Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-19 20:30:43    
kulinda uhai na kuzuia vitendo vya kujiua

cri

    kila mtu wakati fulani anaweza kuwa na wasiwasi, uchungu na hali ya kutojua la kufanya, baadhi yao wanakabiliana na hali hiyo kwa moyo wa ushupavu, na wengine wanachagua kujiua bila ya kufanya juhudi yoyote kukabiliana na hali hiyo. Hivi sasa nchini China, vitendo vya kujiua vikiwa ni moja ya masuala makubwa ya jamii na afya ya umma, vimeanza kufuatiliwa. Ili kupunguza vitendo hivyo, idara nyingi husika za China zimeanzisha hatua kwa hatua shughuli za kutoa misaada ya kisaikolojia ili kuwasaidia watu waliokumbwa na janga kujitoa kutoka kwenye hali hiyo.

    Mshauri wa Shirika la afya duniani Profesa Fei Li Peng anaona kuwa, wengi wa watu wenye nia ya kujiua wana migongano rohoni, wanachotaka ni kumaliza kabisa uchungu moyoni, wala si maisha yao. Hivyo, kama kunakuwepo msaada wa kisaikolojia, watu hao watakuwa na matumaini ya kuendelea kuishi. Alisema,

    Hivi sasa kuna watu wengi wenye tatizo la kisaikolojia, na kuna uwezekano mkubwa kwa watu hao kufanya vitendo vya kujiua, lakini hawajui namna ya kupata matibabu ya kisaikolojia, au wanaogopa gharama za matibabu hayo na kuchukuliwa kama ni wagonjwa wa kiroho. Kwa watu hao, kama kuna simu maalum ya kutoa misaada ya kisaikolojia bure bila haja ya kutaja jina lao, itaweza kusaidia kutatua suala hilo.

    Misaada ya kisaikolojia inayozungumzwa na Profesa Fei ni huduma moja ya afya ya kisaikolojia kwa njia ya ushauri kwa simu, matibabu ya uso kwa uso na kutoa mafunzo kuhusu afya ya kisaikolojia, na hasa kutumia dawa wakati wa lazima, ili kuwasaidia watu wenye tatizo kama hilo kurejea kwenye uwiano wa kisaikolojia, na kuondoa nia ya kujiua. Kutokana na takwimu, baadhi ya nchi na sehemu duniani zimefanikiwa kuzuia asilimia 90 ya vitendo vya kujiua kupitia misaada ya kisaikolojia.

    Katika miaka ya karibuni, wakati suala la vitendo vya kujiua linapofuatiliwa zaidi nchini China, shughuli za kutoa misaada ya kisaikolojia zimeendelea hatua kwa hatua.

    "hallo, hii ni simu maalum ya kutoa misaada ya kisaikolojia. Tunashughulikia vitendo vya kujiua na tatizo la kuwa na huzuni."

    Wasikilizaji wapendwa, hivi sasa mlikuwa mnasikiliza simu maalum ya kwanza ya China ya kutoa misaada ya kisaikolojia------simu maalum ya Beijing ya kutoa misaada ya kisaikolojia. Simu hiyo ilianzishwa katika kituo cha hali hatari ya kisaikolojia na misaada ya kisaikolojia cha Beijing, na Bw. Cao Lian yuan ni mkurugenzi wa kituo hicho. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, simu maalum ikiwa ni njia muhimu ya kutoa misaada ya kisaikolojia, itaweza kutoa huduma ya kitaalamu kwa watu wanaopiga simu.

    "simu hiyo maalum inahudumiwa na wataalamu wa afya ya kisaikolojia, wakiwa ni pamoja na madaktari wa idara ya magonjwa ya kisaikolojia, watumishi wa kijamii na wataalamu wa saikolojia, na walipewa mafunzo maalum kabla ya kutoa huduma kupitia simu hiyo."

    Bw. Cao Lian yuan alisema kuwa, tangu simu hiyo ianzishwe mwezi Desemba mwaka 2002, imepokea simu zaidi ya laki 1.1. na zaidi ya asilimia 80 ya wapiga simu baada ya kupewa misaada ya kisaikolojia, hali hiyo ya wasiwasi na kuona huzuni imepungua na wanarejea katika matumaini ya kuendelea kuishi.

    Bi. Wang Ya xin ni mtaalamu mwenye uzoefu wa kutoa misaada ya kisaikolojia katika kituo hicho, alisema kuwa, uchunguzi husika unaonesha kuwa, watu wengi waliojiua walichukua uamuzi huo kikali kutokana na kutokuwa na watu wanaotaka kusikiliza matatizo yao kuhusu huzuni zao. Hivyo, kuwasikiliza ni jukumu la kwanza la watumishi wanaotoa misaada ya kisaikolojia. Alisema:

    "baadhi ya watu wanapopiga simu hiyo, wana moyo wa kupapatika. Wakati huohuo, tutawaambia kuwa tunawasubiri na kuwasikiliza. Hivyo hisia mbaya za wapiga simu zinatulizwa, na uwezekano wao wa kujiua pia utapunguzwa kwa kiasi kikubwa. Baada ya hisia zao kuwa tulivu, tunajadiliana nao kuhusu sababu zao za kuishi ili kuwapatia uti wa mgongo wa kiroho."

    Hivi sasa, mbali na Beijing, idara maalum za kutoa misaada ya kisaikolojia zimeanzishwa katika miji zaidi ya 10 ya China, ikiwa ni pamoja na Nanjing na Changsha. Idara hizo si kama tu zinaendesha simu maalum ya misaada ya kisaikolojia na kutoa matibabu ya kisaikolojia, bali pia zinatoa misaada ya kisakolojia kwa watu walionusurika baada ya kujaribu kujiua na kuwasaidia watu waliokumbwa na maafa. Aidha, idara hizo zitatoa mafunzo maalum ya kutoa misaada hiyo kwa madaktari, polisi na walimu. Wataalamu pia wanaeneza ujuzi kuhusu afya ya kisaikolojia kwenye makazi na shule na kutoa misaada ya kisaikolojia ya papo hapo.

    Wakati ufahamu kuhusu afya ya kisaikolojia unapoenezwa nchini China, mbali na watu wenye nia ya kujiua, watu wengi zaidi watakwenda katika idara hizo kutatua matatizo yao ya kisaikolojia.

    Wasikilizaji wapendwa, maelezo kuhusu shughuli za kutoa misaada ya kisakolojia nchini China yanaishia hapa kwa leo, asanteni kwa kutusikiliza, kwa herini!

Idhaa ya Kiswahili 2005-01-20