Hapa duniani baadhi ya waimbaji wanaimba kwa ajili ya kuishi, na baadhi wanaishi kwa ajili ya kuimba. Mwimbaji Hazhabu mwenye umri wa miaka 83 ni mwimbaji wa aina ya pili.
Hazhabu alizaliwa katika Mkoa wa Mongolia ya Ndani, mkoa ulioko kaskazini mwa China. Jina lale alilopewa na baba yake lina maana ya "majaaliwa" kwa lugha ya kikabila, kutokana na jina hilo imeonesha wazi jinsi wazazi wake walivyompenda.
Mzee Hazhabu ingawa ana umri wa miaka 83, lakini akili yake ni timamu, na lugha yake ni fasaha. Tokea alipokuwa mtoto alianza kusikiliza na kujifunza kuimba kutoka kwa baba yake ambaye alimpakata mgongoni mwa farasi alipokuwa akichunga farasi kwenye mbuga za majani. Mzee Hazhabu alisema, "Wazazi wangu baba na mama wote walikuwa waimbaji hodari, mimi ni mtoto wao pekee. Kutokana na taathira zao napenda kuimba toka utotoni mwangu, na nilipokuwa na umri wa miaka saba hivi nilianza kuimba pamoja na wazazi wangu. Kila walipopiga kinanda mimi nilikuwa naimba nao. Nilipokuwa na miaka 18 hivi tayari nilikuwa na uwezo wa kuimba nyimbo nyingi za kikabila na nilikuwa na umaarufu kidogo miongoni mwa wenyeji wenzetu."
Baadaye Hazhabu alijifunza uimbaji wa nyimbo za kabila la Wamongolia kutoka kwa mwimbaji mashuhuri wa kabila lao, na uimbaji wake wa mtindo wa kikabila ulikomaa.
Hazhabu alijipatia umaarufu kwa nyimbo zake, aliwahi kupata tuzo ya farasi wawili kutokana na uimbaji hodari. Tuzo hii ni kubwa na ilikuwa mara ya kwanza kutolewa katika sikukuu ya kabila la Wamongolia na tokea hapo jina lake lilianza kuvuma sana katika Mkoa wa Mongolia ya Ndani.
Amini usiamini lakini ukweli wa mambo yanayostaajabisha ni kuwa, nyimbo zake sio tu zilimpatia umaarufu bali pia zilimsaidia kukwepa janga la kuuawa alipokuwa mikononi mwa majambazi. Jambo lilitokea alipokuwa na umri wa miaka 24, siku moja alikamatwa na majambazi na kutaka kumwua. Kabla ya kumwua majambazi walimwuliza kama ana usia wowote. Usia wake ulikuwa ni "Niruhusu niimbe wimbo mmoja."
Wimbo aliouimba ulikuwa wa jadi, ukimfananisha farasi na mbuga za majani. Baada ya wimbo huo majambazi hawakumwua, kisha akaimba wimbo wa pili, wa tatu.... Majambazi walitokwa na machozi kwa kuguswa na nyimbo zake zilizowasisimua. Mmoja wa majambazi alishusha pumzi akisema "Mwache, mwachie aendelee kuimba nyimbo zake katika mbuga zetu."
Mwaka 1953 Hazhabu alijiunga na Kundi la Nyimbo na Ngoma la Mkoa wa Mongolia ya Ndani, aliianza kuimba nyimbo zake katika jukwaa badala ya kwenye mbuga za majani. Tokea hapo alianza kuimba huku na huko nchini China na hata katika nchi nyingine. Alipoimba nchini Jamhuri ya Mongolia, aliwahi kutoa shukrani mara 11 kwa makofi ya watazamaji. Alipoimba nyimbo zake katika nchi za Uswisi na Denmark watazamaji walimshangilia na kupanda jukwaani kumzawadia kwa zawadi za aina mbalimbali. Hazhabu alisema kuwa duniani kuna lugha moja tu ambayo haina haja kutafsiriwa, nayo ni muziki. Alisema, "Natilia maanani sana kila nilipoimba nyimbo zangu, na kila nilipomaliza kuimba watazamaji walipanda jukwaani kunikumbatia nilipoimba nchini Japan, Urusi, Uswisi na nchi nyingine."
Kutokana na maisha ya kuimba zaidi ya miongo kadhaa, Hazhabu amekuwa mwakilishi wa mtindo maalumu katika uimbaji wa nyimbo za kabila la Wamongolia. Mwaka 1989 serikali ya Mkoa wa Mongolia ya Ndani ilimpa sifa ya "Mfalme wa Nyimbo za Kabila la Wamongolia", hii ni mara ya kwanza kwa mwimbaji wa kienyeji kupata sifa kama hiyo mkoani.
Bw. Hazhabu aliimba huku na huko katika miji na vijiji vya China, lakini mwishowe aliamua kupiga maskani kwenye mbuga ya majani. Mwaka 1987 alistaafu kutoka Kundi la Nyimbo na Ngoma la Mkoa wa Mongolia ya Ndani na kuishi kwenye maskani yake, alifahamu kwamba huko ndiko alikoota mzizi wa maisha yake, huko alianza kuandaa vijana. Waimbaji wengi mashuhuri nchini China walikuwa wanafunzi wake, alikutumia pesa zake kuanzisha shule ya uimbaji wa nyimbo za kabila la Wamongolia. Hazhabu alitumia moyo wake wote kuwafundisha ili wawe warithi wake. Mzee Hazabu alisema, "Nimepata uimbaji wangu maalum kutokana na mazoea ya miaka mingi, nisipowafundisha vijana usanii wangu utakatika."
Mpaka sasa mara nyingi watu humwona mzee huyo kwenye mlima akituliza mawazo kuangalia mbuga za majani, wanafahamu kuwa mzee Hazhabu anaimba huko.
Idhaa ya kiswahili 2005-01-17
|