Shu Cai ni mtu aliyewahi kuwa mwanadiplomasia, meneja mkuu wa kampuni na mwishowe kuwa mshairi.
Mshairi Shu Cai ana umri wa miaka 40, ni mshairi anayejulikana sana katika fani ya ushairi.
Mapema alipokuwa katika Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni Beijing alikuwa mshairi aliyejulikana miongoni mwa wanafunzi, Bw. Shu Cai alisema, "Tokea nilipokuwa katika sekondari nilipenda kuandika mashairi ya kisasa, na pia niliwahi kujaribu kuandika mashairi kwa mtindo wa kale. Baada ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni Beijing niliwashirikisha wanafunzi wenzangu kuanzisha jarida la mashairi lililokuwa likijulikana kwa jina la TEST, na nilipokuwa katika kidato cha nne nilianza kuandika mashairi kwa nyakati zote za mapunziko kwa kuwa wakati huo fasihi ilikithiri katika chuo hicho."
Bw. Shu Cai alihitimu katika Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni Beijing mwaka 1987 na alipata kazi katika Wizara ya Biashara ya China na Nchi za Nje. Kwa kuwa lugha aliyojifunza chuoni ni Kifaransa, mwaka 1990 alitumwa na wizara yake kwenda kufanya kazi katika ubalozi wa China nchini Senegal. Miaka kadhaa ya maisha ya wanadiplomasia yalimwathiri sana katika maisha yake ya baadaye. Bw. Shu Cai alisema, "Kwa kweli kazi ya kuwa mwanadiplomasia inanifaa sana, kazi hiyo inataka mtu awe anafuata nidhamu na kutunza siri. Lakini mwishowe niliamua kuacha kazi hiyo, na sababu ni kuwa uandishi wa mashairi ulinivutia zaidi, na waandishi wa mashairi wanahitaji maisha huru."
Baada ya kufanya kazi huko barani Afrika kwa miaka minne, Bw. Shu Cai alirudi nyumbani China mwaka 1994, alichapisha kitabu chake cha mashairi "Siri za Moyoni" ambacho kilikusanya mashairi yake 150 aliyoandika katika muda karibu miaka 10. Bw. Shu Cai alisema kuwa mashairi hayo mengi zaidi yalitokana na undani wake moyoni. Bw. Shu Cai alisema, "Najitahidi kuonesha upendo mkubwa kwa maisha. Naona mambo yanayostahili kuandikwa kwa mashairi katika jamii yetu ni mengi na siwezi kumaliza kuyaandika katika maisha yangu yote."
Ili aweze kutumia muda mwingi kuandika mashairi, mwaka 2002 Bw. Shu Cai aliacha kazi iliyompatia mshahara mkubwa kutokana na cheo chake cha meneja mkuu wa kampuni na kufanya kazi katika taasisi ya fasihi ya nchi za nje katika Taasisi Kuu ya Sayansi ya Jamii. Katika idara hiyo aliandika mashairi na huku akitafsiri mashairi ya nchi za nje kwa Kichina. Kwa nyakati tofauti alichapisha vitabu alivyotafsiri kutoka Kifaransa vya "Mashairi Yaliyoteuliwa ya Rene Char" na "Mashairi Yaliyoteuliwa ya Pierre Reverdy", mashairi yaliyoandikwa na waandishi mashuhuri wa Ufaransa. Bw. Shu Cai alisema kuwa kwa kusoma maandishi ya washairi hao wa Ufaransa alipata hisia zinazofanana nao. Alisema, "Mimi natafsiri tu yale mashairi ya waandishi ninaowapenda, sababu ni kuwa Wachina wanaofahamu Kifaransa ni wachache, na sababu nyingine ni kuwa ninapotafsiri mashairi inanipasa nizame katika mashairi yao na ninapoogelea katika mashairi yao najirutubisha mwenyewe."
Bw. Shu Cai alisema, "Nashindwa kueleza vilivyo ni kwa nini nashabikia uandishi wa mashairi, na kwa ajili ya kuandika mashairi nimetumia juhudi zote, hata watu wengine wananiona kama punguani. Lakini hata hivyo nimekwisha ingia katika bwawa hilo, sitajuta. Mimi sina tamaa ya kutaka umaarufu au kujipatia faida, hamu yangu ni kuandika tu mashairi kwa uwezo wangu wote, na wasomaji wasiojulikana watanikubali kama si leo basi kesho."
Idhaa ya kiswahili 2005-02-17
|