Katika miaka ya karibuni, pamoja na maendeleo ya kasi ya uchumi wa China na kuinuka kwa heshima China duniani, wanafunzi wengi zaidi wanakuja China kuendelea na masomo yao. Chuo kikuu cha Beijing kikiwa ni chuo maarufu nchini China, kinawapokea wanafunzi wengi zaidi kutoka nchi za nje kuliko vyuo vingine vikuu vya China. Lakini kwa nini wanafunzi hao wanachagua chuo hicho kuendelea na masomo yao, na wanaonaje kuhusu maisha yao kwenye chuo hicho? Katika kipindi hiki cha leo, tutaeleza kidogo kuhusu hali hiyo kutokana na maoni ya baadhi ya wanafunzi wa nchi za nje wanaosoma kwenye chuo hicho.
Mwanafunzi wa kwanza mwenye umri wa miaka 21 kutoka Korea ya Kusini, anaitwa Ki Joon Kwon na kuwa na umri wa miaka 21. hivi sasa ni mwanafunzi wa mwaka 3 anasomea shahada ya kwanza katika taasisi ya uchumi na usimamizi ya chuo hicho, na anaweza kuzungumza kwa kichina sanifu. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, hivi karibuni amepata shahada ya ngazi ya pili ya mtihani wa kiwango cha lugha ya Kichina kwa wageni ulioandaliwa na idara ya kiserikali ya China, na hakuna wanafunzi wengi wanaoweza kupata shahada ya ngazi hiyo.
Bw. Ki Joon Kwon akizungumzia sababu zake za kuja China kuendelea na masomo, alisema kuwa,
"China ni nchi muhimu kwa Korea ya Kusini. Kuja China kusoma kunaweza kunipatia nafasi ya kufanya urafiki na wanafunzi wengi wa China wenye mustakbali mzuri, na hiyo itasaidia maendeleo yangu binafsi katika siku za baadaye."
Bw. Ki Joon Kwon anaona kuwa kuja China kusoma katika chuo kikuu cha Beijing ni moja ya uamuzi wake wa busara. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, makampuni makubwa ya Korea ya Kusini, yakiwa ni pamoja na idara kubwa za fedha, yanahitaji sana watu wenye uzoefu wa kuelewa hali ya soko la China. wanafunzi wa nchi hiyo wakiwa wamehitimu kutoka chuo kikuu maarufu cha China, watapata malipo mazuri zaidi kuliko wahitimu wa chuo kikuu cha Seoul, ambacho ni chuo kikuu kizuri zaidi kuliko vyuo vingine nchini humo. Aidha, serikali ya Korea ya Kusini pia inawazingatia sana watu wanaofahamu kichina na kuwaandalia mazingira mazuri ya kazi. Bw. Ki Joon Kwon alisema,
"kutokana na serikali ya Korea ya Kusini na makampuni makubwa kuweka sera zenye nafuu kwa wanafunzi waliosoma nchini China, wanafunzi wengi zaidi wa nchi hiyo wanakuja China kuendelea na masomo yao. Wanafunzi 6-7 niliosoma nao katika shule ya sekondari ya juu pia wanasoma katika chuo kikuu cha Beijing."
Mwanafunzi wa pili ni Angel La Rosa kutoka Venezuela mwenye umri wa miaka 30. Hivi sasa anasoma shahada ya pili katika kituo cha uhusiano cha kimataifa ya chuo kikuu cha Beijing na atahitimu katika majira ya siku za joto mwaka huu. Tofauti na Bw. Ki Joon Kwon anayeweza kuongea kichina kwa ufasaha, ingawa ameishi nchini China kwa miaka miwili, lakini bado hajajua kuongea kichina vizuri. Alimwambia mwaandishi wetu wa habari kuwa, aliwahi kusoma lugha za Kiingereza na Kirusi katika chuo kikuu nchini Venezuela, lakini anafundishwa na kuzungumza na marafiki na wanafunzi wenzake kwa kiingereza katika chuo kikuu cha Beijing, na wanafunzi wa China wa chuo hicho wanaweza kuongea kiingereza vizuri, hivyo si tatizo kubwa kutojua kichina katika chuo hicho.
