Wizara ya Elimu ya China imezitaka shule ziingize elimu ya kinga na tiba ya Ukimwi katika vipindi vya masomo kuanzia mwaka 2004. Imezitaka shule za sekondari za chini ziwe na vipindi hivyo viwe 6 katika kila muhula na katika sekondari za juu kuwe na 4 katika kila muhula na katika shule za ufundi vipindi hivyo viwe 4 hadi 6, na vyuo vikuu pia lazima viwe na vipindi hivyo au mihadhara maalumu na kwa wastani kisipungue kipindi kimoja.
Hayo yalitolewa katika nyaraka zilizotolewa na Wizara ya Elimu ya China mwaka 2004. Naibu waziri wa elimu Bi. Chen Xiaoya tarehe 29 Novemba mwaka jana alisema kuwa katika miaka ya karibuni kwa kufuata maagizo ya Kamati Kuu ya Chama na Baraza la Serikali ya China, wizara ya elimu ilitoa nyaraka nyingi mfululizo zikitaka vyuo vikuu, shule za sekondari na shule za ufundi lazima vieneze "maagizo ya kinga na tiba ya Ukimwi" kwa kila mwanafunzi mpya, na hadi mwaka 2005 asilimia 100 ya wanafunzi lazima wawe na maagizo hayo mikononi. Kabla ya mwisho wa mwaka 2005 walimu wote lazima wawe wameshiriki semina kuhusu elimu ya kinga na tiba ya Ukimwi, na katika maktaba za shule zote lazima kuwe na vitabu vya sayansi kwa umma kuhusu kinga ya Ukimwi, kuepuka dawa za kulevya, na ujuzi wa kujitolea damu. Hadi kufikia mwaka 2005 asilimia zaidi ya 80 ya shule lazima ziwe na vitabu hivyo kwenye maktaba zake. Na kwenye matangazo ya shuleni lazima kuwe na sehemu maalum za kueneza elimu ya kinga na tiba ya Ukimwi katika zaidi ya asilimia 70 shule nchini China.
Naibu waziri wa elimu alieleza kuwa Wizara ya Elimu imeweka mada maalumu ya mafunzo ya kinga na tiba ya Ukimwi. Nyaraka zilizotolewa na wizara hiyo za "matakwa ya kimsingi kuhusu mafunzo ya kinga na tiba ya Ukimwi" na "Programu ya elimu ya kinga na tiba ya Ukimwi kwa wanafunzi wa sekondari" zinataka shule kuwaelimisha wanafunzi kuhusu ugonjwa wa Ukimwi ulivyo, njia na hatua za kujikinga na maambukizi, madhara na elimu ya afya kuhusu mambo ya ujana. Lengo la mafunzo hayo katika sekondari ya juu na vyuo vikuu ni kuwa zaidi ya mafunzo ya shule za msingi wanafunzi, waelimishwe zaidi kuhusu Ukimwi na kuwajali wagonjwa na wenye virusi vya Ukimwi. Elimu hiyo katika sekondari ya juu na vyuo vikuu ikiwa ni pamoja na hali ilivyo ya maambukizi ya Ukimwi, hatari na madhara ya Ukimwi kwa jamii na uchumi, na elimu kuhusu uhusiano kati ya matumizi ya dawa za kulevya na Ukimwi, ujuzi kuhusu kujitolea damu, njia na hatua dhidi ya maambukizi ya Ukimwi na matunzi kwa wagonjwa na wenye virusi vya Ukimwi, afya wakati wa ujana na majukumu ya kinga ya Ukimwi na magonjwa ya zinaa, maadili mema, sheria pamoja na sera za China kuhusu kinga na tiba na udhibiti wa Ukimwi.
Idhaa ya kiswahili 2005-01-07
|