Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-02 20:12:30    
Uganda kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika katika kinga na tiba ya ugonjwa wa ukimwi

cri

    Rais Yoweri Museveni wa Uganda tarehe 29 Novemba alitangaza kwenye ufunguzi wa mkutano wa 3 wa Baraza la Uganda la wenzi wa ushirikiano katika mapambano dhidi ya ukimwi kuwa, kiwango cha maambukizi ya virusi vya ukimwi nchini Uganda kimepungua na kuwa asilimia 6 ya hivi sasa kutoka asilimia 18 ya mwanzoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita. Maarifa hayo ya Uganda yenye ufanisi yamekuwa mfano wa kuigwa kwa Bara la Afrika na nchi za sehemu nyingine.

    Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Umoja wa Mataifa zimeonesha kuwa, hivi sasa idadi ya wagonjwa wa ukimwi na watu walioambukizwa virusi vya ukimwi imefikia milioni 39.4 kote duniani. Hili ni ongezeko la watu milioni 1.6 kuliko mwaka 2003, na pia ni rekodi ya juu zaidi kuliko nyingine katika historia. Inakadiriwa kuwa watu milioni 3.1 wamekufa kwa ugonjwa wa ukimwi mwaka 2004, hili ni ongezeko la watu laki 2 kuliko mwaka 2003, ambalo pia ni rekodi ya juu zaidi. Mwaka 2004, watu walioambukizwa virusi vya ukimwi waliongezeka kwa milioni 4.9, kiasi hiki pia kimezidi kile cha mwaka 2003. Kwa kuwa mpaka hivi sasa hata idara za tiba za kimataifa bado hazijapata dawa mwafaka ya kutibu ugonjwa wa ukimwi, hivyo ugonjwa huo bado unaitwa kuwa "mauaji duniani".

    Uganda iliyoko Afrika ya mashariki ni sehemu yenye wagonjwa wengi wa ukimwi. Tangu kugunduliwa kwa mgonjwa wa kwanza mwaka 1982, watu milioni moja wa nchi hiyo wamekufa kwa maradhi yanayohusika na ukimwi, na hivi sasa nchini humo bado kuna wagonjwa wa ukimwi au watu walioambukizwa virusi vya ukimwi wapatao milioni 1.1, na wengi kati yao ni vijana na watu wa makamo wenye umri wa miaka kati ya 15 na 45. Ugonjwa wa ukimwi umesababisha watoto yatima milioni 2 kwa nchi hiyo. Mwaka jana tu, watu elfu 70 walikufa kwa ugonjwa wa ukimwi, na watu elfu 75 waliambukizwa virusi vya ukimwi.

    Lakini serikali ya Uganda na wananchi wake wamefanya juhudi katika zaidi ya miaka 10 iliyopita, ugonjwa wa ukimwi umedhibitiwa katika nchi hiyo. Hivi sasa kiwango cha maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa watu wazima nchini Uganda kimepungua na kuwa asilimia 6. Hiki ni kiwango cha chini kuliko kile cha nchi nyingine za Afrika. Uganda imefanikiwa kupambana na ugonjwa wa ukimwi, uzoefu wake umesifiwa na jumuiya ya kimataifa, Uganda imesifiwa kuwa mfano wa kuigwa wa kudhibiti ukimwi barani Afrika. Mwaka 1998 Shirika la afya duniani liliipa Uganda "tuzo ya kutoa mchango mkubwa kwa kuhimiza afya barani Afrika"; mwaka 2000 shirika la kupambana na UKIMWI la Umoja wa Mataifa lilimpa rais Museveni wa Uganda "tuzo ya kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika kinga na tiba ya ukimwi duniani.

    Je Uganda ilichukua hatua gani za kupunguza kwa haraka kiwango cha maambukizi ya ukimwi na namna ya kupata mafanikio katika kinga ya ukimwi? Kama rais Museveni alivyosisitiza mara kwa mara kuwa, maambukizi ya virusi vya ukimwi yanapitia hasa shughuli za binadamu wenyewe, wananchi wakihamasishwa ndipo maambukizi ya ugonjwa yanapoweza kudhibitiwa. Hivyo serikali ya Uganda inasisitiza kubadili mwenendo hasa kwa vijana, yaani kutetea kuishi maisha ya kusaidia afya, kukwepa na vitendo vinavyoathiri afya na kuwa na maadili mazuri. Kwa ufupi, hatua za serikali ya Uganda zinaitwa ABC (ufupisho wa maneno ya kiingereza ya "kupunguza maisha ya kujamiiana", "kuwa mwaminifu kwa mpenzi" na "kutumia kondomu"), ambapo inawataka vijana kutofanya vitendo vya kujamiiana kabla ya ndoa, kuwa waaminifu kwa wake au waume baada ya ndoa, na kutumia kwa usahihi kondomu. Rais Museveni alipozungumza na vijana, wanafunzi na askari alisisitiza mara kwa mara na kuwataka wawe na maadili mazuri na kubadili tabia zao mbaya. Mawazo hayo mapya ya maadili yameungwa mkono na watu wa idara za utamaduni. Njia hiyo mwafaka ya kukinga ukimwi imesifiwa na waganda kuwa ni "chanjo mwafaka ya ugonjwa wa ukimwi".

    Serikali ya Uganda inachukulia kazi ya kupambana na ugonjwa wa ukimwi kuwa kazi ya dharura na ya muda mrefu ya serikali. Katika miaka zaidi ya 10 iliyopita, Uganda imepata mafanikio mengi makubwa. Mwaka 1986 iliiweka kinga ya ukimwi kwenye mpango wa maendeleo ya nchi katika mpango wa udhibiti wa ukimwi kote nchini, huu ni mpango wa kwanza ulioanzishwa barani Afrika. Mwaka 1990, Uganda ilianzisha kituo cha kwanza barani Afrika cha utoaji ushauri wa ukimwi na upimaji wa hiari. Mwaka 1992 Uganda ilianzisha kamati ya ukimwi ya nchi nzima ili kuratibu na kusimamia utekelezaji wa mikakati kuhusu ugonjwa wa ukimwi, kamati hiyo pia ni kamati maalum kuhusu ukimwi iliyoanzishwa mara ya kwanza barani Afrika. Mwaka 2001, Uganda ilitangulia kukamilisha majaribio ya chanjo ya virusi vya ukimwi kwenye hospitali. Mwezi Oktoba mwaka huu Uganda ilianzisha kituo cha mafunzo ya madaktari na wauguzi maalum wa ugonjwa wa ukimwi, ambacho ni kikubwa kabisa kwenye sehemu ya kusini mwa Afrika.

    Ingawa Uganda bado inakabiliwa na kazi ngumu na changamoto kubwa katika kupambana na ukimwi, lakini kama itaendelea kuchukua sera ya kuzingatia kwanza kinga ya ugonjwa, bila shaka itapata mafanikio mapya katika kudhibiti ugonjwa wa ukimwi.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-02