Tangu zamani, mahusiano baina ya binadamu na mianzi yalikuwa makubwa. Sanaa ya uchongaji wa mianzi ilianza kutokea katikati ya Enzi ya Ming ya karne ya 15 nchini China, na imekuwa ikiendelea kuboreshwa mpaka sasa, na katika muda huu wote wamejitokeza wasanii wengi hodari katika sanaa hiyo.
Bwana Zhou Hansheng alihitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Sanaa cha Guangzhou. Hivi sasa, anafanya kazi katika kitivo cha sanaa cha Chuo Kikuu cha Jianghan, mjini Wuhan. Huyu bwana ni hodari sana wa kuchonga mianzi. Hakurithi tu ufundi wa wasanii wa zamani, bali pia amebuni njia mpya za uchongaji.
Hebu tutoe mfano wa sanamu ya ajabu aliyochonga ya "Sufii Lu Zhishen". Katika kumchonga sufii huyu kwenye kipande cha mwanzi maajabu aliyoyafanya ni kuupindua mwanzi juu chini, na kutumia mizizi, yake kama masharubu ya sufii. Hakika huo ni ubunifu wa aina yake! Suffi anaonekana amesimama, amevaa joho lakini kitambi kinaonekana wazi, mguu mmoja ameukunja na kukanyaga jiwe; kichwani amevaa kitu kama duara la chuma, shingoni amevaa ukoja ulioteremka hadi kifuani; mkono wa kulia unaelekea ardhini; na macho ameyatoa kwa ukali. Sanamu hii inadhihirisha vizuri tabia ya sufii Lu ya unyoofu na ushujaa wa kuthubutu kulipa kisasi.
Michongo ya mianzi inagawanyika katika aina tatu: ya mviringo, ya kuingia ndani na ya kujitokeza nje. Sanamu ya Sufii Lu Zhishen ni ya mchongo wa mviringo. "chombo cha kuwekea kalamu cha dimbwi la mayungiyungi" ni ya mchongo unaojitokeza nje. Kabla ya kuchonga, msanii anaondoa sehemu ya mwanzi ya usoni kwa kisu, kisha anachonga nakshi kwenye sehemu iliyobaki. Bw. Zhou alichonga mandhari ya kupendeza ya dimbwi, kando yake kuna mvulana anachunga ng'ombe.
" Kitambaa cha kubebea mtoto" ni mchongo mwingine wa mviringo wa Bw. Zhou, unatumia pingili mbili za mwanzi. Mchongo wa mviringo katika pingili moja ya mwanzi ni uvumbuzi wa Bw. Zhou. Katika mchongo wa "Kitambaa cha kubebea mtoto", mtoto mchanga anaonekana amelalia kitambaa, amefumba macho, na midomo yake inaelekea kutaka kufumbuka. Kichwa cha mtoto huyu ni cha upara mwororo unaong'ara na kupendeza kiasi kwamba watu wangetaka kukipapasa. Michongo mingine mizuri ya Bw. Zhou ni "Msichana wa Tibet anayechana nywele", "Msichana Mmiao aliyejipamba", "Mtoto aliyevaa viatu vya kichwa cha chui" n.k.. michongo hiyo imefikisha sanaa ya uchongaji wa mianzi kwenye kiwango kipya cha juu.
Idhaa ya Kiswhili 2005-03-25
|