Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-31 16:53:26    
Gwiji wa Opera ya Kibeijing Mei Langfang

cri

    Bw. Mei Lanfang ni gwiji wa opera ya Kibeijing. Asili yake ni Taizhou, Jimbo la Jiangsu. Alizaliwa tarehe 22 Oktoba, 1894 katika ukoo wa wachezaji wa opera ya Kibeijing jijini Beijing. Alianza kujifunza uchezaji huo tangu alipokuwa na umri wa miaka 8, na kuanza kutumbuiza jukwaani akiwa na umri wa miaka 11. Alicheza opera ua Kibeijing kwa zadi ya miaka 50 kabla hajaaga dunia mwaka 1961. Mei Lanfang alipewa heshima kubwa na upendo wa dhati kutoka kwa wananchi.

    Marehemu Mei aliheshimu jadi ya uchezaji, alikuwa hodari wa kurithi michezo mizuri na kubadilisha ile isiyofaa; alijifunza kwa bidii na kufanya mazoezi magumu; alipenda kuchukua sifa za opera za aina nyinginezo; alitanguliza kuboresha sanaa ya opera ya Kibeijing; alibadili uimbaji, kuongeza ala za muziki na kuendeleza upambaji; alivumbua uchezaji mpya uitwao "huadan", yaani mtindo mpya wa wachezaji wanawake; alicheza michezo mingi ya kusisimua ambayo iliwaachia watazamaji kumbukumbu ya kudumu. Katika opera ya Kibeijing aliunda madhehebu ya Mei.

    Bw. Mei alikuwa na sauti nyororo, aliimba kwa madaha. Yeye alicheza michezo katika hali ya juu, na uimbaji wake siku baada ya siku ulipevuka na kunawiri, ulikuwa mzito na wa kuvutia. Alitunga michezo mingi ya ngoma za kale zenye madaha; alichanganya opera, uimbaji na ngoma; alifanikisha opera ya Kibeijing. Aliwaacha hoi washabiki wa sanaa hiyo. Kwa hivyo, alitukuzwa nchini China na ng'ambo.

    Marehemu Mei alikuwa wa kwanza kuijulisha opera ya Kibeijing kwa dunia. Aliwahi kutembelea na kutumbuiza nchini Japan mwaka 1919, 1924 na 1956; Marekani 1930 na Urusi 1935 na 1952. Chuo Kikuu cha California ya Kusini na Chuo Kikuu cha Pomona vilimtunukia hadhi ya udaktari wa heshima wa fasihi. Katika matembezi hayo, licha ya kuwajulisha watu wa dunia utamaduni na sanaa ya China, kuingiza opera ya Kibeijing miongoni mwa opera ya dunia, na kutoa taathira kwa opera za aina nyingine, alijenga pia urafiki na wasanii wengi, wanaopera, waandishi wa vitatu, waimbaji, wacheza ngoma na wachoraji waliojulikana sana duniani, kama vile Maxim Gorky, Konstantin Stanislavsky, Charles Chaplin, Paul Robesen, Bertolt Brecht, Rabindranath Tagore na Ennosuke Chikawa. Bw. Mei alichangia sehemu kubwa sana katika maingiliano ya utamaduni kati ya China na mataifa mengi. Madhehebu ya opera za China yakiwakilishwa na Mei Lanfang, madhehebu ya Stanislavsky na madhehebu ya Brecht yanahesabiwa kuwa ni mifumo mitatu muhimu ya sanaa ya maonyesho katika dunia ya sasa.

    Bw. Mei alikuwa ni mzalendo hasa. Mapema kipindi cha "Mei Nne" wakati China ilipolazimishwa kusaini mkataba ambao ulikuwa ni wa kuliaibisha taifa, Mei alikasirika, akatunga na kucheza mchezo wa "Mulan Ajiunga na Jeshi" ili kuwahamasisha wananchi walipende taifa lao. Baada ya Japani kuivamia China, Mei alitunga na kucheza michezo ya "Kupigana na Washambulizi" na "Kisasi cha Kufa na Kupona" ili kuwatia hamasa wananchi wawapinge madui na kuliokoa taifa. Katika muda wa miaka minane ambapo Japani iliitawala China, Mei hakuogopa kutishwa wala hakukubali kuhongwa. Ili kususua kuwatumbuiza maadui na maafisa wa bandia, alifuga ndevu. Baada ya China Mpya kuasisiwa alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wananchi la Taifa, mwanachama wa Ofisi ya Kudumu ya Kamati ya Taifa ya Halmashauri ya Mashauriano ya Siasa ya Wananchi wa China. Aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Opera ya China na Mkuu wa Jumba la Opera ya Kibeijing la China, Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Sanaa na Fasihi la China na Makamu mwenyekiti wa Jumuia ya Wacheza opera na Tamthilia wa China. Bw. Mei alitoa mchango mkubwa kwa ajili ya ujenzi wa ujamaa wa China.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-31