijini hawataki kushirikiana kikazi pamoja na wagonjwa hao.
Bw. Song Pengfei amebainisha kuwa jumuiya za wagonjwa wa Ukimwi zinapoomba misaada kutoka kwa mashirika fulani ya China huwa zinakataliwa, tofauti na hali hiyo, mashirika ya nchi za nje yanafurahia kutoa misaada.
Bw. Song alisema, "Wagonjwa wa Ukimwi wana uchungu mioyoni, shughuli za jumuiya zao kwa upande mmoja ni kwa ajili ya kujiokoa na kuwasaidia wao kurudi kwenye jamii, kwa upande mwingine ni kwa jili ya kueneza elimu ya kinga ya Ukimwi."
Kwa kweli tokea mwaka 2003 baada ya kutangazwa kwenye televisheni picha za waziri mkuu wa China Wen Jiabao kupeana na mkono na mgonjwa wa Ukimwi na rais wa zamani wa Marekani Clinton kukumbatiana na mgonjwa wa Ukimwi zilichangia sana kuondoa hofu ya umma kwa wagonjwa wa Ukimwi.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-01
|