Deyang ni mji mpya ulioko kwenye sehemu ya magharibi ya Jimbo la Sichuan. Mji huu ni safi sana na una msingi imara wa viwanda na mandhari nyingi za kiutamadimi. Kati ya mandhari hizo, Ukuta Wenye Sanaa ya Michongo ya Mawe ya Deyang ndio unaowavutia zaidi watalii kwa mtindo wake wa kipekee wa ujenzi na kiwango cha juu cha sanaa.
Deyang ilikuwa makao makuu ya wilaya, mwaka 1983 ulipanuliwa na kuwa manispaa ya jimbo baada ya kupewa kibali na Baraza la Serikali . Kutokana na mahitaji ya ujenzi wa barabara, serikali ya mji iliamua kujaza udongo kwenye ukingo wa mto na kujenga ukuta. Baada ya uchunguzi wa makini, wataalamu wakikubaliana kujenga ukuta wa sanaa ya michongo ya mawe kwa mtindo wa kipkee. Sehemu kuu ya mradi huo ilikamilika kwa muda wa miaka mitatu kuanzia mwaka 1987 hadi 1990. Ukuta huo una urefu wa mita 720 na kimo cha mita 7. Juu ya ukuta kuna barabara safi na sehemu inayozunguka ukuta imepandwa miti na mimea mingi na ikajengwa kuwa "bustani ya michongo".
Ukuta wa sasa una urefu wa mita 1,480. Mpangilio wa maudhui ya aina tatu, yaani historia, sanaa ya kitaifa na maumbile na maisha umeufanya ukuta huo ugawanyike katika sehemu kadha zinazohusiana, lakini kila sehemu ina ujumbe wake kamili. Michongo kwenye ukuta huo ni kielelezo kizuri cha karibu mbinu zote za uchongaji, kama nakshi za kutokeza nje, michongo ya mviringo na michongo ya kutoboa.
Mchongo mkubwa wa kutoboa wa 'Mwanga wa Akili" una urefu wa mita 54 na kimo cha mita 7. Mchongo huu unaundwa kwa mchanganyiko wa nakshi za matofali yenye sura za watu wa Enzi ya Han, michongo ya ngoma za kale, kilimo na uwindaji wa zama za kale na michongo iliyoigiza vinyago vya shaba nyeusi vilivyochimbuliwa huko Guanghan, ambavyo ni chanzo cha Utamaduni wa Sichuan wenye historia ya miaka 5,000 na unaojulikana nchini China na ng'ambo. Ujia mrefu wa sanaa wenye umbo la tao unaundwa na matao 35 na nguzo 37. Kila nguzo imechongwa nakshi ya joka linaloizunguka nguzo hiyo na kila moja ya majoka haya lina umbo tofauti. Katika mlango na madirisha ya kila tao kumechongwa hadithi moja ya zama za kale ya China. Wakati mtalii anapotembea kwenye ujia huo, hujihisi kama amezama katika mto mrefu wa histora na hupata mawazo mengi?
Mchongo mkubwa wa "Wimbo wa Maisha" una urefu wa mita 38 na kimo cha mita 7; unaundwa kwa mpangilio wa "Majita Manne", "Farasi Anayeruka Akivuka Poromoko la Maji" na "Binadamu na Maumbile", na unaonyesha matumainio ya binadamu kwa maumbile na maisha.
"Nguzo za Nyota 12 za Binadamu" ni michongo ya sura za vichwa vya wanyama wa aina 12 ambao ndio nyota za binadamu kwenye nguzo. Michongo hiyo inawapa watalii hisia ya uhusiano wa karibu uliopo kati ya binadamu na wanyama.
Mchongo wa " Roho ya China" unaochongwa sasa, utakuwa na urefu wa mita 380 na utaundwa na michongo ya mawe ya sura za watu zaidi ya 1,000 ambao ni pamoja na waanzilishi wa historia ya China kama Pan Gu na watu wa makabila 56 ya China wa sasa. Baada ya kukamilika, ukuta huo wa sanaa utakuwa na urefu wa kilomita 2, na hautaonyesha tu ushupavu na uhodari wa watu wa Deyang, bali kitu muhimu zaidi ni kwamba utakuwa ni mchanganyiko mzuri wa kipekee wa ujenzi wa mji na sanaa ya uchongaji nchini China.
Idhaa ya Kiswahili 2005-01-07
|