Mkoa wa Hunan ni maskani ya hayati Mao Zedong, wakazi wa mkoa huo wanajulikana sana kwa kula pilipili. Pilipili si kama tu ni chakula muhimu kwa wakazi wa huko, bali pia imeathiri hata tabia zao.
Bwana Liu Liming mwenye umri wa miaka zaidi ya 50 mwaka huu ni mzaliwa wa Hunan, familia yake ina watu watano. Yeye anafanya kazi katika idara ya serikali huko Changsha, mji mkuu wa mkoa wa Hunan, japokuwa anakaribia kustaafu, lakini uso wake bado unanawiri kama kijana, na anaonekana mkakamavu na mwenye ari kubwa. Mke wake ameshastaafu, mtoto wake wa kiume anaendesha kampuni binafsi, mke wa mtoto wake anafanya kazi katika kampuni ya kimataifa, mjukuu wa kike mwenye umri wa miaka minne sasa yuko chekechekea.
Nyumba ya Bwana Liu Liming inaonekana ya maridadi, kila kitu kimewekwa vizuri mahali pake. Kwenye meza ya chakula, vimewekwa viungo vya aina mbalimbali vilivyotengenezwa kwa pilipili. Mtoto wa kiume wa familia hiyo Bwana Liu Jun alisema.
"Sisi hatuwezi kula chakula bila pilipili, tukipika mboga huwa tunaweka pilipili mbichi, na tukitengeneza achali huwa tunaweka pilipili kavu, kila mtu ana desturi za kula pilipili."
Tabia ya kula pilipili zinahusiana na hali ya hewa ya mkoani Hunan. Katika majira ya baridi, hali ya hewa ya mkoa huo ni baridi sana, lakini majira ya joto, hali ya hewa ni ya joto tena ni ya unyevunyevu. Hali hiyo ya hewa si kama tu inafaa kwa kilimo cha pilipili, bali pia imewazoeza watu wa Hunan kupenda kula pilipili. Kwa mujibu wa nadharia ya tiba ya jadi ya kichina, pilipili inaweza kuondoa ubaridi na unyevu, hivyo chakula hicho kimekuwa kitoweo cha lazima kwa wakazi wa Hunan.
Watu wa Hunan wana njia nyingi za kula pilipili, wakazi wa mijini licha ya kula pilipili kavu, pilipili zilizotengenezwa kwa achali, na sosi ya pilipili, pia wanapenda kula pilipili zinazochanganywa kwenye viungo vya sosi ya soya na tangawizi, na pilipili mbichi zinazokatwakatwa na kutiwa chumvi. Sasa katika mikahawa yote ya mapishi ya kihunan kuna kitoweo kiitwacho kichwa cha samaki ambacho kilichochemshwa pamoja na pilipili kinakaribishwa sana na wateja.
Katika vijiji vya Hunan, kila inapofika majira ya kuvuna pilipili, wakulima hupeleka nyumbani pilipili pamoja na mimea yake ili kuhifadhi ladha bora. Ili kuhifadhi vizuri pilipili, wakulima huzifunga pilipili kwa nyuzi na kuzitundika chini ya paa au jikoni, hivyo ukiingia nyumbani kwa wanavijiji wa Hunan katika majira ya mapukutiko na baridi, utaona pilipili nyekundu zimetundikwa, hii imekuwa ni mvuto maalum katika vijiji vya Hunan.
Pilipili si kama tu ni kitoweo kizuri kwa wakazi wa Hunan, bali pia ni dawa nzuri kwao katika kukinga na kutibu magonjwa. Nyumbani kwa Bwana Liu, kama mtu mmoja akipata mafua hana haja ya kwenda hospitali, akila bakuli moja la tambi zenye pilipili na pilipili manga nyingi, basi dalili ya mafua itapungua mara moja.
Umaalum wa watu wa Hunan wa kupenda kula pilipili umetungwa kuwa wimbo unaoimbwa nchini kote. Wimbo huo unaitwa "Wasichana Hodari", ambao unaeleza uhodari na ushupavu wa wasichana wa mkoa wa Hunan wanaopenda kula pilipili.
Wimbo huo unaeleza hivi: wasichana wa Hunan wanaongea sana, wanafanya kazi kwa ushupavu, ni wakarimu kwa wageni ambao wanathubutu kutembea duniani.
Labda ni kweli kutokana na kupenda kula pilipili, wanaume wa Hunan ni wakakamavu na wenye tabia ya kutazamia mema, na wanawake wa Hunan wana tabia ya ushupavu na kuongea bila ya kuzunguka.
Licha ya mkoa wa Hunan, watu wengi katika sehemu nyingine nchini China pia wanapenda kula pilipili, kama vile, watu wa mkoa wa Shangxi, kaskazini magharibi, mkoa wa Sichuan, kusini magharibi, na mkoa wa Jiangxi, kusini mwa China. Lakini watu wa Hunan wanakula pilipili zaidi kuliko watu wa sehemu nyingine. Hivi sasa ni wakati wa baridi, hivyo watu wa Hunan wanakula pilipili nyingi zaidi kuliko siku za kawaida ili kujipatia joto jingi mwilini.
Idhaa ya kiswahili 2005-02-03
|