Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-31 17:17:32    
Maonesho ya Michezo ya Sanaa ya "Radio Aid"

cri

Tsunami iliyotokea ghafla ilisababisha maafa makubwa katika nchi za pwani ya Bahari ya Hindi. Kutokana na maafa hayo, nchi nyingi zilinyoosha mikono yao kuzisaidia nchi hizo. Kadhalika, wasanii nchini China hawakuwa nyuma katika harakati hizo za kuonesha moyo wa upendo, siku chache zilizopita walijitolea kwa michezo yao ili kuchangisha fedha za msaada.

Watazamaji walijaa ukumbini, licha ya kuwa walikata tikiti kwa kulipa kiingilio pia wengi wao walikuwa foleni kutolea mchango.

Maonesho hayo yalihudhuriwa na waimbaji wengi hodari na bendi 11. Wasanii hao waliposikia habari ya maonesho ya kuchangisha fedha kwa ajili ya waathirika na maafa mara walijiandikisha kuhudhuria kwenye maonesho hayo. Ufuatao ni wimbo "Fei Fei Rum"wa bendi ya Muma.


Bendi yetu inaitwa kwa jina langu Muma na mimi ni mwimbaji mkuu wa bendi hiyo. Naona maonesho hayo ya ufadhili ni muhimu sana, siwezi kuacha kuhudhuria."


Maonesho hayo ya "Radio Aid" yaliandaliwa na Redio China Kimataifa na Shirikisho la Hisani la China kwa pamoja. Redio China Kimataifa ni kituo cha redio kinachotangazia duniani kwa lugha 43. Lengo la kufanya maonesho hayo ni kuhamasisha watu wa fani mbalimbali kuonesha moyo wa upendo kwa kuwasaidia kifedha waathirika wa nchi za pwani ya bahari ya Hindi. Naibu mhariri mkuu wa Redio China Kimataifa Bw. Ding Bangying alisema, maafa ya watu wa nchi za Asia ya Mashariki na ya Kusini yamewatia sana wasiwasi wafanyakazi wote wa kitu hicho cha redio wakiwemo wataalamu kutoka nchi za nje.


"Baada ya kusikia habari ya maafa ya tsunami wafanyakazi wa kituo cha redio yetu pamoja na wataalamu kutoka ng'ambo mara walijitokeza kuchangia fedha za msaada. Lengo la maonesho ni kwa ajili ya kuwahamasisha watu wa fani mbalimbali washiriki katika harakati hizo za kuonesha moyo wa upendo kwa waathirika."


Mliosikia ni wimbo "Mimi ni wako Romio". 

Bw. Ding bangying

Labda mtauliza, kwa nini maonesho hayo yanaitwa kwa jina la "Radio Aid"? Jina la "Radio Aid" linatokana kutoka maonesho makubwa ya "Live Aid"ya kuchangisha fedha barani Ulaya na Amerika kuwaokoa waliokumbwa na maafa ya njaa wa Ethiopia mwaka 1985. Watazamaji elfu 170 walihudhuria maonesho hayo na fedha nyingi zilipatikana. Katika maonesho ya "Radio Aid" wasanii wote walijitolea bure na fedha zote zitakabidhiwa kwa nchi zilizokumbwa na maafa ya tsunami kwa kupitia Shirikisho la Hisani la China. 

Ufuatao ni wimbo "Furaha Tele". Mwimbaji wa wimbo huo Yie Bei aliharakisha kufika Beijing siku moja kabla ya maonesho kutoka mji wa mbali wa Shanghai na bila kupumzika alishiriki mazoezi ya kabla ya maonesho. Alipoulizwa na waandishi wa habari alishusha pumzi na kusema, 


"Kwa kweli nimechoka sana, na sijisikii vizuri. Lakini maonesho hayo ni muhimu sana, nitajuta nisiposhiriki. Maafa yalitokea ghafla, na mbele ya maafa binadamu ni wanyonge, kitu kinachohitajika ni kuwasaidia."



Alipoona watazamaji walikuwa kwenye foleni kutoa msaada wa fedha, mwimbaji mkuu wa bendi ya Verse Bw. Huang Bo alisisimka,


"Nasikia furaha moyoni, na naona fahari kwa kuwaimbia watu hao, natumai watapitisha jioni hii kwa furaha na natumai kuwa watatoa fedha nyingi kwa ajili ya watu walioathirika na maafa."

Bendi ya Verse inajulikana kwa muziki wake wa kugusa moyo, ufuatao ni wimbo wa bendi hiyo "Spring".


Tsunami ya bahari ya Hindi limewaua watu wengi, na imedhihirisha kuwa mbele ya bahari binadamu ni kama tone, hawawezi kuyazuia maafa yasitokee. Kitu tunachokuwa nacho ni upendo, na upendo huo unatuunganisha pamoja na kuwa na nguvu kubwa ya kuweza kufidia hasara iliyoletwa na maafa ya maumbile. Kabla ya kukamilisha kipindi hiki tusikilize wimbo uitwao "Yungiyungi".


"Hamjambo, mimi ni Longkuan Jiuduan, natumai yeyote anayehitaji msaada atasaidiwa, maafa sio kitu cha kuogopwa, muhimu ni namna ya kupambana nayo."

Idhaa ya kiswahili 2005-01-31