Muda si mrefu uliopita, kutokana na filamu ya "Shrek 2" kurudufiwa na kuwa sahani za video na kuuzwa madukani nchini China, Studio ya kutengeneza filamu hiyo nchini Marekani iliilalamikia China. Baada ya kupata malalamiko hayo Idara ya Kulinda Hakimiliki ya China mara moja ilichukua hatua ya kusaka sahani hizo katika miji ya Beijing, Shanghai na Guangzhou, licha ya kuzoa sahani hizo iliyatoza faini maduka 50 husika. Studio ya filamu hiyo ya Marekani iliridhika na jinsi China ilivyopambana na uharamu huo wa kurudufu filamu hiyo kuwa sahani za video.
Ofisa wa Idara ya Kulinda Hakimiliki ya China Bw. Wang Ziqiang alisema, harakati hiyo imedhihirisha wazi msimamo wa serikali ya China kupambana kidete na ukiukaji wa hakimiliki. Alisema, "Serikali ya China inaichukulia suala la kulinda hakimiliki kama ni kazi muhimu katika shughuli za kuweka soko katika hali nzuri. Licha ya kuwa serikali inajitahidi kupambana na mauzo ya sahani haramu za video, pia inajitahidi kugundua na kuondoa kabisa vituo vya kurudufu sahani za video."
"Kulinda hakimiliki na kupambana na ukiukaji wa hakimiliki" ni kazi muhimu katika jitihada za kuliweko soko katika hali nzuri na kuimarisha utaratibu wa uchumi nchini China, na kazi hiyo haijawahi kulega lega katika mwaka 2004.
Katika miaka ya karibuni, kutokana na maendeleo ya mtandao wa internet, wizi wa haki ya kunakili pia umeshamiri, namna ya kulinda haki ya kunakili limekuwa tatizo la kimataifa. Imefahamika kuwa katika mwaka 2005 China itatunga sheria ya kulinda haki ya kunakili katika mtandao wa internet. Hivi sasa Wizara ya Upashanaji Habari ya China imetunga mswada wa Sheria hiyo na kukusanya maoni ya umma.
Taasisi ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Beijing, Prof. Zhang Ping alisema kuwa sheria hiyo ni ya lazima katika kukabiliana na changamoto ya teknolojia mpya. Alisema, "Kutokana na hali mbaya ya wizi wa haki ya kunakili katika mtandao wa internet, sheria hiyo ni ya lazima ili kutawala mtandao, lakini mpaka sasa hakuna uzoefu uliokomaa duniani dhidi ya hali hiyo, kwa sababu hili ni jambo jipya kabisa."
Mwaka huu China ilijitahidi kushirikiana na nchi nyingine katika juhudi za kulinda hakimiliki. Tokea mwanzoni mwa mwaka huu Idara ya Kulinda Hakimiliki ya China ilituma ujumbe mara nne kwenye nchi za Umoja wa Ulaya, na Umoja huo pia ulileta ujumbe mara tano nchini China kutoa mafunzo na maelekezo. Na pande mbili zilijadiliana kwa kina namna ya kutunga na kutekeleza sheria, na kutoa mwamko kwa umma ili uwe na mwamko wa kulinda hakimiliki. Mkurugenzi wa Idara ya Hakimiliki ya Idara Kuu ya Biashara ya Umoja wa Ulaya Bw. Paul Vandorean alisema, "Kwa sababu China imetambua uzito wa suala hilo katika maendeleo ya uchumi wa China, mabadiliko makubwa yametokea katika hali ya kulinda hakimiliki nchini. Tutaendelea kushirikiana na idara za China kuendeleza juhudi hizo ili zifanikiwe zaidi."
Mwaka huu serikali ya China ilifanya shughuli za aina nyingi kwa lengo la kueneza mapambano dhidi ya vitendo vya kurudufu sahani za video. Tamasha la Muziki la Asia lililofanyika mwezi Oktoba mjini Shanghai lilifungwa kwa kwaya kubwa za zilizoimba nyimbo zikiwa na mada ya "Wizi wa Hakimiliki Ukomeshwe". Mmoja wa waandaliaji wa tamasha hilo Bw. Lu Guoping alisema, "Katika soko la muziki, pia kuna tatizo la wizi wa hakimiliki, lengo la tamasha hilo ni kulinda hakimiliki ili kustawisha soko la muziki."
Kutokana na juhudi kubwa za serikali na jumuiya mbalimbali za jamii sasa wizi wa hakimiliki unachukiwa katika jamii. Bibi mmoja aliwaambia waandishi wa habari akisema, "Hivi sasa wauza sahani za kurudifiwa wamepungua sana. Nasikia furaha kuangalia filamu katika jumba la sinema kuliko kukaa nyumbani kuangalia sahani ya kurudifiwa nikiwa kama wizi."
Mafanikio yaliyopatikana katika juhudi za kupambana na wizi wa hakimiliki yanaonekana wazi. Mshauri mwandamizi wa Shirikisho la Filamu la Marekani nchini China Bw. Wang Yong alipozungumzia jitihada za China katika mapambano hayo alisema, "Kwa kweli mafanikio ni makubwa na yanastahili kusifiwa, lakini ukweli ni kwamba China ni nchi kubwa, safari ya kuliweka safi soko lake bado ni ndefu."
Aliendelea kusema kuwa hakimiliki haiwezi kulindwa kabisa mpaka wananchi wote watambaue wazi kuwa ni kazi ya uvumbuzi tu ndiyo inayoweza kuleta maendeleo ya jamii. Nchi kama China yenye watu zaidi ya bilioni moja ina safari ndefu kufikia kwenye lengo hilo.
Ni kama Bw. Wang Yong alivyosema kuwa kujenga mfumo ulio kamili wa kulinda kabisa hakimiliki sio kazi ya usiku mmoja tu, hata hivyo serikali ya China haitachoka kufanya juhudi. Imefahamika kuwa mwaka kesho utaendelea kuwa ni mwaka wa kampeni dhidi ya wizi wa hakimiliki, na mpango wa kampeni hiyo tayari umeandaliwa na Idara ya Kulinda Hakimiliki.
Idhaa ya kiswahili 2005-01-10
|