Ngojela za kuchekesha ni moja ya aina michezo ya sanaa za jadi nchini China, ambayo hadi leo imekuwa na historia ya karibu miaka mia mbili. Hapo awali sanaa hiyo ilikuwa ni mazungumzo na simulizi miongoni mwa raia. Mchezo huo unachekesha kwa maneno, kuiga vitendo na kuimba kwa lengo la kudhihaki hali mbaya iliyotokea katika jamii au kuchekesha kwa hadithi za ajabu.
Marehemu Bw. Hou Baolin, baba wa Hou Yuewen alikuwa ni msanii mkubwa wa michezo ya kuchekesha na mazungumzo yake yanajulikana kwa Wachina wengi. Lakini mtoto wake Hou Yuewen alipokuwa mdogo alikuwa hapendi ngojela za kuchekesha na hata alikuwa anakirihishwa na mchezo huo. Sababu ilikuwa baba yake alitumia muda mwingi katika michezo yake bila kuweza kumtunza yeye, hakuwahi mara nyingi kumchukua kwenye sinema au kutembea madukani, na hakudiriki hata kumwuliza hali yake ya masomo. Hou Yuewen aliona kuwa baba yake hakuwajibika ipasavyo, ngojela za kuchekesha ziliwatenganisha. Hivi sasa, Hou Yuewen ambaye amekuwa msanii maarufu wa mchezo wa kuchekesha sasa anamtathmini hivi baba yake. Alisema,
"Nikisema kuto kwenye nafasi ya usanii, baba yangu ni mtu ninayemheshimu sana, ni mtu ninayetamani kuwa kama yeye maishani mwangu. Lakini nikisema kutoka kwa nafasi ya mtoto wake, nina malalamiko mengi. Lakini sasa nimetambua ya yeye kunitendea vile."
Kwa bahati siku moja baba yake alimchukua kwenda kwenye maonesho ya michezo ya ngojela za kuchekesha. Baada ya michezo kumalizika, baba yake alitoka naye na kwenye mlango watu waliomsubiri walijazana wakimpigia makofi kwa shangwe. Kuona hali hiyo Hou Yuewen alisisimka sana, na ndipo wakati huo Hou Yuewen alianza kuwa na hamu ya ngojela za kuchekesha na kuwa na heshima kubwa kwa baba yake.
Baba yake Hou Baolin alimhimiza sana mwanawe Hou Yuewen katika usanii. Mchezo wa kuchekesha ni aina ya sanaa ngumu, ambayo inataka mchezaji awe na uhodari wa kuiga vitendo, awe na elimu pana na kueleza wahusika wa aina mbalimbali vilivyo. Baba yake alisema, msanii wa ngojela lazima awe mtaalamu wa mambo matano, nayo ni fasihi, usanii, siasa, diplomasia na ujuzi wa mambo mbalimbali maishani, lakini baba yake aliona mwanawe alikuwa mbali na mambo hayo matano. Alipokumbuka, Hou Yuewen alisema, baba yake aliwahi kumsifu mara moja tu maishani mwake kwamba baba yake alipomsikia akiimba opera ya Kibeijing, alimsifu kwa kusema "sawa sawa!"
Bw. Hou Yuewen alianza kuonesha michezo jukwaani mwaka 1960, ameurithi moyo wa baba yake uliokuwa wa makini na usioridhika daima na kiwango chake cha usanii. Katika miaka ya 80 ya karne iliyopita, ambapo ngojela za kuchekesha zilikuwa zikipamba moto nchini China Bw. Hou Yuewen alikuwa msanii anayejulikana kwa wengi.
Bw. Hou Yuewen aliwahi kushiriki kwenye michezo mingi ya filamu na televisheni. Anaona kuwa kucheza katika filamu na televisheni kunamsaidia sana usanii wake wa mazungumzo ya kuchekesha.
Katika miaka 40 hivi, Bw. Hou Yuewen hakuwahi kuacha jukwaa lake na hakuacha juhudi zake za kufanya mageuzi na kutunga ngojela za kuchekesha. Katika miaka ya karibuni, kutokana na kuingiliwa na utamaduni wa ng'ambo nchini China, ngojela za kuchekesha zimezorota, na wanaojifunza sanaa ya mchezo huo wamepungua. Ili kurithisha sanaa hiyo, Bw. Hou Yuewen alipokea wanafunzi zaidi ya 20. Alisema,
"Kutokana na hali mbaya ya sanaa hiyo nimepokea wanafunzi. Hivi sasa wasanii wa ngojela wenye umri zaidi ya miaka 60 hadi 70 wanaendelea kuonesha michezo jukwaani kwa sababu wasanii wenye umri wa miaka zaidi ya 30 wako wachache, na hakuna wasanii wenye umri wa miaka zaidi ya 20. Kama tusipoharakisha kuwafundisha wachezaji vijana, pengo kubwa la wachezaji litatokea."
Bw. Hou Yuewen pia ana tumaini lingine, nalo ni kukamilisha tumaini la baba yake la kuandika "mitaala ya elimu ya ngojela za kuchekesha" ili kuviachia vizazi vijavyo urithi wa sanaa ya ngojela za kuchekesha. Bw. Hou Yuewen Anatoa wito kwa vyuo vikuu vya sanaa vianzishe somo la elimu ya michezo ya kuchekesha ili kustawisha sanaa hiyo.
Idhaa ya kiswahili 2005-03-10
|