Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-02-10 19:03:09    
Wachina wanavyojiandaa kusherehekea sikukuu ya jadi ya mwaka mpya wa China .

cri

    Sikukuu ya Spring ambayo ni sikukuu ya jadi ya mwaka mpya wa China ni sikukuu muhimu kabisa nchini China. Sikukuu hiyo ni wakati wa wachina wa familia moja moja kukutana pamoja na kusherehekea sikukuu hiyo kwa pamoja. Kabla ya mwaka mpya wa jadi kuwadia, wachina hasa wanaoishi vijijini hufanya pilika pilika za maandalizi kama vile kusafisha nyumba, na kununua vitu maalum vya mwaka mpya, ambapo vijana wachumba hufunga ndoa kabla ya mwaka mpya, na ukienda vijijini utaona hali ya shamrashamra ya sikukuu, kwani fataki ya kusherehekea ndoa na ya kuhamia kwenye nyumba mpya husikika na kuonekana usiku hapa na pale.

    Katika sehemu tofauti nchini China, desturi za kusherehekea mwaka mpya wa jadi ni tofauti kidogo, lakini mambo mengi yanafanana, kama vile kuandaa chakula kitamu cha aina mbalimbali, kubandika karatasi nyekundu zinazoandikwa maneno ya kusherehekea mwaka mpya na kuombea heri na baraka, kubandika maua yanayokatwa kwa karatasi nyekundu kwenye madirisha, kutundika kandili zenye rangi ya kupendeza na kadhalika. Katika gulio la kitongoji cha Dazhou, mkoani Henan, mwandishi wetu wa habari alimkuta Bwana Li Xinguo aliyenunua vitu vya kusherehekea mwaka mpya, Bwana Li akimwambia kwa furaha:

    "Kwa kuwa mwaka jana tulipata mavuno mengi, familia zote katika kijiji chetu zina pato zuri kuliko zamani, hivyo tunaanza kufanya maandalizi ya mwaka mpya mapema zaidi kuliko ilivyo kawaida. Tofauti na wakati uliopita, mwaka huu mimi nitanunua vitu vyenye thamani zaidi, kama vile mtambo wa kusafisha maji."

    Bwana Li Xinguo alisema kuwa, hivi sasa wanapata faida kubwa zaidi kuliko zamani kutokana na kilimo, kila wakilima hekta moja ya shamba hupewa ruzuku ya yuan 200 na serikali. Mwaka jana familia yake si kama tu imepanda mimea ya nafaka, bali pia imepanda pamba na mboga za aina mbalimbali, pato la familia yake kwa mwaka jana liliongezeka kwa yuan zaidi ya 1500 kuliko mwaka juzi.

    Katika miaka miwili iliyopita, serikali ya China imetekeleza sera ya kutoa ruzuku kwa wakulima, kupunguza kodi za kilimo, na kuwahamasisha wakulima waendeshe shughuli mbalimbali za kilimo ili wapate faida kubwa zaidi.

    Wakulima wanaofanya kazi ya kibarua mijini pia wamerudi nyumbani kusherehekea mwaka mpya wakiwa na pato la mwaka mpya mfukoni. Ili kuwarahisisha wakulima hao kurudi nyumbani, idara za reli za China ziliandaa magarimoshi maalum. Katika kituo cha garimoshi cha Chengdu, mkoani Sichuan, kusini magharibi mwa China, mwandishi wetu wa habari alimkuta kibarua Bwana Chen Haoqing aliyerudi kutoka Beijing ambaye alisema kwa furaha:

    "Nimefanya kazi Beijing kwa miaka mitatu. Mwaka huu serikali imetoa sera maalum ya kuwalazimisha wanakampuni kutupatia mishahara kwa wakati. Hivyo nimekuwa na pesa za kununua vitu vya mwaka mpya."

