Msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa sanduku la posta 161 Bariadi Shinyanga Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, salaam nyingi zenye bashasha na furaha ziwafikie wachina wote pamoja na serikali yao inayoongozwa na chama cha kikomunisti cha China. Salaam hizi zinatoka Afrika, hasa kutoka katika nchi iliyo rafiki mkubwa kabisa wa China kwenye eneo hili la Afrika mashariki nayo ijulikanayo kuwa ni Tanzania. Tanzania ni muungano wa nchi mbili huru katika Afrika. Wananchi wa Tanzania kama ilivyo wananchi wenzao wa Jamhuri ya watu wa China wanaamini kwamba "umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu", anasema ndiyo maana watanzania wamebaki wamoja na wataendelea kubaki wamoja karne na karne. Watanzania dua zao siku zote kuhusu taifa la China ni kuona China yenye umoja na mshikamano. Kwa sababu hii tutaendelea kuunga mkono muungano wa amani baina ya China bara na Taiwan, Amina.
Tarehe mosi Oktoba mwaka huu wa 2004 China mpya imeadhimisha miaka 55 tangu kuzaliwa kwake. Tukio hili ni kubwa na jambo la kujivunia kwa wachina wote na watu wote wanaopenda amani na maendeleo katika dunia nzima, wakiwemo ndugu na marafiki wakubwa wa China yaani watanzania,
Anasema anatoa pongezi kwa Radio China kimataifa kwa kuanzisha mashindano ya chemsha bongo kuhusu ujuzi wa miaka 55 ya China mpya. Anasema akiwa msikilizaji wa uhakika wa Radio China kimataifa, anapenda aseme kuwa ameshiriki kikamilifu katika mashindano hayo yaliyoandaliwa maalum kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 55 ya China mpya. Mageuzi ya kiuchumi na kuzifungulia mlango nchi za nje kumeleta maendeleo na mafanikio makubwa sana nchini China.
Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya China yameleta taathira kubwa sana siyo katika China tu, lakini katika dunia nzima, ndio maana inatubidi kusifu na kuyanadi mafanikio ya China katika nyanja zote mahali popote na wakati wowote.
Anasema nakala hii ameandika ili kuonesha furaha yake kubwa kuhusu maadhimisho ya miaka 55 tangu kuzaliwa kwa China mpya tarehe mosi Oktoba mwaka huu wa 2004. Hii ni makala ya utangulizi makala mahsusi ataiandaa na kuituma Radio China kimataifa, anakamilisha makala hii kwa kusema kuwa China idumu milele na amani italeta duniani kote.
Msikilizaji wetu Kilulu Kulwa anasema katika barua yake nyingine kuwa, wahariri na watangazaji wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa pokeeni salaam nyingi kutoka Tanzania, yeye msikilizaji wetu mzima sana ni matumaini yake kuwa sisi watangazaji pia tu wazima wa afya njema.
Anasema anapenda kutuma fursa hii kutushukuru sana kwa juhudi kubwa tunazozifanya kwa ajili ya kuwahudumia vyema wasikilizaji wetu kwa kuwatangazia vipindi maalum na habari motomoto katika idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa. Vipindi kama vile Sanduku la barua, Daraja la urafiki kati ya China na Afrika, Klabu ya utamaduni, Tazama China, Elimu na afya, Wapenzi wa michezo, kwa kweli vipindi hivyo ambavyo siku zote hutanguliwa na taarifa ya habari na maelezo baada ya habari vinawapatia ujuzi na maarifa mengi kuhusu taifa la China na ulimwengu mzima. Hivyo hatuna budi kuwashukuru sana. Aidha anapenda kutueleza kuwa katika kipindi cha sanduku la barua cha tarehe 12 mwezi Septemba mwaka huu wa 2004 pamoja na mambo mengine mtangazaji aliweza kunukuu barua yake aliyokuwa ametutumia siku za nyuma. Hakika alifurahi sana kwa kuwa hii inawatia moyo sana wasikilizaji wetu na kuzidi kuwa tayari kutoa michango mbalimbali ya mawazo na ushauri na kuiwasilisha idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa. Akiwa msikilizaji wa siku nyingi wa Radio China kimataifa anaahidi kuendelea kuwa msikilizaji mwaminifu na kushiriki kikamilifu kusikiliza na kushiriki katika chemsha bongo ya mashindano ya ujuzi yanayotolewa na kuandaliwa na Radio China kimataifa takribani kila mwaka. Katika mwaka huu wa 2004 ambapo Radio China kimataifa imewaletea mashindano ya ujuzi kuhusu miaka 55 ya kuasisiwa kwa China mpya. Anasema, sisi wasikilizaji wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, tutaiunga mkono sana Radio China kimataifa, serikali ya China na wananchi wote wa Jamhuri ya watu wa China na hivyo taifa kuzidi kuwa na umoja na mshikamano.
Msikilizaji wetu Yaaqub Saidi wa sanduku la posta 2519 Kakamega Kenya ametuletea barua akisema kuwa, pokeeni salaam nyingi kutoka kwake akitarajia sisi wazima kwa uwezo na nguvu zake mwenyezi mungu. Anasema lengo na madhumuni ya kutuandikia barua hii ni kuwapongeza watangazaji na wasimamizi wa Radio China kimataifa kwa kazi yetu nzuri na kwa zawadi zetu kwake za mara kwa mara , ambazo zimemwezesha yeye kuwashawishi marafiki zake wengi kujiunga na naye kuwa wasikilizaji na wanachama sugu wa Radio China kimataifa. Yeye akiwa mwanachama mkongwe wa Radio China kimataifa amefurahishwa sana na kipindi cha chemsha bongo ndicho chanzo chake yeye kuwapata marafiki ambao wameshiriki kwa kujibu maswali na kushiriki kwenye kipindi cha chemsha bongo.
Anasema anapenda kuwapongeza kwa kipindi hicho na mwenyezi mungu akitupa uhai mwaka ujao wa 2005 tutashiriki tena. Pia anawapongeza watangazaji kwa namna wanavyoendesha shughuli za kila siku hasa kwa kuzungumza kiswahili fasaha kwa kutumia mtiririko adimu wenye kuvutia ambapo wasikilizaji hupata matumaini na matarajio ya moja baada ya nyingine kwa kuelimisha, kuwafahamisha, kuwaburudisha na kuwashauri hasa kuhusu sayansi asilia, historia, siasa, michezo, uchumi na maendeleo, elimu na afya.
Hivyo anasema anatuomba tuendelee bila kuchoka au kufifia kwani wao wako sambamba nasi. Anamaliza kwa kusema hongera Radio China Kimataifa na idumu milele
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-07
|