Mto Manjano ni mto wa pili kwa urefu nchini China. Chanzo chake kiko kwenye bonde la Yueguzonglie lililoko kaskazini ya mlima Bayankela kwenye uwanda wa juu wa Qinghai. Mto huo unaingia kwenye Bahari ya Bohai kupitia uwanda wa juu wa udongo manjano na tambarare ya Mto manjano, Mto Huai na Mto Hai. Urefu wa tawi lake kuu ni kilomita 5464, tofauti ya urefu wa kwenda juu kati ya sehemu ya mwanzo na ya chini ni mita 4480, na eneo la bonde la mto huo ni kilomita za mraba laki 7.95.
Kufuatana na utafiti wa historia ya mabadiliko ya kijiografia, Mto Manjano ni mto wenye historia fupi. Kabla ya miaka milioni 1.15 iliyopita, katika eneo hilo kulikuwa na maziwa kadhaa tu, na kila ziwa lilikuwa na mifumo yake ya mito. Kufuatana na kuongezeka kwa urefu kutoka usawa wa bahari wa uwanda wa juu wa sehemu ya magharibi na mabadiliko ya mito, baada ya miaka milioni 1.05 maziwa hayo yalianza kuungana pamoja na umbo la asili la Mto Manjano likaanza kutokea. Kuanzia miaka laki 1 hadi miaka elfu 10 iliyopita, Mto Manjano ulikuwa mto mkubwa ulioingia baharini.
Kwa sababu maji ya Mto Manjano ni yenye udongo na mchanga mwingi ambao hurundikana haraka katika tambarare ya sehemu ya chini ya mto, tawi kuu la mto huo hubadilisha njia yake mara kwa mara. Watu walianza kujenga kingo za kuzuia mafuriko ya maji, lakini udongo na mchanga unaendelea kurundika na kusababisha sehemu ya chini ya mto kuendelea kuinuliwa, na mto huo ukawa mto mwenye kitanda kilichoko juu ya ardhi. Sehemu ya mwisho ya mto huo inafurika na kubadili njia yake mara kwa mara. Hali hiyo ni nadra sana kutokea duniani. Kufuatana na rekodi za kihistoria, katika kipindi cha miaka zaidi ya 1700 kuanzia mwaka 602 BC katika enzi ya Zhou hadi kufikia mwaka 1128 AD katika enzi ya Song ya Kusini, mto huo ulibadili njia yake katika sehemu iliyoko kaskazini ya njia yake ya sasa na kuingia kwenye bahari ya Bohai kupitia mto Haihe. Na katika kipindi cha miaka zaidi ya 700 kuanzia mwaka 1128 hadi 1855, mto huo ulibadili njia yake katika sehemu iliyoko kusini ya njia yake ya sasa na kuingia kwenye bahari ya Huanghai kupitia mto Huaihe. Mwaka 1855, mto huo ulibomoa kingo huko Dongbaitou, Lankao mkoani Henan, na kuanza kupita kwenye njia yake ya sasa, yaani kuingia kwenye bahari ya Bohai kupitia mto wa Daqinghe mkoani Shandong. Kutokana na mabadiliko ya njia ya mto na athari ya bahari, urefu na eneo la bonde la sehemu ya chini ya mto huo linaendelea kubadilika. Na hii ni tofauti kubwa kati ya mto huo na mito mingine.
Katika zama za kale, sehemu ya mwisho ya mto Manjano ilikuwa ni sehemu nzuri sana kwa maisha ya mababu-jadi kutokana na hali nzuri ya hewa na mvua nyingi. Na ardhi ya uwanda wa juu wa udongo manjano na tambarare ya sehemu ya chini ya mto huo inafaa sana maendeleo ya kilimo na ufugaji. Pia udongo manjano uliwafaa mababu-jadi kuchimba mapango na kuishi ndani yake. Mazingira hayo yalileta nafasi nzuri kwa maendeleo ya utamaduni wa kale nchini China. Kabla ya miaka milioni 1.1, mababu-jadi wa Lantian walianza kuishi katika bonde la mto huo. Na mababu-jadi wa Dali, Dingcun na Hetao pia waliwahi kuishi hapo. Masalio ya utamaduni wa kale wa Yangshao, Majiayao, Dawenkou na Longshan yamesambaa katika sehemu hiyo. Si kama tu masalio hayo ni mengi sana na ya aina nyingi, bali pia ni masalio ya utamaduni wa vipindi vya mfululizo, ambayo yanaweza kuonesha kimfumo maendeleo ya utamaduni wa kale wa China.
Katika historia ya China, kwa muda mrefu vituo vya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni viko katika bonde la mto Manjano. Sehemu ya kati na ya chini ya mto huo ni sehemu ambako sayansi, teknolojia, fasihi na sanaa za China zilipata maendeleo mapema zaidi. Kabla ya miaka elfu 2 iliyopita, vyombo vya shaba nyeusi vilianza kutengenezwa katika sehemu hiyo. Hadi kufikia enzi ya Shang, ufundi wa kuyeyusha shaba nyeusi ulikuwa wa hali ya juu. Na vyombo vya chuma pia vilianza kutengenezwa, ambavyo vimeonesha kuwa wakati huo nguvu ya uzalishaji ilifikia kiwango kipya. Majembe na mashoka ya chuma yaliyogunduliwa huko Luoyang yameonesha kuwa China ilivumbua teknolojia ya kulainishia chuma cha kusubu mapema kuliko nchi za Ulaya kwa miaka elfu 2. Na mavumbuzi manne, yaani utengenezaji wa karatasi, uchapaji wa mpangilio huru wa maneno, ufundi wa kutengeneza baruti na dira pia yalitokea katika sehemu hiyo. Aina nyingi mashuhuri za fasihi zikiwemo Kitabu cha Mashairi, mashairi ya enzi ya Tang na mashairi ya aina ya ci ya enzi ya Song, na vitabu vingi vya kiutamaduni pia vinatokea hapo. Baada ya enzi ya Song ya Kaskazini, kituo cha kiuchumi wa China kilianza kuhamia sehemu ya kusini, lakini katika maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni ya China, bonde la Mto Manjano bado linachukua nafasi muhimu. Historia ndefu ya mto huo imeipatia China urithi adimu na mabaki mengi ya kale, na ni fahari ya taifa la China.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-02
|