Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-09 19:47:55    
Mfereji wa Jinghang

cri

  

    Mfereji wa Jinghang unaojulikana duniani ni mfereji mrefu kabisa uliochimbwa zamani kabisa duniani.

    Mfereji huo unaanzia Beijing katika sehemu ya kaskazini na kufikia Hangzhou katika sehemu ya kusini. Unapitia mikoa ya Heibei, Shandong, Jiangsu na Zhejiang na miji ya Beijing na Tianjin, na kuungana na Mito Haihe, Manjano, Huaihe, Changjiang na Qiangtangjiang. Urefu wake ni kilomita 1794. Katika historia ya China, mfereji huo ulitoa mchango mkubwa katika usafirishaji na maingiliano ya kiuchumi na kiutamaduni kati ya sehemu ya kaskazini na kusini ya China.

     Mfereji wa Jinghang ulianza kuchimbwa mwaka 486 KK. Mwaka 1293, yaani ulitumia miaka 1779 kabla ya kutumika kwa usafirishaji. Katika kipindi hicho kirefu, kwa ujumla miradi mitatu mikubwa ya uchimbaji ilifanyika.

     Mradi wa kwanza ulianzia mwishoni mwa enzi ya Spring na Autumn karne 5 KK. Wakati huo, mfalme Fuchai wa dola la Wu iliyokuwa katika sehemu ya chini ya Mto Changjiang aliwakusanya wafanyakazi kuchimba mfereji kuanzia mji wa Yangzhou, halafu kufikia Ziwa Sheyang na mwishoni kufikia Mto Huaihe huko Huai'an, ili kulipeleka jeshi lake kaskazini kuishambulia dola la Qi, na kugombea utawala wa sehemu ya kati ya China. Kutokana na mfereji huo kupita kwenye mji wa Hancheng, ulipewa jina la Han'gou. Urefu wa mfereji huo ni kilomita 170. Maji ya Mto Changjiang yanaweza kuingia kwenye Mto Huai kupitia mfereji huo. Na mfereji huo ni sehemu iliyochimbwa zamani zaidi ya Mfereji wa Jinghang.

     Mradi wa pili ulifanyika mwanzoni mwa karne 7 baada ya watawala wa Enzi ya Sui kuunganisha China nzima na kuufanya mji wa Luoyang kuwa mji mkuu wa China. Ili kuitawala sehemu kubwa ya kusini ya Mto Changjiang na kusafirisha bidhaa nyingi zilizozalishwa katika delta ya Mto Changjiang kwenda Luoyang, mwaka 603 mfalme Suiyang alitoa amri ya kuchimba mfereji wa Yongji wenye urefu wa kilomita 1000 kutoka Luoyang hadi kufikia Zhuojun (sehemu iliyoko kusini magharibi mwa Beijing kwa sasa) kupitia Linqing mkoani Shandong, na mwaka 605 alitoa amri ya kuchimba mfereji wa Tongluo wenye urefu wa kilomita 1000 kutoka Luoyang hadi Qingjiang (yaani mji wa Huaiyin wa sasa mkoani Jiangsu). Mwaka 610, mfereji wa sehemu iliyoko kusini ya Mto Changjiang wenye urefu wa kilomita 400 kutoka Zhenjiang mkoani Jiangsu hadi Hangzhou mkoani Zhejiang (ambao ilikuwa bandari ya biashara ya nje wakati huo) ulichimbwa, mfereji wa Han'gou pia ulitengenezwa upya. Baada ya hapo, mfereji wenye urefu zaidi ya kilomita 1700 ulimalizika.

     Mradi wa tatu ulianzia mwishoni mwa karne 13 baada ya watawala wa Enzi ya Yuan kuufanya mji wa Beijing kuwa mji mkuu wa China. Ili watu waweze kwenda kusini kutoka kaskazini moja kwa moja kuzunguka ya kutoka Luoyang, serikali ya Enzi ya Yuan ilitumia miaka 10 kuchimba Mfereji wa Luozhou na Mfereji wa Huitong ambayo iliunganisha pamoja mito na maziwa ya kimaumbile kati ya Tianjin na Qingjiang mkoani Jiangsu, na kufika kwenye mfereji wa Han'gou na Mfereji wa sehemu iliyoko kusini mwa Mto Changjiang, na mwishoni kufikia Hangzhou. Kutokana na kuharibika na kutotumika kwa mfereji uliochimbwa zamani kati ya Beijing na Tianjing, serikali ya Enzi ya Yuan pia ilichimba mfereji wa Tonghui. Baada ya hapo, urefu wa mfereji mpya kutoka Beijing hadi Hangzhou ulifupishwa kwa kilomita 900 kuliko mfereji wa zamani uliopitia Luoyang.

      Mfereji wa Jinghang ni njia kuu ya usafirishaji kati ya sehemu ya kaskazini na ya kusini, na katika historia umewahi kutoa mchango mkubwa ambao ulisifiwa kuwa nusu ya mali na kodi nchini China zilipelekwa katika mji mkuu kupitia njia hiyo. Na usafirishaji wa mto huo pia umesukuma mbele maendeleo ya miji iliyoko kando ya mfereji huo.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-09