Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-10 14:35:56    
Kwenda Hangzhou kuonja chai ya Longjing

cri
Watu wengi wa mkoa wa Zhejiang wanapenda sana kunywa chai ya kijani. Wanaona kuwa baada ya kufanya kazi kwa siku moja, wakinywa chai ya kijani, mioyo inatulia na uchovu unatoweka. Na ukinywa chai, harufu nzuri ya chai ya kijani inabaki mdomoni kwa muda mrefu, hii inaburudisha sana. Na chai ya kijani inayopendwa na watu wengi wa mkoa wa Zhejiang ni chai ya Longjing inayosifiwa kuwa ni "chipukizi la dhahabu", "chai nzuri isiyo na mpinzani".

Chai ya Longjing imekuwa na historia ya zaidi ya miaka 1200, ilianza kuzalishwa katika kijiji cha Longjing, kusini magharibi ya Ziwa Xihu la Hangzhou. Kijiji cha Longjing kiko katika sehemu ya milima Shifeng ambapo hali ya hewa ya huko ni ya fufutende, mvua ni ya kutosha, mazingira mazuri ya kimaumbile yanaifanya chai ya Longjing iote vizuri kwenye milima Shifeng.

Mtaalamu wa chai wa mji wa Hangzhou Bwana Hu Xinguang alipofahamisha historia ya chai ya Longjing ya Ziwa Xihu alisema:

Chai ya Longjing ya Ziwa Xihu ilianzia Enzi ya Tang, ilizalishwa zaidi kuanzia Enzi ya Son na ikajulikana kuanzia Enzi ya Ming, na hadi Enzi ya Qing, chai ya Longjing ikawa maarufu sana nchini na ng'ambo.

Inasemekana kuwa, wakati wa enzi ya Son, katika kijiji kidogo cha Longjing aliishi bibi kizee mmoja ambaye hakuwa na jamaa. Maisha yake yalikuwa yakitegemea miti 18 ya chai aliyoipanda. Mwaka mmoja ubora wa chai ya miti hiyo ulikuwa sio mzuri, hivyo chai ya bibi kizee huyo haikuweza kununuliwa, Bibi kizee huyo alikuwa karibu kukaa na njaa. Siku moja mzee mmoja aliingia nyumbani kwake, akaona kinu kimoja cha mawe, alimwambia bibi kizee huyo kuwa alitaka kununua kinu hicho. Bibi kizee alifurahi sana kwani mzee huyo alimlipa pesa nyingi aliponunua kinu hicho, hivyo akasafisha mavumbi na majani yaliyooza yaliyolundikana kwenye kinu hicho, akayafukia chini ya miti yake ya chai. Baadaye mzee huyo na wenzake walikuja kuchukua kinu cha mawe, akagundua kuwa kinu hicho kilisafishwa, alikasirika sana, akamwambia bibi kizee kuwa alichotaka kununua ni takataka alizosafisha. Bibi kizee alisikitika sana kwani hakupata pesa. Lakini baada ye siku chache, mwujiza ukatokea, miti 18 ya chai aliyoipanda ikatoa chipukizi mpya, chipukizi hizo zilikuwa chai nzuri yenye harufu ya kupendeza. Habari hiyo ilienea pote kando la Ziwa Xihu, wanavijiji wengi walikuja kununua mbegu za chai. Siku baada ya siku, chai ya Longjing ikapandwa kwenye sehemu ya kando la Ziwa Xihu, na chai ya Longjing ya Xihu ikajulikana.

Hivi sasa kuna vijiji 13 vilivyoko karibu na Ziwa Xihu vinavyozalisha chai ya Longjing, kila kijiji kina kiwanda chake cha kutengeneza chai, uzalishaji wa chai unafikia tani 1000 kwa mwaka.

Watu wa mkoa wa Zhejiang wana hisia kubwa kwa Chai ya Longjing, wanasema bora kukosa chakula kwa siku moja kuliko kukosa chai. Mikahawa ya chai imetapakaa kote mkoani humo. Bwana Hu Xinguang anasema:

Baada ya kufanya juhudi za miaka mingi, watu wa vizazi hadi vizazi wakaifanya chai ya Longjing ijulikane nchini na ng'ambo.

Haya basi wasikilizaji wapendwa, mkipata nafasi ya kwenda mkoa wa Zhejiang kufanya utalii msisahau kwenda kando la Ziwa Xihu kuonja chai ya Longjing yenye ladha nzuri.

Idhaa ya kiswahili 2005-01-10