Ingawa kulikuwa giza kidogo ndani ya jumba lakini mara niligundua mwandishi Bi. Zhao Meiping aliyepewa sasa hivi tuzo ya fasihi ana kovu mkononi.
"Hili kovu ulipata kazini ulipovunja mawe?"
"Ndio."
Kutokana na umaskini, Bi. Zhao Meiping alikuwa mvunja mawe alipokuwa na umri wa miaka 14, wakati huo alikuwa amemaliza tu kidatu cha tano katika shule ya msingi.
Kazi ya Zhao Meiping ilikuwa ni kuvunja mawe kwa nyundo yenye uzito wa ratili 10, alipitisha maisha yake katika mazingira ya kelele ya kugonga gonga mawe.
Kila alipomaliza kuvunja mawe tani moja alipewa hela senti themanini na tano. Zhao Weiping alisema, ili aweze kuvunja mawe mengi kila siku alifika kwenye machimbo ya mawe mapema na kuchelewa kurudi nyumbani, kila mara aliposikia tu mngurumo wa kulipua mawe kwa baruti naye hukimbilia huko ili apate mawe mengi zaidi wakati vipande vya mawe vilivyorushwa vilikuwa bado vikianguka, na mara nyingi alipigwa na vipande hivyo. Kovu kwenye mkono wake wa kushoto ndio jeraha alilopata kwa kupigwa na kipande cha mawe kilichorushwa.
Kazi hiyo nzito aliifanya kwa miaka mitano, mikono yake ilijaa sugu nene. Ingawa kazi ngumu ilimchosha sana lakini hamu yake ya kujifunza haikufifia. Aliandika vitabu vya shajara 14 ndani ya nyumba ya mawe, kwenye shajara aliandika hisia, uchungu na furaha aliyoipata mara chache. Kutokana na kuwa maneno mengi kwake yalikuwa mageni na hakujua namna ya kuandika, kamusi ilikuwa tegemeo pekee, na kamusi kadhaa zilichanika kwa sababu ya kupekuliwa sana. Kamusi ilikuwa ni kitabu alichopenda sana. Alisema, "katika miaka nilipofanya kazi katika machimbo ya mawe, nilikuwa sina pesa za kununulia vitabu vingine, hivyo nilisoma kamusi kila siku na nilipata elimu nyingi kutoka kamusi."
Bi. Zhao Meiping alipitisha maisha yake ya kijana kwenye machimbo ya mawe, na huku uwezo wake wa kuandika pia ulichipuka huko na kukua katika miaka hiyo. Kwenye mashairi yake aliandika, "Ukiwa jani dogo chini ya jiwe, na hakuna mtu aliyeondoa jiwe hilo basi uliondoe wewe mwenyewe na ujiokoe."
Zhao Meiping alipokuwa na umri wa miaka 19 alikwenda mji mkuwa wa China Shanghai akiwa na vitabu vyake 14 vya shajara, huko mjini alikuwa kibarua mbali na maskani yake, vitabu 14 vya shajara na kamusi iliyochanika vilikuwa nguvu yake ya kujiokoa.
Kazi aliyoipata katika mji wa Shanghai ilikuwa ni mtumishi wa mkahawa mmoja. Hapo mwanzo, alikuwa na furaha tele kwa sababu hatateswa na jua kali wala kupigwa na upepo. Alifanya kazi hiyo bila kujali uchovu, alionekana mwenye juhudi nyingi miongoni mwa watumishi wenzake. Lakini baada ya muda aliiacha kazi hiyo ingawa alishawishiwa sana na mwenye mkahawa kutokana na kuwa alishindwa kuvumilia jinsi mwenye mkahawa alivyowadanganya vibarua wakulima kwa kuwauzia tambi iliyochachika na mayai viza, akajipatia kazi katika kiwanda cha kushona nguo. Alifikiri, kazi ya ushonaji ni kazi ya ufundi, ni kazi bora kuliko kusafisha mabakuli na sahani kila siku katika mkahawa.
Mwaka 1994 Zhao Meiping alijaribu kupeleka makala yake kwenye mashirika ya uchapishaji, siku moja makala yake kweli ilikubaliwa na kuchapishwa katika jarila moja. Tokea hapo makala yake yalikuwa yanachapishwa moja baada ya mengine, na baadaye alianza kuchapisha hadithi zake kwenye majarida ya "Riwaya Shanghai", "Hadithi Shanghai" na Gazeti la Jioni la Xinmin. Katika muda wa miaka mitatu, aliandika hadithi nyingi kwa mujibu wa matukio ya kweli na kuchapishwa kwenye Jarida la Shanghai. Mwaka 1998 alialikwa kuwa mhariri wa Jarida la Zhiyin na kuwa mfanyakazi wa fasihi. Mwaka 2005 alipata tuzo ya fasihi kutokana na kitabu chake cha "Maisha Yangu". Kwenye utangulizi wa kitabu hicho aliandika, "maisha magumu ni somo la chuo kikuu mradi tu hukuangushwa hayo utajiimarisha; mradi tu ukijitahidi kwa nia imara, jambo lolote unaweza kulifanikisha."
Idhaa ya kiswahili 2005-02-21
|