Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-23 21:37:48    
Mkulima Yu Lianjiang anayetajirika kutokana na kilimo

cri

    Mwezi Desemba ni wa majira ya baridi, sehemu ya kaskazini mashariki mwa China, ambako ni sehemu muhimu inayozalisha nafaka nchini China hufunikwa na theluji. Mtu tunayemzungumzia katika kipindi hiki mkulima Yu Lianjiang na familia yake, wanaishi katika wilaya ya Nong'an, mkoani Jilin, katikati ya sehemu ya kaskazini mashariki nchini China.

    Nyumba ya Yu Lianjiang ni ya kijadi ya wakulima wa kaskazini mashariki mwa China: vyumba vinne maridadi vimepangwa kuelekea upande wa kusini, upande wa magharibi kuna kibanda cha bata bukini, zizi la nguruwe, na kibanda cha mbwa, upande wa mashariki ni sehemu ya kuwekea kuni. Theluji kubwa iliyoanguka muda si mrefu uliopita imezifunika nyumba hiyo na kuifanya ipendeze zaidi. Kitu kinachovutia zaidi ni mahindi yanayolundikwa uani, mahindi yenye rangi ya dhahabu yanang'ara chini ya theluji nyeupe.

    Mkulima Yu Lianjiang mwenye umri wa miaka 80 mwaka huu bado anaonekana mkakamavu na mwenye afya, lakini uso wake unaonesha dhahiri mikunjo ya uzee.

    Jikoni mke wa bwana Yu Lianjiang, Bibi Lin Xiujuan alikuwa anawaongoza wake wa watoto wao watatu kupika chakula. Japokuwa binti yao mmoja na wavulana watatu wote wameanza kujitegemea na kuishi peke yao, lakini siku hiyo wote wamerudi nyumbani kwa wazazi, kwa sababu nguruwe anachinjwa kwa ajili ya kusherehekea mwaka mpya. Ni desturi ya wakazi wa sehemu ya kaskazini mashariki mwa China kuchinja nguruwe wakati wa kusherehekea mwaka mpya wa kijadi. Mzee Yu Lianjiang alisema kuwa, mwaka huu familia yake ilipata mavuno mengi ya mahindi. Hivyo siku hiyo atawaalika jamaa wengi ili kufurahia mavuno ya mwaka huu.

    Ikiwa moja ya sehemu muhimu inayozalisha nafaka nchini China, wakulima wa sehemu ya kaskazini mashariki mwaka huu karibu wote wamepata mavuno mengi. Mzee Yu na mke wake wana hekta moja ya shamba. Alisema:

    "Mwaka huu nimevuna kilo elfu 18 za mahindi. Kama kilo moja ya mahindi inaweza kuuza kwa senti 80, basi nitapata yuan za renminbi elfu 15, nikiondoa gharama, nitabaki yuan za renminbi elfu 10."

    Mzee Yu alisema kuwa, mwaka huu wakulima hawana haja ya kulipa kodi ya kilimo, na tena wanapewa ruzuku, hivyo wakulima wote wana moyo mkubwa wa kulima mashamba.

    "Wakulima wote nchini China wana hisia zinazofanana na za Mzee Yu. Kupanda kwa bei ya nafaka kuanzia mwishoni mwa mwaka 2003 kumewapatia wakulima faida halisi. Katika miezi 9 iliyopita ya mwaka huu, kwa wastani mapato ya wakulima nchini China yameongezeka kwa asilimia 10 kuliko mwaka jana wakati kama huu, hii ni ongezeko kubwa kabisa kwa wakulima tangu mwaka 1997."

    Jambo linalomfurahisha zaidi mzee Yu Lianjiang ni kuwa, mwanzoni mwa mwaka huu, serikali ya China ilitoa sera ya kufuta kodi zote za kilimo katika miaka mitano ijayo na kuondoa kodi ya mazao maalum ya kilimo isipokuwa tumbaku. Mzee Yu alisema, sera hiyo ni nzuri sana, watu wote wazee kwa watoto wana furaha kubwa.

    Kupata faida kubwa kumewahamasisha wakulima kutumia teknolojia mpya ya uzalishaji, na kujifunza jinsi ya kuchagua mbegu, mbolea na zana nyingine za kilimo. Hivi sasa wazo la kulima mashamba kwa njia ya kisayansi linakubalika sana kwa wakulima vijijini.

    Mtoto mdogo wa mzee huyo Bwana Yu Shihai ni mkulima hodari katika kijiji chake, yeye ana nadharia pekee kuhusu jinsi ya kulima shamba vizuri na kujipatia mavuno mazuri. Alisema kuwa, kulima shamba kunatakiwa kuchagua mbegu bora na mbolea mwafaka, hekta moja ya shamba inaweza kuzalisha kilo zaidi ya elfu 10 za nafaka na kupata mapato ya yuan za renminbi elfu nane, ukipanda nusu hekta ya mboga pia unaweza kupata mapato yanayolingana na hayo, lakini kunahitaji kazi nyingi zaidi.

    Hivi sasa kwa wastani mapato ya wakulima wa kijiji chao ni yuan za renminbi zaidi ya 4000, wakulima wote wanaishi katika nyumba za matofali na vigae, karibu barabara zote zimetandikwa saruji. Asilimia 80 ya familia za kijiji hicho zina matrekta yenye magurudumu manne, maji ya bomba yameingia katika kila familia, pamoja na simu na TV ya kebo. Nyumbani kwa mzee Yu, vitabu kuhusu mambo ya kilimo vimejaa kwenye safu mbili za vitabu, uani pikipiki mpya imeegeshwa kwenye ukuta. Kama walivyo wakulima wengine, mzee Yu anakwenda shambani kwa pikipiki.

    Wakati wa baridi, jua linazama mapema katika sehemu ya kaskazini mashariki mwa China. Baada ya kuwasindikiza jamaa, giza tayari lilikuwa limetanda, na mzee Yu na familia yake walirudi nyumbani na kukaa pamoja wakitazama TV na kusikiliza wimbo wa kienyeji, huo ni wakati wa kustarehe kabisa kwa mzee Yu. Kabla ya kwenda kulala, mzee Yu anazunguka tena uani, akitazama mahindi yanayolundikwa uani huku akitabasamu kwa furaha na kufikiria kuhusu mpango wa kilimo wa mwakani.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-23