Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-10 22:15:59    
Msomi mkubwa wa China Bw. Feng Yidai

cri

Bw. Feng Yidai na Bibi Zheng Anna

Mnamo tarehe 23, katika sikukuu ya taa ya Kichina, Wachina wanapojumuika na jamaa zao kusherehekea siku hiyo kama ilivyo desturi yao, msomi na mfasiri mkubwa wa China Bw. Feng Yidai alifariki dunia mjini Beijing kutokana na ugonjwa. Watu wa nyanja za utamaduni walifanya shughuli za kila aina kumkumbuka mwanautamaduni huyo mkubwa aliyekuwa na umri wa miaka 92.

Bw. Feng Yudai anajulikana na kuheshimiwa sana katika nyanja za utamaduni, kutokana na mchango wake mkubwa katika uchapishaji na kutafsiri. Bw. Feng Yidai alilazwa hospitali mwaka mmoja uliopita, alilazimika kuacha upendo wake wa kusoma na kuandika. Ingawa alilazwa hospitali lakini kifo chake pia kiliwashitusha watu wengi. Mchoraji mashuhuri wa picha za dhihaka Bw. Ding Cong alikuwa ni rafiki yake mkubwa. Alisema, "Nilianza kumfahamu mwishoni mwa mwaka 1937 nilipokuwa Hong Kong, urafiki wetu ulioanzia wakati huo mpaka sasa umekuwa na zaidi ya miaka 70. Mtoto wake aliponiambia kuwa amepata ugonjwa wa kiharusi, nilidhani atapona kwani aliwahi kupata ugonjwa huo mara saba hivi lakini mara zote alipita salama, sikutegemea kama safari hii angeshindwa haraka, hata sikuweza kuongea nane. Kwa kweli nimesikitika sana."

Bw. Feng Yidai alizaliwa mwaka 1913 mjini Hangzhou, kusini mwa China, alijiita "mtoto asiye na mama". Mama yake alimzaa yeye nchini Japan alipokuwa na umri wa miaka 28, lakini baada ya mwezi mmoja alifariki dunia kutokana na ugonjwa wa uzazi. Bw. Feng Yidai aliweza tu kumwona mama yake kwa picha.

Mwaka 1936 Bw. Feng Yudai alihitimu katika chuo kikuu mjini Shanghai, somo lake lilikuwa ni menejimenti ya viwanda na biashara. Katika miaka alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu alifahamiana na Bi. Zheng Anna, mwanachama wa kikundi cha tamthilia ya Kiingereza, baadaye walioana. Mchoraji Bw. Ding Cong alipokumbuka alisema, "Alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu alipenda sana tamthilia. Mkewe alikuwa hodari wa kutafsiri, walitafsiri kwa pamoja. Bw. Feng Yidai alikuwa mtu asiyejali uchovu na mwenye juhudi kubwa katika kazi ya kutafsiri, baadaye alikuwa mfasiri mkubwa kwa kutumia muda wa mapumziko."

Bw. Ding Cong aliposema Bw. Feng Yidai kuwa ni mfasiri mkubwa wa muda wa mapunziko, alikuwa na maana kuwa tokea miaka ya 30 ya karne iliyopita, Bw. Feng Yidai alikuwa anajulikana katika nyanja za uchapishaji na utamaduni. Aliwahi kuanzisha machapisho ya utamaduni huko Hong Kong, kushiriki na kuanzisha jarida la Kiingereza "Waandishi wa China", jarida la "Kupalilia" na "Filamu na Tamthilia". Katika kazi ya utafsiri, Bw. Feng Yidai pia alijulikana sana, yeye ni mmoja wa watu waliotangulia kuwajulisha Wachina maandishi ya mwandishi wa Marekani Ernest Hemingway. Baada ya Jamhuri ya Watu wa China kuasisiwa mwaka 1949, katika miaka mingi alikuwa mkurugenzi wa kitengo cha uchapishaji katika Shirika la Uchapishaji wa Lugha za Kigeni na mkurugenzi wa jarida la "Fasihi ya China" katika shirika hilo. Alitetea fasihi ya nchi za nje zitafsiriwe bila miiko na alitumia juhudi kubwa katika utafiti na uhakiki kuhusu fasihi ya Ulaya na Marekani. Katika maisha yake alitafsiri vitabu zaidi ya 20.

Bw. Feng Yicai na Bibi Huang Zongying

Kama wasomi wengi wa China walivyokuwa, kwamba katika miaka ya 60 ya karne iliyopita, kutokana na fikra potofu zilizoshamiri kote nchini China, alidhalilishwa na hakuweza kufanya kazi mpaka alipokuwa na umri wa miaka karibu 60. Mnamo mwezi Aprili mwaka 1979, akiwa pamoja na wengine alianzisha jarida la "Kusoma Vitabu" na kuwa naibu mhariri mkuu wa jarida hilo. Aliandika makala nyingi na uhakiki wa fasihi. Jarida hilo mpaka sasa linaendelea kusomwa sana.

Bw. Feng Yidai alipenda kuweka urafiki na watu wengi, alikuwa mkarimu wa kuwasaidia wenzake kielimu na aliheshimiwa sana katika nyanja za fasihi na sanaa. Katika majira ya Autumn mwaka 1993, Bw. Feng Yidai aliyekuwa karibu kufikia umri wa miaka 80 alioana na mwandishi mkubwa aliyekuwa karibu na umri wa miaka 70 Huang Zongying, ndoa yao ilikuwa simulizi la furaha. Mtoto wake Feng Hao alisema, "Marafiki zake walikuwa wengi sana. Akilini mwangu yeye ni baba mpole tena mkali. Bila makusudi nilijifunza mengi kutoka kwake, moja ni kuandika makala, upeo wangu wa kuandika makala ni mkubwa na napenda kusoma. Yote hayo yanatokana na baba yangu. Jambo moja ambalo nalikumbuka sana ni kuwa mwanzoni nyumba tuliyoishi ilikuwa ndogo sana, na halafu tulihama kwenye nyumba kubwa. Katika shughuli zote za uhamisho jambo la kwanza alilotaka lilikuwa ni kutaka kumwekea meza yake ya kusomea, kisha akaanza kusoma na kuandika, alijifanya hajui shughuli nyingine."

Idhaa ya kiswahili 2005-03-07