Kutokana na maendeleo makubwa ya uchumi wa China na mazingira mazuri ya kuanzisha shughuli yanayoboreka siku hadi siku, wanafunzi wengi wa China wamerejea na matokeo ya utafiti wao baada ya masomo katika nchi za nje na kuanzisha shughuli zao nchini. Hivi sasa viwanda vyao vinaendelea vipi? Katika siku za karibuni, mwandishi wetu wa habari alifanya mahojiano katika eneo maalum la sayansi na teknolojia la Zhong Guan Cun.
Eneo maalum la sayansi na teknolojia la Zhong Guan Cun lililoko sehemu ya kaskazini magharibi ya Beijing, ni eneo maarufu kabisa la sayansi na teknolojia kote nchini. Kuna raslimali nyingi za utafiti wa sayansi na teknolojia na elimu kwenye eneo hilo, zikiwa ni pamoja na taasisi za utafiti wa sayansi na teknolojia zaidi ya 100 na vyuo vikuu zaidi ya 30 vya elimu ya juu. Aidha, ili kuwahamasisha na kuwaunga mkono wanafunzi warejee baada ya masomo yao katika nchi za nje na kuanzisha shughuli zao katika eneo hilo, eneo hilo lilianzisha idara kuu ya utoaji huduma kwa kuanzisha shughuli na kutoa misaada ya fedha kwa watu hao, ikiwa ni pamoja na kuwapa watu hao kiasi fulani cha fedha bila ya malipo na mikopo yenye riba nafuu, na kutekeleza sera yenye manufaa kwao katika utozaji wa kodi.
Kutokana na sababu hizo, eneo la Zhong Guan Cun limewavutia wanafunzi wengi waliosoma nje kuja na kuanzisha shughuli zao. Bw. Cui Chun guang aliyerudi kutoka Uingereza mwaka jana alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema:
"tulikuwa tunafanya utafiti kuhusu teknolojia mpya, na tumerudi kutafuta nafasi na mahali pazuri pa kuanzisha shughuli zetu. Utumiaji wa teknolojia mpya katika uzalishaji mali unahitaji viwanda vya sekta husika, soko na njia husika za kusambaza bidhaa, pia unahitaji mawasiliano na uungaji mkono ndani ya sekta hiyo. Hivyo tunatafuta mahali zilipokusanyika teknolojia mpya za juu, na mahali kama hapo nchini China bila shaka ni eneo la Zhong Guan Cun. "
kiwanda kilichoanzishwa na Bw. Cui Guang cun kinatafiti kuhusu teknolojia ya kukusanya taarifa bila waya (wireless info-collecting technology). Kutokana na maelezo yake, teknolojia hiyo inaweza kutumika katika sekta ya usambazaji wa bidhaa, uchukuzi na mawasiliano. Kwa mfano, teknolojia hiyo ikitumiwa katika maduka makubwa, wateja hawana haja tena ya kusubiri kwenye foleni kwa ajili ya kulipia bidhaa. kwa sababu wateja wanaposukuma vitoroli vya kubebea bidhaa dukani, bidhaa zote zilizochaguliwa nao zitatambuliwa mara moja na wapokea fedha watajua mara moja kuwa umenunua kitu gani na bei yake; katika maghala na bandari za makontena, teknolojia hiyo inaweza kuonesha mahali halisi ya bidhaa, hivyo wateja watapata bidhaa zao kwa urahisi kutoka kwenye bidhaa nyingi zilizopangwa.
Hivi karibuni, teknolojia hiyo imepewa tuzo ya ubunifu na serikali ya Uingereza. Bw. Cui Guang cun alimwambia mwandishi wetu wa habari kwa furaha,
"teknolojia hiyo hivi sasa inaongoza duniani kote, wateja wengi wa nchini na duniani wanawasiliana nasi. Utumiaji wa teknolojia hiyo una mustakbali mzuri, na hiyo inasifiwa kuwa ni mapinduzi ya sekta hiyo."
Kiwanda kilichoanzishwa na mwanafunzi mwengine aliyerudi kutoka Italia Bw. Zhang Bao cheng pia kimepata mafanikio. Bw. Zhang alimwambia mwandishi wa habari kuwa, China ni nchi yenye upungufu mkubwa wa maji, hivyo kiwanda chake kinatafiti na kutengeneza bidhaa za kushughulikia maji na kuhimiza matumizi tena ya maji yaliyotumika. Pia, bidhaa hizo zinaweza kupunguza matumizi ya nishati, na kuondoa vijidudu na virusi kwenye maji kwa ufanisi. Kutokana na kuwa bidhaa hizo zilizobuniwa naye zinatangulia duniani katika kushughulikia maji, hivyo zinaaminiwa na wateja wengi wa nje. Bw. Zhang alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa,
"Ingawa kampuni yetu ilianzishwa kwa muda mfupi tu uliopita, lakini tumeshapata baadhi ya wateja, hasa wateja wa nje. Hivi sasa, bidhaa zetu zinauzwa nchini Japan, Hispania, Marekani, India, Korea ya Kusini, Australia, Singapore na Uturuki."
Katika eneo maalum la sayansi na teknolojia la Zhong Guan Cun, kuna wanafunzi wengi waliorudi kutoka nje kama Bw. Cui Chun guang na Bw. Zhang Bao cheng. Kwa mfano, Bw. Deng Zhong han aliyerudi kutoka Marekani baada ya masomo mwaka 1999 pamoja na kikundi cha wanafunzi wengine anachokiongoza, wamefanikiwa kupata utaalamu zaidi ya 200 nchini na duniani katika sekta ya kutengeneza digital CMOS chip, na zaidi ya chip hizo milioni 20 ya bidhaa hizo walizotengeneza zimeuzwa duniani, zikiwa zinachukua asilimia 60 ya soko la dunia; Bw. Cheng Jing aliongoza kuanzisha kampuni moja ya kutengeneza Bio-CMOS chip, baadhi ya bidhaa zao zimefikia kiwango cha kimataifa.
Takwimu zinaonesha kuwa, katika miaka ya karibuni, wanafunzi wengi zaidi waliorudi kutoka nje wanachagua kuanzisha shughuli zao katika eneo la Zhong Guan Cun, kwa wastani kila siku makampuni mawili yaliyoanzishwa na wanafunzi hao yanaandikishwa kwenye eneo hilo. Hivi sasa kwa ujumla, kuna makampuni zaidi ya 2300 yaliyoanzishwa na wanafunzi kama hao kwenye eneo hilo, na wanafunzi karibu 6000 waliorudi kutoka nje wanafanya kazi katika makampuni hayo, na wengi wao wanafanya utafiti wa miradi inayofanyiwa utafiti pia na maeneo maalum ya nje ya sanyasi na teknolojia yanayojulikana kote duniani, kama vile eneo la Silicon valley nchini Marekani.
Mkuu anayehusika wa kamati ya usimamizi wa eneo la Zhong Guan Cun Bw. Chu Jun wei alisema kuwa,
"katika siku za baadaye, tutaendelea kuweka mazingira mazuri zaidi ya ajira na kuanzisha shughuli kwa wanafunzi waliorudi baada ya masomo nje, na kutarajia kuwavutia wanafunzi wengine zaidi ya 4000 kuanzisha shughuli zao hapa katika miaka 3 hadi 5 ijayo, ili kuongeza idadi ya wanafunzi hao walioajiriwa katika makampuni ya teknolojia mpya ya juu kwenye eneo hilo ifikie elfu 10 na idadi ya makampuni yaliyoanzishwa na wanafunzi hao ifikie elfu 3."
Idhaa ya Kiswahili 2005-02-16
|