Sehemu ya mtiririko wa kati na chini ya mto Changjiang ambayo ni mto wa kwanza kwa urefu nchini China ni moja ya maeneo makubwa ya ardhi oevu, ambayo ina idadi kubwa ya watu.
Ardhi oevu ni mfumo wa ikolojiaa wenye umaalum wa ardhi kavu na mtiririko wa maji, ardhi oevu ya kawaidi ikiwemo kinamasi, malisho, ufuko, maziwa na mito. Mkuu wa Idara inayoshughulikia hifadhi ya mfumo wa ikolojiaa nchini China yaani idara ya misitu ya China Bw. Zhou Sheng xian alieleza kuwa, hifadhi ya ardhi oevu ina maana muhimu kwa usalama wa ikolojia wa nchi fulani. Alisema:
"ardhi oevu, pamoja na misitu na bahari zinaitwa mifumo mitatu mikubwa ya ikolojia duniani, inafanya kazi muhimu katika kuhifadhi vyanzo vya maji, kusafisha maji, kulimbikiza maji kwa ajili ya matumizi katika wakati wa ukame, kurekebisha hali ya hewa na kuhifadhi aina mbalimbali za viumbe. Mfumo wa ardhi oevu unaofaa ni sehemu muhimu ya mfumo wa taifa wa usalama wa ikolojia na msingi muhimu wa maendeleo endelevu ya uchumi."
China ni moja ya nchi zenye aina nyingi za ardhi oevu duniani, ambayo ina hekta zaidi ya milioni 36 za ardhi oevu na kuchukua nafasi ya nne duniani. Ardhi oevu hiyo imesambaa kwenye maeneo matatu yaani uwanda wa juu wa Qinghai-Tibet, sehemu ya kusini magharibi ya mkoa wa Yunnan, mkoa wa Guizhou na sehemu ya mtiririko wa kati na chini ya mto Changjiang. Kwenye maeneo mawili ya uwanda wa juu wa Qinghai-Tibet na kusini magharibi ya mkoa wa Yunnan, China imejenga sehemu nyingi za hifadhi ya kimaumbele kwa ajili ya hifadhi ya ardhi oevu. Lakini njia hii dhahiri haifai kwa sehemu ya mtiririko wa kati na chini ya mto Changjiang yenye idadi kubwa ya watu.
Sehemu ya mtiririko wa kati na chini ya mto Changjiang ina maziwa mengi ambayo wanaishi samaki na ndege wa aina nyingi, na hali yake ya aina nyingi za viumbe inajulikana kote duniani. Lakini kwenye sehemu hiyo, uchumi umeendelea vizuri na kuna idadi kubwa ya watu, idadi ya wakazi wa sehemu hiyo, pato la jumla na uzalishaji wa mazao ya chakula zote zinachukua theluthi ya nchi nzima. Hivyo, kama sehemu za hifadhi ya ardhi oevu zikiwekwa kwenye sehemu hiyo, zitaweza kuathiri maendeleo ya uchumi na maisha ya wakazi wa huko. Hivyo katika muda mrefu uliopita, ardhi oevu katika sehemu hizo haikuweza kuhifadhiwa kwa hatua zinazofaa, na kusababisha eneo la ardhi oevu kupungua na mfumo wa ikolojia kuzidi kuwa mbaya kwa kasi zaidi.
Ili kushughulikia vizuri uhusiano kati ya hifadhi ya ardhi oevu na maendeleo ya uchumi, kuanzia mwaka 1999, serikali ya China ilianza kushirikiana na shirika la hifadhi ya maumbile duniani na kufanya jaribio la kuweka utaratibu mpya wa hifadhi ya ardhi oevu yaani usimamizi wa jumla wa sehemu ya mtiririko wa mto kwenye sehemu ya mtiririko wa kati na chini ya mto Changjiang.
Wakati wa kutekeleza utaratibu huo mpya, kwanza China ilichagua vijiji viwili mkoani Hubei na Hunan kufanya majaribio.
Ofisa mtendaji wa mfuko wa hifadhi ya maumbile duniani Bw. Li Li feng alimwambia mwandishi wa habari kuwa, baada ya majaribio hayo kuanzishwa, kazi yao ya kwanza itakuwa ni kuwataka wakulima kuacha vitendo vya kuzuia maji ya ziwa na kuanzisha mashamba, na kuhifadhi hali ilivyo ya ardhi oevu, na kuwasaidia wakulima hatua kwa hatua kutumia mbinu ya kisasa ya kiikolojiaa ya uzalishaji wa chakula. Alisema:
"mwanzoni ilikuwa vigumu sana, kwanza ni kubadilisha mtizamo wao. Sisi tuliwasaidia kwa fedha baadhi ya wakulima kufuga nguruwe, kuku na bata, pia tuliwaalika wataalamu wa kilimo kutoa mafunzo kwa wakulima. Kama vile kuwasaidia wafugaji wa samaki kuchagua samaki wenye thamani kubwa, na kuwafundisha teknolojia ya uvuvi wa kiikolojiaa na kuwaambia wasitumie kupita kiasi kemikali na madawa ya samaki, ili kuzuia uchafuzi wa maji."
Ili kupata uungaji mkono wa wakulima, idara husika pia zinazingatia kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu hifadhi ya ardhi oevu. Mwakilishi wa shirika la hifadhi ya maumbile duniani (World Wild Fund) nchini China Bw. Jim Harkness alieleza kuwa, katika miaka kadhaa iliyopita, shirika hilo liliwashirikisha wanafunzi wa vyuo vikuu kueneza mtizamo kuhusu hifadhi ya ardhi oevu kwenye sehemu za majaribio." Alisema:
"shughuli hiyo inalenga kuyashirikisha mashirikisho ya hifadhi ya mazingira kwenye vyuo vikuu katika kueneza mtizamo wa hifadhi ya ardhi oevu. Wanafunzi walikwenda sehemu hizo wakati wa likizo ya siku za joto kueneza ujuzi na kubadilishana maoni na wakazi wa sehemu hizo."
Habari zinasema kuwa, katika miaka 5 tangu mradi huo uanze kutekelezwa katika mikoa ya Hubei na Hunan, vijiji vinavyofanya majaribio vimepata manufaa makubwa ya kiuchumi na kiikolojiaa. Eneo la ardhi oevu lililopandwa mpunga hivi sasa limejazwa maji tena, na kuwa maskani ya samaki na ndege, pia mapato ya wakulima yameongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na mabadiliko ya njia za uzalishaji.
Habari zinasema kuwa, kuanzia mwaka 2005, China itatekeleza hatua kwa hatua utaratibu wa usimamizi wa jumla wa maeneo ya mtiririko wa mto kwenye sehemu nyingine ili kuhifadhi kihalisi eneo kubwa zaidi la ardhi oevu.
Idhaa ya Kiswahili 2005-03-23
|