    Bwana Chen Haoqing alisema kuwa, yeye na mke wake wote wanafanya kazi za kibarua mjini Beijjing, pato lao la mwaka mzima linazidi yuan elfu 20. kutokana na serikali kuimarisha usimamizi wa vibarua kutoka vijijini, hivi sasa si kama tu vibarua wakulima wanaweza kupata mishahara kwa wakati, hali yao ya kimaisha na ya kikazi pia imeboreshwa dhadhiri.

    Mwandishi wetu wa habari amefahamishwa kuwa, kutokana na serikali ya China kuimarisha nguvu katika kuwapatia vibarua kutoka vijijini mishahara yao, hadi ilipofika mwanzoni mwa mwezi wa Januari ya mwaka huu, mashirika mbalimbali nchini yamewalipa mishahara yote vibarua waliokuwa wanadai kwa miaka mingi. Hivyo mwaka huu kama Chen Haoqing, vibarua wakulima wote wanaweza kusherehekea mwaka mpya kwa furaha.

    Wakati watu wanaposhughulikia kununua vitu vya mwaka mpya, Bwana Wang Erli anayeishi mjini Tianjin alipata vitu vya mwaka mpya vilivyotolewa na shirikisho la wafanyakazi la mji huo kama vile mchele, unga wa ngano, mafuta na kadhalika. Bwana Wang alisema kuwa, hana mguu mmoja kutokana na ajali aliyopata miaka 10 iliyopita, kuanzia wakati huo, chini ya msaada wa serikali, amewahi kupata kazi katika kiwanda fulani, lakini sasa kiwanda hicho kilisimama, hivyo hana ajira. Shirikisho la wafanyakazi la Tianjin lilipopata habari yake lilimworodhesha kama mmoja ya watu wanaohitaji msaada. Bwana Wang alipewa kadi moja maalum ya kijani na shirikisho kuu la wafanyakazi, kila baada ya muda fulani, yeye anaweza kupata vitu vya kimaisha kutokana na kadi hiyo. Na kila inapofikia sikukuu, viongozi wa mjini huenda nyumbani kwake kumpatia pesa au vitu vya mahitaji.

   Mwandishi wetu wa habari alipata habari kutoka shirikisho kuu la wafanyakazi la China ikisema kuwa, ili kuziwezesha familia nyingi zenye matatizo ya kiuchumi kama ya Bwana Wang Erli nchini China zisherehekee mwaka mpya kwa furaha, kila inapofika wakati wa mwaka mpya wa jadi, mashirika ya wafanyakazi na idara za huduma za raia katika ngazi tofauti nchini zinakwenda nyumbani kwao kuwasalimia, na kuwapatia chakula na mahitaji ya lazima ya kimaisha. Mwaka huu shirikisho kuu la wafanyakazi la China limetoa yuan milioni 35 kwa watu wenye matatizo ya kiuchumi.

    Sikukuu ya mwaka mpya wa jadi pia ni likizo ya shuleni, wanafunzi wengi wanarudi nyumbani kukutana na wazazi wao, lakini wale wenye matatizo ya kiuchumi wanalazimika kubaki shuleni na kujaribu kujipatia kazi ya muda ili kuwasaidia wazazi wao kiuchumi. Lakini mwaka huu, wanafunzi zaidi ya 400 wa vyuo vikuu vya mjini Beijing akiwemo Zhang Lei walipewa nauli ya kurudi nyumbani, pesa hizo zilichangishwa na shirika moja la magazeti kutoka kwa jamii. Zhang Lei alifurahi sana akisema:

    "Mimi najisikia vizuri sana, kwangu mimi hizo pesa siyo nauli tu, bali ni matumaini ya kukutana na familia yangu, kwani sikukuu ya Spring ni muhimu sana. Bila shaka nitakumbuka upendo huo kutoka kwa jamii, nitajifunza kwa bidii zaidi siku za usoni ili nipate matokeo mazuri ya kimasomo na kuihudumia jamii yenye upendo."

Idhaa ya Kiswahili 2005-02-10