Kwa wakulima na wafugaji wa kabila la wahazak la mkoa unaojiendesha wa kabila la wauygur wa Xinjiang, kaskazini magharibi mwa China kuna desturi kuwa, mtoto akizaliwa huwa na mama wawili, mmoja ni mzazi na mwingine ni mkunga wake. Mtoto atamheshimu mama yake mkunga katika maisha yake yote kama mama mzazi.
Wakulima na wafugaji elfu kadhaa wa wilaya ya Fuhai ya mbuga ya Aletai wanamheshimu mama mkunga, ambaye ni mkuu wa kituo cha afya cha wanawake na watoto wachanga cha wilaya ya Fuhai Bibi Jianger Reharti .
Bibi Jianger Reharti mwenye umri wa miaka 52 ameshughulikia kazi ya ukunga kwa miaka 34. Katika miaka 34 iliyopita, amewapokea watoto elfu kadhaa kuja duniani, na ana visa vingi vya kusimulia. Mwezi wa Mei wa mwaka 1980, mjamzito mmoja wa kabila la wahazak alikosa uwezo wa kudhibiti haja ndogo na haja kubwa wakati wa kujifungua, hivyo mtoto wake alipozaliwa alikuwa amechafuliwa mwilini na kinywani, na mtoto huyo alikuwa mahututi. Ili kuokoa maisha ya mtoto huyo, bibi Jianger hakujali uchafu, alivuta vitu vya uchafuzi kutoka kinywani mwa mtoto kwa kutumia kinywa chake mwenyewe. Baada ya dakika saba mtoto aliokolewa, wanafamilia wa mtoto huyo walisisimka sana na kumshukuru sana bibi Jianger.
Mwaka 1971, Bibi Jianger Reharti alianza kufanya kazi ya uuguzi katika hospitali ya shamba la Gongan la wilaya ya Fuhai lenye idadi kubwa ya watu wa kabila la wahan. Siku ya kwanza alikutana na tatizo gumu, kwa kuwa yeye aliishi katika mazingira ya lugha ya kihazak, hakufahamu kichina, hivyo hakuweza kusoma maagizo ya matumizi ya dawa, na hakuweza kuelewana na wagonjwa wa kabila la wahan, na hata hakujua jinsi ya kudunga sindano na kubadilisha dawa. Hali hiyo imewahi kumfanya alaumiwe na wagonjwa kutokana na kosa hilo.
Ili kuweza kuimudu kazi ya uuguzi, bibi Jianger alijifunza mwenyewe lugha ya kichina na ujuzi wa uuguzi. Ili kufahamu haraka sehemu za mwili alifanya mazoezi ya kujidunga sindano katika mwili wake mwenyewe. Baadaye alitumwa kusoma katika chuo kikuu cha utibabu cha Xinjiang. Baada ya kusoma kwa bidii, Bibi Jianger alikuwa anaweza kuongea kichina vizuri na kiwango chake cha ujuzi wa uuguzi pia kiliinuka sana, hata alichapisha makala maalum kuhusu mada ya kazi yake kwa lugha ya kichina.
Bibi Jianger alifuatilia sana maisha na afya ya wagonjwa. Baada ya kuwa mkuu wa kituo cha afya cha wanawake na watoto cha wilaya ya Fuhai mwaka 1998, yeye huwaambia wenzake kuwa, wajawazito na watoto wachanga huwa na nguvu dhaifu sana, wakiwa wafanyakazi wa utibabu lazima wawashughulikie watu hao kwa makini.
Kila alipokwenda Bibi Jianger hakuweza kusahau kuwafahamisha wakazi ujuzi wa jinsi ya kuwatunza watoto na kuwahamasisha wajawazito kwenda hospitali kujifungua ili kukwepa hatari.
Mwaka 2004, bibi Jianger alieneza ujuzi kuhusu kinga na tiba ya maradhi kwa wanawake elfu kumi, na kati ya watoto wachanga 687 waliozaliwa mwaka huo, zaidi ya 300 walikaguliwa naye. Mpaka sasa ametembelea vijiji vyote 62 vya wilaya hiyo.
Ili kuboresha zana duni za kituo chake na kuongeza uwezo wa kuwatibu wagonjwa zaidi, bibi Jianger mara kwa mara alikwenda Urumqi, mji mkuu wa mkoa huo ulio kwenye umbali wa kilomita 600 kwa kupanda basi la usiku na kubeba chakula kutafuta mwenyewe msaada. Kutokana na juhudi zake, hospitali za vitongoji vyote vya wilaya ya Fuhai zimekuwa na zana zinazohitajika. Pia aliwatuma makada husika wa vituo vya afya vya wanawake na watoto kushiriki kwenye semina husika kwa zamu, ili kuinua uwezo wa wafanyakazi husika, na kuhakikisha afya za wajawazito au watoto wachanga wa sehemu hiyo. Katika miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2001 hadi 2004, hakuna mjamzito aliyekufa wakati wa kujifungua na mtoto mchanga kuugua ugonjwa wa pepopunda katika wilaya ya Fuhai. Mwaka 2004, kituo cha afya cha wanawake na watoto cha wilaya ya Fuhai kilipata tuzo ya idara hodari iliyotolewa na wizara ya afya ya China, pamoja na kamati ya kazi ya wanawake na watoto ya baraza la mawaziri la China na wizara ya fedha. Bibi Jianger Reharti pia alisifiwa kuwa mwanachama hodari wa chama cha kikomunisti katika mkoa wa Xinjiang.
Idhaa ya kiswahili 2005-02-25
|