Idara ya Afya ya mkoa wa Guizhou nchini China hivi karibuni imetoa "Maoni kuhusu matibabu ya wagonjwa wa Ukimwi", yakisema kuwa, watu wenye virusi vya Ukimwi kimsingi watatibiwa nyumbani kwao.
Kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa na Wizara ya Afya ya China kuhusu matibabu ya wagonjwa wa Ukimwi, idara ya afya ya mkoa wa Guizhou imeamua kuwa wagonjwa wa Ukimwi watibiwe kwa hiari, na kimsingi watibiwe nyumbani kwao.
"Maoni" yanasema kuwa idara za udhibiti wa maambukizi ya magonjwa zitatoa huduma za dawa, kuwaambia wagonjwa namna ya kutumia dawa na madhara yanayotokana na dawa zenyewe. Na wagonjwa ambao wanahitajika kulazwa hospitali lazima wapate kibali cha wataalamu zaidi ya wawili kwa saini. Idara za Afya kuanzia ngazi ya wilaya zinawajibika kuunda vikundi vya matibabu ya Ukimwi na kuwajibika kuandaa mpango wa matibabu. Kabla ya madaktari wa ngazi ya msingi kuwatibu wagonjwa lazima wawafahamishe mpango wa matibabu na wakati wa kutumia dawa, na kuwaambia uwezekano wa kutokea hali ya madhara ya dawa na kuanza kuwatibu baada ya wagonjwa kutia saini kwenye fomu ya "Kibali cha kutibiwa baada ya kufahamu matibabu ya Ukimwi". Mkurugenzi wa Ofisi ya Matibabu katika Idara ya Afya ya mkoa wa Guizhou Ruan Zhongjian alifafanua kuwa kwa sababu wagonjwa wengi wenye ugonjwa mwepesi na mzito wa kiasi wana uwezo wa kufanya kazi na kujitunza kimaisha, kwa hiyo matibabu yanaweza kufanywa nyumbani kwao.
|