Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-24 16:50:57    
Mwanadiplomasia wa China aliyewafahamisha wachina ngano za Finland Bw. Du Zhongying

cri

Usiku mmoja wa mwishoni mwa mwaka jana, balozi wa Finland nchini China Bwana Bassin aliandaa tafrija maalum katika makazi yake. Kwenye tafrija hiyo, Bw. Bassin alimkabidhi mzee wa China Bw. Du Zhongying nishani iliyotolewa na rais wa Finland. Hii ni mara ya kwanza kwa rais wa Finland kumtunukia nishani mchina.

Bw. Du Zhongying mwenye umri wa miaka 73 mwaka huu, aliwahi kufanya kazi katika ubalozi wa China nchini Finland, pia aliwahi kuwa balozi wa China nchini Vanuatu na Kiribati. Kabla ya miaka 52 iliyopita, Bw. Du Zhongying baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Beijing alijiunga na wizara ya mambo ya nje ya China. Muda si mrefu baadaye alitumwa kufanya kazi katika ubalozi wa China nchini Finland. Kuanzia wakati huo Bw. Du alikuwa na uhusiano asioweza kuuacha na nchi hiyo. Alisema:

"Nilifurahi sana kutumwa kufanya kazi nchini Finland kwa sababu mimi naipenda sana nchi hiyo. Maana ya maneno ya Finland kwa kichina ni aina ya maua fulani yanayonukia na maua hayo ni maua yanayopendwa na wakazi wa maskani yangu."

Bw. Du Zhongying alianza maisha yake ya kidiplomasia nchini Finland kwa hisia hiyo nzuri, na kwa ujumla aliishi nchini Finland kwa miaka 15. Ili kufanya vizuri kazi yake, muda si mrefu baada ya kufika Finland, Bw. Du alianza kujifunza lugha ya Finland na kusoma vitabu vya fasihi vya nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na ngano.

"Niliona kuwa, ngano za Finland zina umaalum wake, yaani zinaainisha dhahiri mambo mema na mabaya, ambazo zinasaidia kuwaelimisha watoto. Wakati huo nilifikiri kuwa, kama nikiwa na wakati nitazitafsiri kwa kichina ili kuwafahamisha watoto wa China."

Lakini Bw. Du alikuwa ana kazi nyingi sana, licha ya kufanya kazi nchini Finland, yeye pia aliwahi kufanya kazi katika ujumbe wa China katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, na kuwa balozi wa China katika Jamhuri ya Vanuatu na Kiribati. Hivyo ilipofika mwaka 1994 baada ya kustaafu, Bw. Du Zhongying ndipo alipoanza kutafsiri ngano za Finland kwa kichina.

Ili kuharakisha kazi yake ya kutafsiri ngano za Finland kwa kichina, Bw. Du aliacha shughuli nyingi za kijamii, na kujitumbukiza kabisa katika dunia ya ngano za Finland. Kutokana na msaada wa mke wake aliyefahamu kidogo lugha ya kifinland, kitabu cha kwanza cha kichina cha ngano za Finland kilichapishwa miaka minne baadaye.

Bw. Du alifurahi kuona kuwa, ngano alizotafsiri zinakaribishwa sana na wasomaji watoto wa China, alisema:

"Watoto wengi wanakipenda kitabu hicho, mjukuu wa rafiki yangu siku chache zilizopita alinipigia simu akiniuliza lini nitaweza kutafsiri kitabu kingine cha ngano za Finland? Aliniambia kuwa, anapenda sana hadithi za ngano za Finland, jambo hilo linanifurahisha sana."

Licha ya "ngano za Finland", Bw. Du Zhongying pia alitafsiri kwa kichina vitabu vingi kuhusu fasihi ya Finland vikiwa ni pamoja na "Jukumu huko Belgrade" kilichoandikwa na rais wa zamani wa nchi hiyo Bwana Martti Ahtisaari na "mkusanyiko wa riwaya fupi wa Finland".

Juhudi za Bwana Du si kama tu zinakaribishwa na wasomaji wa China, bali pia zinaheshimiwa na Finland. Ili kusifu juhudi alizozifanya katika kuhimiza uhusiano wa kirafiki kati ya Finland na China, mwezi Septemba mwaka 2004 rais wa Finland Bwana Tarja Halonen alimtunukia nishani ya ushujaa. Balozi wa Finland nchini China Bwana Bassin alisema:

"Bwana Du ametafsiri kwa kichina vitabu vingi vya fasihi ya Finland, kazi yake ni muhimu sana katika kuwasaidia wachina wafahamu mambo ya Finland. Shughuli alizofanya zinasaidia sana katika kuimarisha maelewano ya kimataifa."

Hivi sasa Bw. Du Zhongying ameanza kutafsiri kwa kichina kitabu kingine cha ngano za Finland. Mzee huyo aliyeshughulikia mambo ya kidiplomasia kwa maisha yake yote alisema kuwa, kutafsiri fasihi ya Finland kwa kichina ni kazi yake muhimu baada ya kustaafu, ameamua kuendelea kutoa mchango wake katika kuhimiza kadiri awezavyo maelewano na maingiliano ya kiutamaduni kati ya watu wa China na wa Finland.

Idhaa ya kiswahili 2005-03-24