Hivi sasa, kwa Bw. Angel La Rosa, jambo muhimu ni kutafuta kazi na anatumai kufanya kazi nchini China. alisema:
"tangu kuanza kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango kwa nje, uchumi wa China umeendelea kwa kasi sana, jumuiya nyingi za kimataifa zikiwa ni pamoja na shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa, zimeweka matawi yake nchini China. Mimi nikiwa mwanafunzi wa uhusiano ya kimataifa, natumai kuwa naweza kufanya kazi inayohusu siasa ya kimataifa na mawasiliano ya kiutamaduni. Nchini China, hivi sasa kuna nafasi nyingi kama hiyo kwa kuwa wanahitaji watu kama mimi wanaoweza kufahamu kihispania, kiingereza na kirusi. Lakini katika nchi nyingine, hakuna nafasi nyingi za kazi kama hiyo. Nadhani hali hiyo ni moja ya sababu ambayo China inazidi kuwavutia wanafunzi wa nchi za kigeni."
Hivi sasa, chuo kikuu cha Beijing kina wanafunzi zaidi ya elfu 28, karibu 2100 wao wakiwa wanatoka nchi zaidi ya 90, na mbali na hayo, wanafunzi 2000 wengine wa nchi za nje wanapewa mafunzo ya muda mfupi katika chuo hicho.
Bw. Wang Yong wa chuo kikuu cha Beijing anayeshughulikia mambo ya wanafunzi kutoka nchi za kigeni alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, katika miaka ya karibuni, wanafunzi wengi zaidi wamekuja chuo hicho kuendelea na masomo yao. Alisema kuwa,
"katika miaka ya karibuni, idadi ya wanafunzi wa nchi za nje waliokuja kusoma katika chuo chetu imeongezeka siku hadi siku, mwaka 1999, kulikuwa na wanafunzi 1200 wa nje na kwa mwaka huu ni 2100, ongezeko hilo ni kubwa."
Hivi sasa, kati ya wanafunzi wa nje wanaosoma katika chuo kikuu cha Beijing, zaidi ya nusu wanatoka Korea ya Kusini na Japan, pia wako wengi wanaotoka katika nchi nyingine za Asia, lakini ni wachache tu wanaotoka Ulaya, Amerika na Afrika. Bw. Wang Yong alisema kuwa, ili kuwavutia wanafunzi wengi wa nje, chuo kikuu cha Beijing kimeimarisha ushirikiano na vyuo vikuu maarufu vikuu vya nchi za nje, zikiwa ni pamoja na Marekani na Uingereza, kuongeza idadi ya wanafunzi wa mabadilishano kati ya vyuo vikuu; pia kimeweka mafunzo ya maandalizi kwa ajili ya masomo katika nchi za nje ili kuwasaidia wanafunzi wa nje waweze kusoma katika chuo hicho bila matatizo.
Habari zinasema kuwa, chuo kikuu cha Beijing kinafanya mitihani ya kuingia chuoni kwa wanafunzi wa nje (HSK) mwezi Aprili kila mwaka. Mtihani huo unahitaji wanafunzi hao wawe na uwezo wa kimsingi wa kutumia kichina, wanafunzi walioshindwa kutimiza sharti hilo lazima kwanza waende kwenye kituo cha kichina kujifunza kichina. Gharama ya kusoma katika chuo kikuu cha Beijing ni karibu yuan elfu 60 hadi 70 kwa mwaka, ikiwa ni pamoja na gharama ya masomo yuan elfu 30 hadi 40. wanafunzi wa nje wanaweza kuishi katika mabweni ya wanafunzi na kula chakula katika mabwalo ya chuo hicho, pia wanaruhusiwa kupangisha nyumba nje ya chuo. maktaba, maabara na zana za mtandao wa Internet zinafunguliwa kwa wanafunzi wa nje bure.
Idhaa ya Kiswahili 2005-02-09
|