Wakati wa sikukuu, wakulima wa Wilaya ya Pizhou, sehemu ya kaskazini ya Jimbo la Jiangsu hucheza ngoma ya simba. Wachezaji wawili wananyanyua sanamu ya simba huku wakicheza ngoma. Sanamu hiyo ina sehemu mbili: kichwa na kiwiliwili. Shi Shengrong na mkewe ni mafundi maarufu wa kutengeneza kichwa cha simba. Ufundi wao umekuwa ukirithiwa kwa vizazi vitano, kwa hivyo utengenezaji na maumbo ya kichwa cha simba umebaki kuwa ni sanaa ya jadi. Wakati wa msimu usio na kazi za kilimo, familia nzima inajumuika katika utengenezaji wa kichwa cha simba.
Utengenezaji unagawanyika katika hatua nne: Kufinyanga sanamu ya kichwa cha simba, kutengeneza kalibu, kuchora nakshi na kupamba. Kwanza kabisa, fundi anafinyanga sanamu ya kichwa cha simba kwa towe isiyopasuka kwa urahisi. Sanamu hii haifinyangwi kwa makini sana ila macho, pua na mdomo vinaonekana kwa udhahiri. Baada ya sanamu kukauka kabisa, fundi anatandaza karatasi ua bitana au anamwaga unga wa talki juu ya nyingine mpaka kufikia unene wa milimita nne; anaianika tena juani hadi ikauke kabisa; halafu anaivunja sanamu na kupata kitu kama fuvu la kichwa cha simba. Baada ya hapo, anachanganya gundi na lithopone, anapaka mchanganyiko huu kwenye fuvu, kisha anachora kwa rangi macho, pua, mdomo n.k.. Anachukua kamba ya katani ya kienyeji, anaitia rangi nyekundu na ya kijani, anakata kamba ya katani hiyo kuwa vipande vipande, anapachika vipande vya katani kwenye mzunguko wa fuvu ili vionekane kama ni mithili ya manyoya, mwisho anafunga kengele ndogo kwenye katani. Wakati wa kucheza ngoma, kengele inalia na manyoya mekundu ma ya kijani yanapepeapepea. Simba anaonekana kuwa hai, mkali na mwenye nguvu. Wenyeji wa hapa wanachukulia kichwa cha simba kuwa ni alama ya baraka na ya kuepukana na maafa na shetani. Familia nyingi zinatundika vichwa vya simba, kupamba nyumba.
Katika miaka hii ya karibuni, chini ya misaada ya ofisi ya utamaduni, wakulima wamebadili matumizi ya kichwa cha simba, wanakitumia kama pambo la nyumba.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-10
<>
1 2
|