Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-24 21:22:17    
Mji wa Nanjing

cri

Mji wa Nanjing ambao ni mji mkuu wa Mkoa wa Jiangsu unaitwa Ning kwa kifupi. Mji huo uko kwenye tambarare ya sehemu ya chini ya Mto Changjiang na sehemu ambayo yenye nguvu kubwa ya kiuchumi nchini China yaani Delta ya Mto Changjiang. Umbali kutoka kwenye mji huo hadi mji wa Shanghai ni kilomita 300, ni kilomita 1200 hadi Beijing, na kilomita 1400 hadi Chongqing.

Hali ya hewa ya mji wa Nanjing ni ya pepo za misimu ya ukanda wa semitropiki ya kizio cha kaskazini. Kuna majira manne, mvua nyingi na maliasili ya kutosha ya nishati ya mwanga wa jua. Wastani wa joto kwa mwaka ni nyuzi 15.7 sentigredi. Kwa wastani mvua inanyesha kwa siku 117 kila mwaka. Katika majira ya joto upepo huvuma kutoka upande wa kusini mashariki, na katika majira ya baridi upepo huvuma kutoka upande wa kaskazini magharibi. Mwishoni mwa mwezi Juni hadi katikati ya mwezi Julai ni kipindi cha masika. Na mwezi Septemba hadi mwezi Novemba katika majira ya Autumn ni kipindi chenye hali ya hewa nzuri mjini humo.

Eneo la Mji wa Nanjing ni kilomita za mraba 6598. Katika mji huo kuna maliasili nyingi za kimaumbile. Hivi sasa aina zaidi ya 40 za madini zimegunduliwa mjini Nanjing. Miongoni mwa madini hayo, kiasi cha madini ya chuma na salfa yaliyogunduliwa kinachukua asilimia 40 ya madini yote. Na kiasi na ubora wa madini ya Strontium ni cha juu katika sehemu ya Asia Kusini Mashariki. Maliasili ya maji chini ya ardhi ni nyingi tena ni yenye ubora wa juu. Chemchemi za maji ya madini katika wilaya za Jiangning, Jiangpu na Pukou ni maarufu zaidi.

Mjini humo kuna milima, mito na misitu mizuri ambayo imeufanya mji huo uwe na mandhari nzuri. Mji wa Nanjing ni mji maarufu wa kitalii nchini China. Kutokana na sehemu nzuri ya kijiografia na mandhari nzuri, mji huo ulisifiwa na wanasiasa, wanajeshi na wasomi wengi mashuhuri katika historia ya China. Hivi sasa mji huo umekuwa ni kituo muhimu chaa viwanda vya aina mbalimbali, usafirishaji na mawasiliano katika sehemu ya mashariki ya China, kimoja kati ya vituo vinne vya utafiti wa sayansi na elimu nchini China na mji mkubwa wa pili wa kibiashara mashariki mwa China baada ya Shanghai.

Mji wa Nanjing ni mji maarufu wenye historia ndefu na utamaduni mkubwa ambao ni mmoja kati ya miji mikuu 7 ya kale katika historia ya China. Kuanzia karne ya 3 mji wa Nanjing ulikuwa mji mkuu wa enzi na mamlaka 5 ambazo zimeupatia mji huo urithi mwingi wa kiutamaduni.

Jina la Nanjing lilianza kutumika mwanzoni mwa Enzi ya Ming, kabla ya hapo mji huo uliwahi kuitwa Jinlin, Jian'ye, Jiankang, Jiangning, Yingtian n.k. Baadaye katika Enzi ya Qing ulibadilishwa jina na kuitwa Jiangning. Na baada ya mapinduzi ya Xinhai yaliyotokea mwaka 1911 ulianza kutumia jina la Nanjing hadi sasa.

Idhaa ya Kiswahili 2005-03-08