Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-18 21:05:29    
China yadumisha ongezeko kubwa katika biashara na nchi za nje

cri

    Katika makazi yajulikanayo kwa jina la Wangjing, yaliyoko kwenye sehemu ya kaskazini mashariki ya Beijing kuna wakazi wengi kutoka Korea ya Kusini wanaofanya kazi hapa nchini China. Hivyo huko kuna maduka mengi ya kikorea. Bw.Hong Chunzhi mwenye umri wa miaka 36, anaendesha kampuni moja ya chakula kinachoagizwa kutoka Korea ya Kusini. Ingawa kampuni hiyo ilianzishwa si muda mrefu uliopita, lakini biashara ya Bw. Hong Chunzhi inapamba moto siku hadi siku.

   "Kampuni yetu ambayo ilianzishwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita, hasa inashughulikia mauzo ya chakula cha Korea ya Kusini, na hivi sasa inaendelea vizuri. Kabla ya hapo niliendesha duka moja dogo lenye eneo la kati ya mita za mraba 30 hadi 40. Hivi sasa kampuni yetu imekuwa na matawi matano, ambayo kodi za majengo yake zinafikia Yuan laki kadhaa kwa mwaka.

   Bw.Hong Chunzhi alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa bei za chakula zinafanana na za chakula kinachouzwa nchini Korea ya Kusini, hivyo wakorea wengi wanaotoka Korea ya Kusini wanapenda sana kununua vitu katika maduka yake. Hivi sasa pia kuna wachina wengi wanaonunua vitu katika maduka yake. Mwaka jana aliagiza makontena 6 ya chakula kutoka Korea ya Kusini, ambacho thamani yake inakaribia Yuan milioni 2.

   Katika miaka ya karibuni idadi ya wachina wanaoshughulikia mauzo ya rejareja ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi za nje imeongezeka kwa mfululizo. Pamoja na maendeleo kasi ya uchumi, kiwango cha ununuzi cha wakazi wa kawaida kinainuka kwa mfululizo, ambapo China inaagiza bidhaa kwa wingi kutoka nchi za nje. Takwimu za wizara ya biashara ya China zinaonesha kuwa, thamani ya bidhaa zilizosafirishwa na China kwa nchi za nje, na bidhaa zilizoagizwa na China kutoka nchi za nje ilikuwa na ongezeko kubwa katika miezi 11 mwaka 2004 na kuzidi dola za kimarekani bilioni 500 zikiwa ni ongezeko la karibu 40% kuliko mwaka uliotangulia katika kipindi kama hiki.

    Mfanyakazi wa idara ya utafiti wa mambo ya fedha, biashara na uchumi ya taasisi ya sayansi ya jamii ya China bibi Zhao Jin ambaye amefanya kazi hiyo ya utafiti kwa miaka mingi kuhusu biashara na uwekezaji duniani, Alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema kuwa, kuna vitu vingi ambavyo vimechangia ongezeko kubwa thamani ya bidhaa zilizoagizwa na China kutoka nchi za nje katika mwaka 2004. Alisema,

    "Ongezeko kubwa la thamani ya bidhaa zinazoagizwa na China kutoka nchi za nje, licha ya kutokana na mahitaji ya wateja, uwekezaji mkubwa nchini pamoja na kuathiriwa na uwekezaji wa nchi za kigeni nchini China, kwa upande mwingine inatokana na sera za ufunguaji mlango za China. Baada ya kujiunga na shirika la WTO, mazingira ya biashara ya China yameboreshwa zaidi, ambapo kiwango cha ushuru kinaendelea kupungua na vikwazo husika vya biashara vimeondolewa hatua kwa hatua.

