China na Korea ya kusini ni nchi jirani ambazo zimetenganishwa kwa bahari. Kutokana na maendeleo ya uhusiano kati ya nchi hizi mbili, mawasiliano kati ya watu wa nchi hizo mbili yameongezeka siku hadi siku. Muda si mrefu uliopita, mwandishi wetu wa habari aliwakuta marafiki kadhaa waliokuwa na shauku kubwa ya kuielewa China.
Wachina wengi wanajifunza na kufanya kazi nchini Korea ya kusini. Ili kujua hali zaidi ya maisha ya wachina waishio nchini Korea ya kusini, mwandishi wetu wa habari alitaka kwenda mji wa Tezhen kutoka Pusan, na Bwana Choi Young alijitolea kumpeleka kwa kuendesha gari lake. Kusafiri kutoka Pusan hadi Tezhen unatumia muda wa saa nne hivi, njiani mwandishi wa habari na Bwana Choi Young walizungumzia mambo mengi. Bwana Choi alisema kuwa, yeye anaipenda sana China na utamaduni wake, na aliona kuwa China na Korea ya kusini zinashirikiana katika mambo mengi . Akisema:
"Najisikia vizuri sana ninapokutana na wachina kwa mara ya kwanza, si kama tu sisi sote tuna rangi na sura zinazofanana, bali pia mawazo yetu, historia yetu na utamaduni wetu vinalingana."
Bwana Choi alizaliwa katika mji wa Qiongzu, ambao ni mji maarufu wa kihistoria na kiutamaduni nchini Korea ya Kusini, alisema kuwa, anatarajia kuitembelea China, hasa mji wa Guilin, ambao unafanana sana na maskani yake Qiongzu kwa uzuri wa mandhari.
Kulingana kiutamaduni kati ya China na Korea ya kusini kunaonekana katika fani nyingi, kama vile utamaduni wa dini ya kibuddha. Bwana Wonteak ni kiongozi maarufu wa dini ya kibuddha nchini Korea ya kusini. Miaka 10 iliyopita, alialikwa kujiunga na shughuli za ukaguzi wa kiutamaduni kwa siku zaidi ya 20 nchini China. Katika safari yake hiyo nchini China, alifanya majadiliano na waumini wa dini ya Buddha. Pia aliwahi kutembelea sehemu nyingi zenye utamaduni wa kibuddha nchini China, kama vile mlima wa Wutai na mlima wa Emei. Alisema kuwa, sanamu za buddha zilizoko kwenye mlima wa Wutai, mkoani Shanxi zinafanana sana na sanamu za buddha zilizoko katika hekalu ya Bulkusen ya nchini mwake.
Kutokana na kulinganisha utamaduni kati ya China na Korea ya kusini, pamoja na kuimarika kwa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizi mbili, hivi sasa idadi ya wachina wanaojifunza Kikorea na wakorea wanaojifunza Kichina inaongezeka siku hadi siku. Kwon Hana ni msichana mrembo na mtulivu wa Korea ya kusini, mwaka huu amehitimu kutoka idhaa ya Kichina ya chuo kikuu nchini kwake, na sasa anafundisha Kichina katika shule ya sekondari mjini Seoul. Alisema:
"Katika shule yetu, wanafunzi wana uhuru wa kuchagua somo la lugha ya kigeni, karibu wanafunzi wote wanachagua Kichina kati ya lugha mbili za Kichina na Kijerumani. Hali hiyo inamaanisha kuwa, Kichina kinapendwa zaidi na wanafunzi wa Korea ya kusini. Naona fahari kuwa mwalimu wa kichina."
Na lengo la wanafunzi wengi wa chuo kikuu wanaojifunza lugha ya Kichina ni kutafuta ajira kwa urahisi. Bwana Park Bo Sun mwenye umri wa miaka 31 mwaka huu pia alihitimu masomo ya Kichina, alisema:
"Hivi sasa China inaendelea haraka, hivyo ina mvuto mkubwa kwa watu wengi wa Korea ya kusini. Wanaofahamu Kichina watapata fursa nyingi zaidi katika kutafuta ajira, na wana uwezo mkubwa zaidi wa ushindani katika jamii."
Bwana Park sasa anafanya kazi katika tawi moja la kampuni ya usafiri wa ndege ya Dongfang ya China huko Pusan. Alisema kuwa, kujifunza Kichina ni chaguo zuri kwake, na anafurahia kupata kazi hiyo.
Kati ya watu wanaopenda kujifunza Kichina, mzee Oh Tae Soo mwenye umri zaidi ya miaka 60 mwaka huu amempa mwandishi wa habari picha nzuri sana. Mzee Oh na mke wake wamekuwa wakifanya kazi kwenye duka la wanyama vipenzi kwa miaka 15. Miaka mitatu iliyopita, walifungua duka lingine mjini Harbin, mji maarufu ulioko kaskazini mashariki mwa China. Ili kuwasiliana vizuri na wachina, mzee Oh alijaribu kujifunza Kichina. Alisema kuwa, wachina ni wakarimu na waaminifu, anapenda sana kufanya biashara na wachina. Alisema:
"China ni mahali penye uhai mkubwa, soko la China ni kubwa, tena lina nafasi kubwa ya maendeleo."
Mzee Oh alisema kuwa, anaipenda sana China, hivyo yeye na mke wake wataishi maisha yao ya uzeeni nchini China.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-09
|