Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-03 21:39:55    
Hali ya biashara ya visiwani Zanzibar na changamoto inayowakabili wakulima kutokana na kushuka kwa bei ya karafuu kwenye soko la kimataifa

cri

    Bwana Issa Jalemia ni mkulima wa karafuu wa kijiji cha Dole, kisiwani Unguja, umbali wa kilomita 15 hivi kutoka Zanzibar, mji mkuu wa visiwani Zanzibar. Miaka mitano iliyopita, Bwana Issa alikodi eka tatu ya shamba kutoka serikalini kwa ajili ya kupanda mikarafuu. Sasa ameanza kuvuna, lakini kutokana na kushuka kwa bei ya karafuu kwenye soko la kimataifa, badala ya kupata faida yeye alipata hasara kubwa. Alisema:

    "Zao la karafuu kwa kusema ukweli kipindi hiki halina thamani kutokana na kazi kubwa na kipato kidogo kutokana na bei kushuka. Sasa utawakuta wakulima wengi hili zao sasa hivi wameliweka nyuma tofauti na zamani. Zamani kila mtu alikuwa akililia apate karafuu au akodi shamba la karafuu. Lakini sasa hivi hata upandaji wa wakulima umepungua. Kipindi cha nyuma zao lao la karafuu lilikuwa likitegemewa sana kwa kitega uchumi, lakini huu ni mwaka wa pili nimepata hasara kutokana na bei ya karafuu kushuka katika soko la dunia. Nyuma ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita bei ilitokea shilingi 3500 kwa kilo, lakini sasa hivi imeshika mpaka shilingi 1200. Sasa utamkuta mchumaji hapo analipwa shilingi 200 kwa kuonewa tu kwa sababu atashinda kutwa. Zamani labda mchumaji atapata shilingi 3000, anachuma mchana na jioni achambue, lakini sasa analala mpaka saa saba ya usiku."

    Bwana Jalemia aliongeza kusema kuwa: "Sasa kwa kweli wakulima wanalia, sasa utakuta hili zao karibu linaweza kutoweka kwa sababu mikarafuu inakauka, na watu wakiipanda wanarudi nyuma, tegemeo la zao la Unguja sasa hivi linarudi nyuma."

    "Mwaka jana, nilikodi shamba la karafuu kwa shilingi milioni tatu, mapato yangu yakaanguka mpaka nikapata hasara, nilipata shilingi milioni moja na laki mbili. Mwaka huu nimekodi shamba kwa shilingi milioni moja na laki moja, lakini mapato yenyewe ninayoyategemea ni kidogo tu. Kwa hivyo kubwa zaidi tunasikitika katika mashirika ya kimataifa yanayoendelea kushusha bei namna hii. Wanakuwa wanatuumiza sisi wanyonge. Kwa hiyo kilio chetu hatulilii katika serikali yetu, tunalilia huko nje katika soko la dunia. Likishusha bei, lisishushe kwa kiasi kikubwa. Kwani tunakuwa tumeshazitoa akiba zetu ndani ya majumba kukodi vitu kama hivi. Leo moja kwa moja ukishusha bei na mnyonge unamrudisha nyuma hata kiimani. Kwa sababu binadamu wana imani sasa ukimkatisha tamaa na imani yake inakuwa inaondoka, kwa serikali ya nchi na kwa Umoja wa Mataifa."

    Kutokana na utaratibu, mtu binafsi visiwani Zanzibar haruhusiwi kushughulikia uuzaji wa zao la karafuu kwa nchi za nje, biashara ya karafuu ya visiwa vya Zanzibar inashughulikiwa tu na serikali kwa kupitia shirika la biashara la taifa la Zanzibar ZSTC.

    Meneja masoko wa Shirika hilo Bwana Suleiman Juma Jongo alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari kuhusu hali ya biashara ya zao la karafuu visiwani Zanzibar alisema :

    "Kwa sheria mpaka sasa hivi iliyopo ni kwamba, karafuu haijaruhusiwa kushughulikiwa na watu binafsi, kama ilivyo mazao mengine ya pilipili hoho, mwani na kombe. Karafuu bado inashughulikiwa na serikali kwa kupitia ZSTC."

    "Sasa jukumu letu sisi ni kuhakikisha karafuu yote inayolimwa na wananchi tunainunua na kuiuza nje. Sasa katika kununua tulikuwa mara nyingi tunatazama bei ya nje inakuwa iko katika hali gani, kwa sababu hatuwezi tu kutoa bei kwa wakulima wakati bei yenyewe ya kuiuza nje ni ndogo. Ni kweli kuna muda bei inakuwa kubwa, na tunawapa wakulima bei nzuri, na kuna muda bei inakuwa ndogo na hatuna la kufanya, hatuwezi kusema kwamba tuchukue pesa tuwape wakati huko nje bei inakuwa ndogo. Hatuwezi kutoa ruzuku kiasi kikubwa."

    "Kwa mfano katika majira ya 2000/2001, sisi tulikadiria tutanunua kutoka kwa wakulima tani 2900, lakini tulipata tani 300 tu, hiyo ina maana pengine bei tuliyokuwa tukitoa sisi inaweza ndogo lakini bei ya nje pia ni ndogo. Lakini kuna jambo moja ambalo linatufanya tusitoe bei kubwa. Wananchi siku zote wanaitegemea ZSTC isisite hata mara moja kununua karafuu zao, hata kama bei ya nje imeshuka. Sasa bei imeshuka ZSTC iendelee kununua, na kwa kuwa unanunua, lakini huwezi kuuza kwa sababu bei imeshuka, bila shaka unachokinunua itabidi ukiweke ukihifadhi angalau ungoje hali ya bei inapotengemaa. Sasa katika ile kipindi hicho bila shaka inahitaji pesa za kuzihifadhi karafuu hizo."

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-01