    Bibi Zhao Jin alipofanya uchambuzi alisema kuwa pamoja na kuinuka kwa kiwango cha maisha ya watu wa China, bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi za nje, hususan bidhaa za teknolojia ya mawasiliano zinauzwa kwa haraka sana katika masoko ya China; ongezeko la kasi la uwekezaji wa mali zisizohamishika nchini pia limehimiza ongezeko la uagizaji wa nishati, mali ghafi na mitambo kutoka nchi za nje. Mbali na hayo, upanuaji wa uwekezaji wa makampuni ya kimataifa nchini China pia umesukuma kuongezeka kwa haraka kwa bidhaa zinazoagizwa na China kutoka nchi za nje. Viwanda vilivyojengwa kutokana na uwekezaji wa makampuni ya kimataifa nchini China hususan ni viwanda vinavyoajiri wafanyakazi wengi, vinafanya kazi za usindikaji au uzalishaji kwa kutumia mali ghafi, na zana za kazi na vipuri muhimu vilivyoagizwa kutoka nchi za nje. Bidhaa zinazozalishwa na viwanda hivyo licha ya kuuzwa hapa nchini, kuna sehemu nyingine kubwa inayosafirishwa kwenda nje. Wataalam wanaona kuwa pamoja na kuongezeka kwa mitaji ya kigeni iliyovutiwa kuja nchini China, nguvu ya uhimizaji ya makampuni ya kigeni kwa ongezeko la bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi za nje, pia inakuwa kubwa siku hadi siku.

    Kiasi cha 50% ya bidhaa mbalimbali zilizoagizwa na China kutoka nchi za nje mwaka 2004 zilikuwa ni mitambo na bidhaa za elektroniki. Naibu kiongozi wa jumuiya ya uuzaji na uagizaji wa bidhaa za mitambo na elektroniki kutoka nchi za nje bibi Yao Wenping alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, katika miaka ya karibuni uagizaji wa bidhaa za mitambo na elektroniki kutoka nchi za nje ulidumisha ongezeko kubwa. Katika miezi kumi ya mwaka 2004, jumla ya thamani ya mitambo na bidhaa za elektroniki zilizoagizwa na China kutoka nje ilizidi dola za kimarekani bilioni 270 ikiwa ni ongezeko la 36% kuliko mwaka 2003 katika kipindi kama hiki. Bibi Yao alisema kuwa mitambo na bidhaa za elektroniki zimechukua nafasi kubwa zaidi katika biashara ya China na nchi za nje, hivi sasa usafirishaji na uagizaji wa mitambo na bidhaa za elektroniki umeingia katika hali ya kuchangiana. Alisema,

    Bidhaa zilizosafirishwa nje na China katika miaka mitano iliyopita zilikuwa ni mitambo, elektroniki, vyombo vya kazi na vipuri. Lakini bidhaa zinazosafirishwa na China kwa nchi za nje ni bidhaa kubwa kubwa za seti nzima pamoja na za teknolojia ya kiwango cha kisasa. Bidhaa hizo za teknolojia ya kiwango cha juu zinazosafirishwa kwa nje, zilizalishwa kwa kutumia kiasi cha 50% ya vipuri vilivyoagizwa kutoka nchi za nje. Usafirishaji bidhaa kwa nje umechangia ongezeko la bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi za nje. Usafirishaji bidhaa wa China kwa nje usingeweza kufikia kiwango hicho bila bidhaa nyingi zilizoagizwa na China kutoka nchi za nje. Mashirika maarufu duniani yamethabitisha kuwa China imekuwa nguvu inayohimiza ongezeko la uchumi duniani, hususan kwa uchumi wa Asia ya mashariki, na kufufuka kwa uchumi wa Japan kulitegemea sana ongezeko la bidhaa zilizosafirishwa kwa China.

    Bibi Zhao anaona kuwa mahitaji ya wanunuzi na uwekezaji yataendelea kuwa makubwa. China inatekeleza ahadi ilizotoa wakati ilipojiunga na WTO, imepunguza ushuru wa forodha kwa mara nyingine tena mwanzoni mwa mwaka 2004, na imehimiza ongezeko kubwa la bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi za nje.

Idhaa ya Kiswahili 2005-01-18